Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku mpya ya wiki mpya, tunayo nafasi nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KILICHOKUFIKISHA HAPO ULIPO SASA.
Iko hivi rafiki, hujafika hapo ulipo sasa kama ajali, wala siyo bahati.
Wala haijatokea tu wewe ukajikuta hapo ulipo sasa.
Bali umetengeneza njia ya kukufikisha hapo ulipo sasa, wewe mwenyewe, kwa kujua au kutokujua.
Umefika hapo ulipo sasa, kutokana na fikra ambazo zimetawala akili yako na hatua unazochukua.
Kama upo kweye kazi iliyokwamba, ambayo huoni mbele, ni kwa sababu fikra zako zimekwama hapo, na hatua unazochukua ni za kuendelea kulinda kazi hiyo.
Kama upo kwenye biashara ambayo haikui, ni kwa sababu fikra zako juu ya biashara hizo ni kwenye udogo pekee, na hatua unazochukua ni ndogo sana.
Habari njema ni kwamba, kutoka hapo ulipo ni rahisi, na kinachohitajika ni kubadili fikra zako na kuboresha hatua unazochukua.
Anza kuwa na fikra chanya na kufikiri makubwa kweye chohote unachofanya kwenye maisha yako.
Pia chukua hatua kubwa sana, ili uweze kupata matokeo bora kabisa kwenye maisha yako.
Itakuwa jambo la kushangaza, iwapo utaendelea kufikiri na kufanya kama ulivyokuwa unafanya siku za nyuma, halafu utegemee matokeo tofauti. Ni kitu ambacho hakiwezekani na utapoteza muda wako na kulaumu watu bure.
Tengeneza fikra sahihi na chukua hatua kubwa, hivyo vitakufikisha mbali zaidi.
Nakutakia siku njema sana ya leo, nenda kafikiri vyema na uchukue hatua kubwa.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info