Moja ya changamoto kubwa kwa kila mtu ni muda, kwa sababu muda upo kwa kiwango kile kile kwa siku. Huwezi kukopa muda, lakini pia ukishapoteza muda, huwezi kuupata tena.Vimeandikwa vitabu vingi sana kuhusu muda, imetengenezwa mifumo mingi sana ya kutumia muda vizuri, lakini changamoto bado ni kubwa, na inaendelea kubwa kila siku. 

Moja ya vitu ambavyo vinakuza changamoto hii, ni maendeleo ya teknolojia, ambayo yanaongeza mambo ya kufanya, huku muda ukiwa ni ule ule.

Sasa hivi tuna simu ambazo zina kila kitu, kuanzia simu, ujumbe, mitandao ya kijamii, email na kadhalika. Kwa kifupi simu yako pekee inaweza kuwa adui yako namba moja kwenye matumizi mazuri ya muda.

Watu wengi wamekuwa na mipango ya kufanya, lakini hawaifanyi kutokana na tabia ya kuahirisha mambo (procrastination). Tabia hii inawafanya wengi kushindwa kufanikiwa na hata kupoteza muda wao.

Mwandishi Rory Vaden anatuambia kwamba, tabia ya kuahirisha mambo, iwapo itatumiwa vizuri basi inatuwezesha kuwa na matumizi mazuri ya muda wetu na hata kuuzidisha.

Mwandishi amefanya utafiti wa kuwafuatilia watu wenye mafanikio makubwa licha ya kuwa na mambo mengi ya kufanya, na amegundua wao siyo kwamba wanatunza muda, bali wanazidisha muda. Wanahakikisha wanakuwa na muda mwingi kuliko watu wengine.
Unaweza kujiuliza hilo linawezekanaje iwapo muda wa siku ni ule ule kwa kila mtu, ambao ni masaa 24? Mwandishi hapa ametupa siri kubwa sana. Siri hiyo ni kwamba, wale wenye mafanikio, wamekuwa wakizidisha muda wao kwa kuchagua vizuri yale wanayoyafanya. Wamekuwa wakifanya mambo leo, ambayo yatawatengenezea muda zaidi kesho.

Mwandishi anatuambia kwamba, changamoto ya muda kwa wengi ni kutaka kufanya kila kitu. Wanaweka umuhimu kwenye kila kitu na hivyo kushindwa kufanya jambo lolote kwa mafanikio. Anatufundisha namna ya kutengeneza kipaumbele muhimu na kufanyia kazi.

Kupitia kitabu hichi cha Procrastinate on purpose, mwandishi anatushirikisha ruhusa tano ambazo kila mmoja wetu anapaswa kujipa ili aweze kutengeneza muda zaidi kwenye maisha yake na kuweza kufanikiwa.

Karibu twende pamoja kujifunza ruhusa hizi tano na jinsi ya kuzitumia. Ruhusa hizi zinaenda kwa mwendelezo, ni kama hatua, hivyo lazima upitie zote, moja baada ya nyingine mpaka ufikie kile muhimu kwako kufanya.

RUHUSA YA KWANZA; ONDOA NA PUUZIA MAMBO YASIYO MUHIMU.

Hii ni ruhusa ya kwanza unayopaswa kujipa, ruhusa ya kupunguza mambo ambayo siyo muhimu kwako, li upate muda wa kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi.

1. Changamoto kubwa ya muda kwa watu wengi inatokana na kuwa na mambo mengi ya kufanya, ambayo siyo muhimu. Wengi hufikiri kufanya mambo mengi ndiyo mafanikio. 

Hivyo hukazana na mambo yasiyo muhimu na kukosa muda wa kufanya yale muhimu.

2. Hatua ya kwanza kabisa ya kuweza kuzidisha muda wako ni kuanza kuangalia mambo gani ambayo unayafanya kwenye maisha yako sasa hivi, ambayo unaweza kuacha kuyafanya na kusiwe na madhara yoyote kwenye maisha yako.

3. Ili uweze kupunguza mambo kwenye maisha yako, lazima uwe tayari na usiogope kusema neno HAPANA. Neno hapana litakupa uhuru mkubwa sana kwenye maisha yako. 

Lakini wengi wetu tunaogopa kulitumia tukiona wengine watatuchukulia tuna roho mbaya au hatujali. Hivyo tunakubali kila kitu na kushindwa kufanya yale muhimu. Kama jambo siyo muhimu, sema HAPANA, na tumia lugha nzuri kusema hivyo.

4. Usiposema hapana unakuwa pia umechagua kusema hapana. Watu wengi hufikiri wakisema ndiyo basi wameepuka kusema hapana. Ukweli ni kwamba unaposema ndiyo kwenye jambo moja, maana yake umesema hapana kwenye jambo jingine. Ukisema ndiyo kwenye mambo ya wengine, maana yake umesema hapana kwenye mambo yako. Sasa pima mwenyewe wapi panahitaji ndiyo na wapi panahitaji hapana.

5. Wakati mwingine unahitaji kuacha kufanya mambo, bila hata ya kutoa sababu au maelezo kwa mtu yeyote. Unaacha tu kufanya, na unatumia muda huo kufanya yale muhimu zaidi.

RUHUSA YA PILI; WEKEZA MUDA WAKO KWA KUTAFUTA MIFUMO YA KUKUSAIDIA.

Hapa unajipa ruhusa ya kutumia mifumo mbalimbali kutekeleza baadhi ya majukumu yako, ili wewe upate muda zaidi wa kufanya yale muhimu.

6. Kila kitu ambacho unachagua kufanya na muda wako, unawekeza muda huo. Swali ni je unawekeza muda huo kwenye nini? Kwa sababu kila uwekezaji una gharama na faida zake. Ukiwekeza vizuri unapata faida, ukiwekeza vibaya unapata hasara.

7. Kitu chochote unachofanya ambacho kinapoteza muda wako, ni sawa a kuchagua kupoteza fedha zako. Lakini ukipoteza fedha unaweza kuzipata, ila muda haurudi tena. 

Hivyo pima matumizi yako ya muda kama uwekezaji, na kuwekeza maeneo ambayo yatazalisha zaidi baadaye.

8. Tumia mifumo ambayo itakuokolea muda wako. Sasa hivi tunaishi kwenye dunia ambayo unaweza kurahisisha mambo mengi. Kitu chochote ambacho kinaweza kufanywa na teknolojia, usifanye wewe mwenyewe, ni kupoteza muda wako. Kwa mfano, badala ya kuingia kwenye kila mtandao wa kijamii na kuandika unachotaka kuandika, unaweza kutumia programu moja inayopeleka ujumbe wako kwenye mitandao yote ya kijamii unayotumia.

9. Ukiwa mdadisi, utaona namna unavyoweza kutengeneza mfumo wa kurahisisha mambo mengi unayofanya. Mfano kutuma ujumbe wa simu, kulipa gharama mbalimbali, kutuma email na kadhalika. Wekeza kwenye mfumo ambao unaokoa muda wako.

RUHUSA YA TATU; WAPE WATU WENGINE MAJUKUMU YAKO.

Hii ni ruhusa ya kuwapa watu wengine majukumu yako wayafanye. Kitu chochote unachofanya sasa, ambacho kinaweza kufanyika na mtu mwingine, kwa gharama kidogo, kukifanya ni kupoteza muda wako.

10. Ili kuweza kugatua majukumu yako na kuwapa wengine, unahitaji kujua marejesho ya uwekezaji wa muda wako, kwamba ukiweka muda wako mahali unapata kiasi gani. Pia unahitaji kujua thamani ya muda wako, kwamba saa yako moja inagharimu kiasi gani. 

Kujua thamani ya muda wako, chukua kipato chako cha mwezi, kisha gawa kwa siku unazofanya kazi kwenye mwezi na masaa unayofanya kazi. Kwa mfano kama kipato chako kwa mwezi ni milioni tatu, na unafanya kazi siku sita za wiki, kwa wiki nne ni siku 24, kama kila siku ya kazi unafanya kazi masaa 10, basi kwa mwezi utafanya kazi masaa 240. Hapo sasa chukua milioni tatu gawa kwa 240 utapata 12,500/= hii ina maana kwamba, kila saa yako moja ya kazi ina thamani ya 12,500/=. Hivyo ukitumia saa moja ya kazi kufanya kitu ambacho unaweza kumpa mtu mwingine akakifanya kwa chini ya kiasi hicho, unapoteza muda wako.

11. Watu wengi wamekuwa wakisema hawawezi kutoa majukumu yao kwa wengine kwa sababu hawana uwezo wa kuwalipa. Lakini ukweli ni kwamba, watu huwa hawapigi mahesabu. Wakipiga mahesabu vizuri, wataona namna wanavyopoteza fedha nyingi kuliko wanazodhani wanaokoa.

12. Hofu kubwa, ambayo wengi huwa hawaisemi inayowazuia kuwapa watu wengine majukumu yao, ni kufikiri kwamba hawawezi kuyafanya vizuri kama wanavyoyafanya wao. Na hilo linaweza kuwa kweli kabisa, lakini unapaswa kujipa ruhusa ya kuwapa watu majukumu hayo na kujipa ruhusa ya kukubali matokeo ya kawaida, hasa mwanzoni.

13. Unapokwepa kuwalipa watu wengine kwa viwango vyao, unajilipa wewe mwenyewe viwango vyao hivyo. Kwa mfano kama saa yako moja ya kazi ina thamani ya shilingi elfu 10, halafu unakazana kufanya kitu ambacho ungeweza kumpa mwingine akakifanya kwa shilingi elfu 5, wewe unakuwa umeamua kujilipa elfu 5 kwa saa badala ya elfu kumi.

14. Kazi zozote unazofanya, ambazo wengine wanaweza kuzifanya, tafuta wa kuzifanya, wewe weka muda wako kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi, ambayo wewe pekee ndiye unayeweza kuyafanya.

RUHUSA YA NNE; JIRUHUSU KUAHIRISHA.

Baada ya kuondoa yale ambayo hayana umuhimu kabisa, ukajengea mfumo yale yanayofaa kuwa kwenye mfumo na kuajiri wengine kukusaidia yale ambayo yanaweza kufanyika na wengine, unakuwa umebaki na yale ambayo wewe pekee ndiye unaweza kuyafanya. Hapa sasa una hatua mbili za kuchukua; kufanya sasa au kufanya baadaye. 

Hapo unaangalia kile muhimu zaidi unakifanya sasa, na kile kinachoweza kusubiri unakifanya baadaye.

15. Kila jambo lina muda wake maalumu wa kulifanya. Epuka kuwahi sana kufanya jambo, inakugharimu, pia epuka kuchelewa kufanya jambo, itakugharimu. Jua wakati sahihi kwako kufanya kila jambo, na ukiweza hivyo, utaweza kutumia muda wako vizuri.

16. Jifunze kuwa na subira. Dunia ya sasa ni ya kutaka kila kitu kitokee kwa wakati ambao tunataka sisi kitokee. Lakini mambo huwa hayawi hivyo, unahitaji kuwa na subira, uahirishe yale mambo ambayo wakati wake bado.

17. Chagua kuahirisha mambo ambayo yanaweza kusubiri. Japokuwa lengo lako ni kuchukua hatua, huwezi kuchukua hatua sawa kwenye kila jambo. Bali jua wakati sahihi wa kuchukua hatua, na ahirisha jambo mpaka wakati wake sahihi.

18. Kuna makundi mawili ya watu, wapo wale wenye hofu ya kuchelewa, na hivyo hufanya mambo haraka na mapema, hawa kuingia gharama ya kurudia kufanya mambo. 

Kundi la pili ni wale wanaosubiri mpaka muda wa mwisho wa kufanya ufike, huwa wanachelewa kufanya na kupata gharama ya adhabu ya kuchelewa. Wewe unapaswa kuwa mtu wa kufanya jambo, kwa wakati wake, bila kuwahi sana na wala usichelewe.

RUHUSA YA TANO; WEKA NGUVU NA LIND AKILE UNAFANYA.

Ukishajua kipi kinaweza kusubiri, sasa unabaki na kile ambacho unapaswa kufanya, na unapaswa kukifanya sasa. Kile ambacho wakati wake umefika. Na hichi pekee ndiyo kinapaswa kutumia muda wako. Kingine chochote tofauti na hicho ni usumbufu.

19. Ili kuzidisha muda wako, fanya kazi kubwa kwenye muda mfupi, ili kupata muda mwingi wa kuwa huru. Yaani unapaswa kuweka kazi kubwa ndani ya muda mfupi, kwa kuweka nguvu zako kwenye kitu kimoja, baada ya kukimaliza unakuwa na muda mwingi wa kuwa huru.

20. Unahitaji kuwa na kipaumbele ambacho unakifanyia kazi. Kipaumbele hicho ndiyo kinachochukua muda wako pekee, vitu vingine vyote unaachana navyo, kwa kuacha kabisa, kutengenezea mfumo, kuwaajiri wengine wakusaidie au kwa kuvisubirisha.

21. Ili uweze kusimamia kipaumbele chako, usitake kumridhisha kila mtu. Usitake kuwaambia watu ndiyo kwenye mambo yao, halafu mambo yako yakakwama.

22. Njia bora kabisa ya kuwaheshimu watu wengine, ni kuwa wewe, kwa kufanya yale muhimu kwako. Kuwakubalia kila kitu kwa sababu tu unataka kuwaonesha unawaheshimu, halitakusaidia wewe wala wao.

Tumia ruhusa hizi tano ili kuweza kutengeneza muda zaidi kwako, muda ambao utakuwezesha kufanya yale muhimu kabisa na kukupa muda zaidi wa kuwa huru na kufanya yale ambayo unapenda kufanya.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita