Kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wapya wamekuwa wanafanya ni kutaka siku ya kwanza ya biashara wawe na wateja wengi, waliopanga foleni kusubiri kuhudumiwa. Hilo halijawahi kutokea, hivyo achana nalo, kama ndiyo unaanza biashara au unapanga kuanza biashara.

Hata kama watu wanakuahidi kiasi gani kwamba watanunua kwako, ukweli unaupata unapoanza biashara, hutawaona. Hii ni hali ambayo inakatisha tamaa, na kuona labda kuna kosa kubwa ambalo umefanya. Hakuna kosa umefanya, ila unachofikiria kufanya ndiyo kinatengeneza kosa.

Unapokazana kumfikia kila mtu awe mteja wako, tena kwa haraka na siku za mwanzo za biashara, ndiyo kosa kubwa unaloweza kufanya na likakuondoa kabisa kwenye biashara.

Badala ya kufanya kosa hilo, anza kujenga biashara yako mteja mmoja baada ya mwingine. Namaanisha kutengeneza mteja mmoja mmoja. Ndiyo hata kama ndoto zako ni kuwa na biashara kubwa, lazima uanze na mteja mmoja.

Sasa unachofanya, ni kuchagua mteja mmoja ambaye utampa huduma au bidhaa ambazo zitamwezesha kuwa na maisha bora zaidi, kwa kutatua changamoto zake na kumpa mahitaji yake. Kisha mteja huyu anaporidhika, unaweza kumtumia kuwafikia wateja wengine wengi zaidi. Kwa sababu yeye mwenyewe atakuwa tayari kuwashirikisha wengine kuhusu biashara yako. Na hutahitaji kuweka nguvu kubwa kwa wateja hao wanaoletwa.

SOMA; Teknolojia Pekee Mteja Anayojali Kwenye Biashara Yako Ni Hii.

Sasa fikiria unamhudumia mteja mmoja, ukifanikiwa vizuri anakuwezesha kuwafikia wateja watano, wale watano nao wanakufikisha kwa wateja wengi. Utaona ni jinsi gani njia hii ina nguvu, kuliko kukazana kumfikia kila mtu kwa wakati mmoja.

Kwa njia hii unahitaji kuweka juhudi za kutosha, unahitaji kuweka muda, unahitaji uvumilivu. Na ninachojua mpaka sasa, hakuna mafanikio ambayo yanakuja bila ya vitu hivyo muhimu.

Mteja mmoja baada ya mwingine, njia bora ya kutengeneza wateja wa kudumu kwenye biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog