Ni rahisi sana kufikiria kwamba adui mkubwa wa biashara yako ni washindani wako. Hivyo kuangalia namna ya kuwashinda na kuwaangusha ili uweze kufanikiwa kwenye biashara hiyo.

Hapo ndipo wengi wanapokosea, kwa sababu wanajaribu kupambana na mtu ambaye siyo sahihi. Hivyo hata wapambane kiasi gani, bado hilo haliwasaidii.

Kabla hujafikiria kwamba mshindani wako ndiye adui yako kibiashara, jiulize kwa nini wateja wanaenda kwa mshindani wako? Na sababu itakuwa wazi kabisa, kuna kitu wanakipata kwa mshindani wako, ambacho hawakipati kwako. Kuweza kufikiria hivi, ni ushindi mkubwa sana kwa biashara yako.

Sasa kama kipo kitu, ambacho wateja wanakipata kwa mshindani wako, ila hawakipati kwenye biashara yako, nani atakuwa adui wa biashara yako? Ni wewe mwenyewe. Ndiyo, yaani wewe mwenyewe ndiye adui mkubwa wa biashara yako.

Wewe kama mmiliki wa biashara, unayeendesha biashara yako, ndiye adui mkubwa wa biashara hiyo. Uvivu wako ndiyo uadui mkubwa kwa biashara yako. Kusahau kwamba kazi yako kubwa ni kumridhisha mteja ni uadui mkubwa kwa biashara yako.

SOMA; Uongo Huu Unaojiambia Kila Siku, Ni Adui Mkubwa Wa Mafanikio Yako.

Biashara yoyote unahitaji kutatua changamoto za wateja, kuwapa kile ambacho wanahitaji na kwa njia ambayo ni bora kwao. Kwa namna hiyo, wateja wataendelea kuja kwenye biashara yako.

Hivyo badala ya kupoteza muda kupambana na washindani wa kibiashara, badala ya kupoteza muda kuangalia wengine wanafanya nini, weka muda huo kuangalia mteja wako anataka nini na mpatie. Wahudumie wateja wako vizuri sana na wataendelea kuja kwenye biashara yako.

Acha kuwa adui wa biashara yako wewe mwenyewe, weka juhudi za dhati kuhakikisha mteja anapata kwako kitu ambacho hawezi kupata sehemu nyingine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog