Rafiki yangu mpendwa,
Mipango ni rahisi sana, kila mtu anapanga na msimamishe mtu yeyote njiani na muulize mipango yake ni ipi, atakupa mipango mizuri sana.
Pamoja na kila mtu kuwa na mipango mizuri, ni wachache sana ambao wanaweza kufanyia kazi mipango hiyo na ikawa uhalisia kwenye maisha yao. Wengi wamekuwa wanabaki na mipango tu, lakini haiwi uhalisia.
Kinachowazuia wengi kutekeleza mipango waliyonayo ni tabia ya kuahirisha mambo. Hii ni tabia ambayo ni asili yetu sisi binadamu, huwa hatupendi kufanya chochote ambacho kinatuumiza au kinataka tuweke kazi.
Huwa tunapenda kutumia muda wetu kwa vitu visivyo na maana. Kwa muda ule ule na kwa nguvu zile zile, huwa tunaona ni bora kutumia kufanya vitu ambavyo vitatupa raha ya muda mfupi, kuliko kufanya vitu ambavyo havina raha ya muda mfupi lakini kwa muda mrefu vina maana.
Kinachowatofautisha wale wanaopata mafanikio makubwa kwenye maisha yao na wale wanaoshindwa siyo bahati wala akili wala fursa. Kinachowatofautisha ni namba wanavyoweza kuishinda tabia ya kuahirisha mambo. Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wanakuwa kwenye mazingira sana, wanakutana na fursa sawa, lakini wale wanaoshindwa huwa wanasubiri wakati wanaofanikiwa wanachukua hatua.
Wanaofanikiwa wanachukua hatua siyo kwa sababu wao hawana kabisa tabia ya kuahirisha mambo. Wanayo sana, ila wamejifunza njia za kuishinda tabia hiyo na kuweza kuchukua hatua.
Ni njia hizo za kuishinda tabia ya kuahirisha mambo utakwenda kujifunza leo, na kama utaanza kuzifanyia kazi leo, basi siku zijazo utajishukuru sana kwa hatua hizo ulizoanza kuchukua leo.
Karibu tujifunze njia tano za kuishinda tabia ya kuahirisha mambo na kuweza kufanya kila ulichopanga kwa wakati wake.
Moja; TENGENEZA ORODHA YA VITU VYA KUFANYA.
Watu wengi pamoja na kuwa na mipango mizuri, hawana njia ya kujipima kwenye utekelezaji wa mipango yao. Mipango hiyo huwa inakaa kwenye fikra zao na wao kukazana na siku zao. Siku inaisha, wanakuwa wamechoka lakini hawajui kama wametekeleza kile walichotaka kutekeleza. Kwa kuiendesha siku yako hivi, ni rahisi sana kutokufanya yale muhimu, kwa sababu kelele za siku zinapoanza, ni rahisi sana kusahau yale muhimu.
Njia bora ya kuepuka hili ni kutengeneza orodha ya yale muhimu ya kufanya kwenye kila siku yako. Unapoamka asubuhi, fikiria mipango yako yote muhimu uliyonayo, kisha orodhesha vitu utakavyofanyia kazi siku hiyo. Tembea na orodha yako popote uendapo na unapotekeleza jambo lililopo kwenye orodha weka alama ya vema. Endelea hivyo kwa mambo mengine yaliyopo kwenye orodha.
Lengo lako kwa siku ni kutekeleza angalau asilimia 80 ya yale uliyopanga kutekeleza kwenye siku husika. Kwa kutumia njia hii, siyo rahisi kelele za siku kukusahaulisha yale muhimu.
Mbili; KUWA NA TANO ZA SIKU.
Kila siku unayoianza, ainisha mambo matano muhimu ambayo ukiyafanya siku hiyo yatakusogeza karibu na mafanikio unayotaka kuyafikia. Mambo hayo matano unapaswa kuyafanyia kazi bila ya kujali mazingira yapoje. Inyeshe mvua au liwake jua, hayo matano ni muhimu kwa siku yako na unapaswa kuyafanyia kazi.
Kwa kuwa na tano za siku, unajiweka kwenye nafasi ya kutekeleza yale muhimu na kuepuka kupotezwa na kelele ambazo zimekuzunguka kila mahali.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Procrastinate On Purpose (Ruhusa Tano Za Kujipa Ili Kuzidisha Muda Wako).
Tatu; TENGENEZA UKOMO WA MUDA.
Mtu mmoja amewahi kusema kwamba jukumu huwa linachukua muda uliopangwa lifanyike. Akimaanisha kama kuna jukumu ambalo linapaswa kufanywa kwa masaa mawili, litakamilika ndani ya masaa mawili. Jukumu hilo hilo likipangwa kufanyika ndani ya masaa matano, litachukua masaa matano.
Huwa tunasukumwa kufanya zaidi pale ambapo muda unakuwa mdogo, na tunaahirisha mambo pale muda unapokuwa mwingi. Ndivyo maana wanafunzi ni vigumu sana kusoma siku za kawaida, lakini mtihani unapokaribia, hamasa ya kusoma inakuwa juu.
Jiwekee muda wa ukomo kwa chochote unachopanga kufanya, na muda huo uwe mfupi kuliko muda uliozoeleka. Kwa kuwa na muda huu na kuufuata, utaweza kujisukuma kufanya zaidi. Kadiri unavyokuwa na muda mfupi wa kutekeleza jambo, ndivyo mawazo ya kuahirisha yanavyopotea kwenye akili yako. Waahidi watu kwamba jukumu litakamilika mapema kuliko kawaida, na tekeleza hilo uliloahidi.
Nne; KUWA NA MTU WA KUKUSIMAMIA.
Sisi binadamu ni wabaya sana kwenye kujisimamia wenyewe, huwa tunajionea sana huruma na ni rahisi sana kujidanganya. Unaweza kuwa na orodha yako ya siku, umepanga mambo yako matano muhimu na hata kujiwekea ukomo. Lakini katikati ya siku yako ukawa hujisikii kuendelea na yale uliyopanga, ni rahisi kujihalalishia kwamba labda umechoka au ni kitu hakiwezekani.
Lakini unapokuwa na mtu wa pembeni, mtu ambaye jukumu lake ni kuhakikisha umekamilisha uliyopanga na hapokei sababu bali matokeo, utalazimika kufanya kile ulichopanga kufanya.
Tafuta mtu wa karibu kwako, ambaye hakuonei huruma kisha mtake akusimamie kwa karibu ili utimize unachotaka. Kama huwezi kupata mtu wa karibu basi kuwa na kocha au menta ambaye atakusimamia kwa karibu.
Tano; JIAMBIE “NAFANYA SASA”.
Kuna wakati unakuwa umeshapanga kabisa nini utafanya na kwa wakati gani. Lakini inapofika muda wa kufanya, mawazo ya kuahirisha yanaanza kukuingia. Unaanza kuona labda hujawa tayari au ni bora kusubiri.
Ni katika wakati kama huu ndiyo unapaswa kujiambia kauli hii, NAFANYA SASA HIVI, rudia kauli hiyo mara nyingi uwezavyo na utajikuta umeanza kufanya. Kila unapofikiria kuahirisha kufanya kitu, jiambie kauli hiyo kwamba unafanya. Kila unapoanza kujiambia kwambe umechoka, anza kujiambia kauli hiyo.
Kwa kurudia rudia kujiambia kauli hiyo, unaanza kuiamini na kujiamini wewe mwenyewe na kuanza kufanya.
Rafiki, fanyia kazi njia hizi tano kila siku na kazana sana kukamilisha kila ulichopanga kufanya. Haitakuwa rahisi mara zote, na hilo ndiyo linapelekea mafanikio yawe na thamani kubwa. Kama mafanikio ni muhimu sana kwako, basi kuwa mtu wa kufanya, kuwa mtu wa kuchukua hatua.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge