Hongera sana rafiki yangu mpendwa kwa kulimaliza juma namba 48 la mwaka huu 2018. Naamini lilikuwa juma bora sana kwako, kwa hatua ulizoweza kupiga na matokeo uliyoyapata. Kila matokeo uliyopata ni muhimu sana kwako, matokeo mazuri yanakusogeza mbele na matokeo mabaya yanakupa funzo. Hivyo usinung’unike wala kukata tamaa kwa matokeo yoyote uliyopata, bali yatumie kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Karibu kwenye TANZO ZA JUMA NAMBA 48, ambapo nimekukusanyia yale matano muhimu sana ya kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora sana.

Yasome haya matano niliyokuandalia, yatafakari namna yanavyohusika kwenye maisha yako, kisha chukua hatua mara moja ili uweze kupata matokeo bora na kusogea karibu zaidi na mafanikio makubwa.

Karibu sana rafiki yangu kwenye tano za juma.

#1 KITABU NILICHOSOMA; SANAA YA KUPATA FEDHA.

Juma namba 48 nimepata nafasi ya kurudia kusoma kitabu kinachoitwa THE ART OF MONEY GETTING kilichoandikwa na P. T. Barnum. Ni kitabu kifupi sana kinachoeleza kwa kina sanaa ya kupata fedha. Na siyo tu sanaa kwamba ni kitu cha juu juu, bali kitabu hiki kimeeleza misingi muhimu sana kuhusu kupata fedha.

Mwandishi wa kitabu hiki, P. T Barnum aliishi zaidi zaidi ya miaka 120 iliyopita, lakini misingi aliyoieleza kwenye kitabu hiki iko sahihi mpaka leo hii. Ni hazina kubwa sana inayopatikana kwenye kitabu hiki kifupi sana kusoma.

Barunum alikuwa akijihusisha na biashara ya burudani na maonesho, na hivyo ndiyo iliyompa umaarufu na utajiri mkubwa. Lakini pia alikuwa mwanasiasa aliyepata nafasi ya kuongoza kama meya, pia alikuwa mwandishi. Kwenye kitabu cha sanaa ya kupata fedha, Barnum anatushirikisha kwa uzoefu wake, kwa makosa aliyofanya na yale aliyojifunza.

Ipo misingi 20 muhimu sana ambayo Barnum aliandika kwenye kitabu hiki kuhusu fedha. Na hii ndiyo ninayokwenda kukushirikisha hapa.

Kabla hatujaingia kwenye misingi hii, Barbum anasisitiza kwamba njia ya kuelekea kwenye utajiri iko wazi kama njia ya kuelekea kisimani. Anasema fursa zipo nyingi na kwenye kila sekta kwa yeyote anayetaka kupata fedha. Na kwa misingi hii 20 anayotushirikisha, hakuna kinachoweza kukuzuia usipate fedha pale unapoitumia.

Karibu kwenye misingi 20 ya sanaa ya kupata fedha.

  1. USIKOSEE WITO WAKO.

Barnum anasema utafanikiwa zaidi iwapo utafanya kazi au biashara inayoendana na wito uliopo ndani yako. kwa kufanya kile unachopenda au kila ambacho una kipaji nacho, utafanya vizuri zaidi kuliko kukazana kufanya kile ambacho hakiendani na wewe.

Kinachofanya mtu afanikiwe siyo kile anachofanya, bali namna anavyokifanya.

  1. CHAGUA ENEO SAHIHI.

Ukishachagua ni nini unataka kufanya kwenye maisha yako, chagua eneo sahihi la kufanyia kitu hicho. Eneo ambalo wale unaowalenga wanapatikana. Kwa sababu hata kama unafanya kitu vizuri kiasi gani, kama unaowalenga hawapatikani, huwezi kufanikiwa.

  1. EPUKA MADENI.

Barnum anasema hakuna kitu kinachowarudisha watu nyuma kama madeni, hasa pale madeni hayo yanapokuwa ni ya matumizi yasiyozalisha. Anasema mtu yeyote anayeanza maisha, anapaswa kuepuka sana kuingia kwenye madeni, kwa sababu atakuwa mtumwa kwa maisha yake yote. Atajikuta anafanya kazi lakini hapigi hatua maana ukishaingia kwenye madeni inakuwa vigumu kutoka.

Barnum anasema, fedha inapaswa kuheshimiwa kama moto, moto ukiutumia vizuri utakunufaisha sana, lakini ukifanya nao uzembe utakuteketeza kabisa.

Pia anatuambia yule anayekopesha akilala usiku anaamka akiwa na fedha nyingi zaidi kwa sababu mikopo anayotoa ina riba. Ila yule anayedaiwa akilala na kuamka ana fedha kidogo zaidi kwa sababu riba inaongezeka. Usiwe kwenye upande wa kila unapolala na kuamka unazidi kuwa masikini. Epuka mikopo.

  1. KUWA MVUMILIVU.

Ukishachagua njia yako ya mafanikio, basi unachopaswa kufanya ni kukaa kwenye njia hiyo mpaka ufanikiwe. Mafanikio hayatakuja haraka hivyo lazima uwe na uvumilivu, lazima uwe tayari kuumia na kujituma bila kuyaona mafanikio haraka.

Pia jitegemee, watu wengi wanashindwa kwenye maisha kwa sababu hawawezi kusimama kwa miguu yao wenyewe, wengi wanafanya kile ambacho wengine wanafanya au wanawaambia wafanye. Huwezi kufanikiwa kwenye haya maisha kama huwezi kusimama kwa miguu yako mwenyewe, hata kama dunia nzima inakwenda tofauti.

  1. CHOCHOTE UNACHOFANYA, KIFANYE KWA NGUVU ZAKO ZOTE.

Fanya kazi kama ikibidi kwa kuanza mapema na kuchelewa kumaliza, wakati wa msimu na wakati ambao siyo wa msimu. Usiache jiwe lolote halijageuzwa na usicheleweshe hata kwa saa moja kile ambacho ungeweza kukifanya sasa.

Chochote ambacho unachagua kukifanya, basi kifanye kweli na kwa ubora wa hali ya juu sana. Kwa kuifanya kazi au biashara yako kwa umakini na kwa juhudi, utafanikiwa kuliko wale ambao wanafanya kwa ukawaida.

Bahati huwa inaenda kwa wale ambao ni wapambanaji, hivyo pambana sana, weka kazi, fanya zaidi, na hakuna kitakachokuzuia kufanikiwa.

  1. TEGEMEA JUHUDI ZAKO BINAFSI.

Hata kama umewaajiri watu wakusaidie kwenye kile unachofanya, hakikisha unakijua kwa undani. Lazima ujue kila kinachohusika kwenye biashara yako na usitegemee mtu mwingine afanye hivyo kwa ajili yako.

Barnum anasema hakuna mtu anayeweza kufanikiwa kama haijui vizuri biashara yake na hakuna anayeweza kuijua vizuri biashara yake kama hajajifunza kwa vitendo na uzoefu.

  1. TUMIA ZANA BORA.

Katika kufanya kile ulichochagua kufanya, hakikisha unatumia zana ambazo ni bora sana. Na eneo la kwanza kuangalia ubora ni kwa wale unaowaajiri wakusaidie. Lazima wawe ni watu bora sana wanaojali kile wanachofanya. Na ukiwapata watu wa aina hiyo, basi usiwaachie. Hata kama itakubidi kuwalipa zaidi, kama watu wanafanya vizuri, wanakuzalishia vizuri, basi hakikisha unaendelea kuwa nao. Lakini kama watakuwa wasumbufu, basi achana nao mara moja.

  1. USIENDE JUU YA BIASHARA YAKO.

Watu wengi wanapokuwa wanaanza kile wanachopanga kufanya, huwa wanapenda kuanzia juu, wengi hawataki kuanzia chini. Na hapa ndipo wengi hujiingiza kwenye matatizo. Mfano mtu anakopa fedha ili aanze biashara.

Barnum anasema hakuna kosa kubwa kama mtu kufikiri atafanikiwa kwa kuanza kitu na fedha za kukopa. Anasema mtu anapoanzia chini kabisa, anajifunza kupitia ugumu na kipato chake kinavyoongezeka anakitumia vizuri. Lakini mtu anapoanzia juu, labda kwa fedha za mkopo, anajikuta ametumia vibaya na kubaki kwenye madeni ambayo yanamfanya awe mtumwa.

Barnum anasisitiza usemi wa kinachopatikana kwa urahisi hupotea kwa urahisi, na anasema hakuna kitu chenye thamani kama hakijagharamiwa juhudi.

  1. JIFUNZE KITU CHENYE MANUFAA.

Barnum anasema kila mtu anapaswa kuwa na ujuzi wenye manufaa, ujuzi ambao mtu anaweza kulipwa kupitia ujuzi huo. Anasema mtu akiwa na ujuzi fulani, hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani, hatakosa njia za kuendesha maisha yake.

  1. ONGEZWA NA MATUMAINI, LAKINI USIWE NA UHAKIKA KUPITILIZA.

Barnum anatukumbusha mithali ya zamani kwamba usihesabu kuku kabla mayai hayajaanguliwa. Kwamba kama kuna mayai 10 yanaatamiwa, haimaanishi kwamba tayari una kuku wapya kumi. Ni vizuri kuwa na matumaini kwamba mambo yatakwenda vizuri na kutegemea yaende vizuri, lakini usijipe hilo kama uhakika. Jipe nafasi ya mambo kwenda tofauti na hilo litakuwezesha kuchukua hatua sahihi pale mambo yanapokwenda tofauti.

  1. USITAWANYE NGUVU ZAKO.

Barnum anasema jihusishe na kitu kimoja pekee, na komaa na kitu hicho mpaka utakapofanikiwa au pale uzoefu wako unapokuonesha kwamba ni wakati wa kuachana nacho. Kugonga nyundo kwenye msumari mmoja kwa kurudia rudia kunafanya msumari huo uingie ndani.

Pale ambapo umakini wa mtu unawekwa kwenye kitu kimoja, akili yake inakuwa inamletea njia za kuboresha ambazo asingeziona kama akili yake ilikuwa imezama kwenye vitu vingine vingi kwa wakati mmoja. Watu wengi wamepishana na bahati kwa sababu akili zao hazikuwa na utulivu, walikuwa wamechoshwa na mengi wanayofanya.

  1. KUWA NA UTARATIBU WA KILA UNACHOFANYA.

Kwenye kazi au biashara yako, unapaswa kuwa na utaratibu wa namna unavyofanya mambo yako. Lazima uwe na sheria zako unazozifuata kwenye shughuli zako unazofanya, kila jambo liwe na wakati na mahali pake.

Jiwekee utaratibu wa kufanya jambo moja kwa wakati, kukamilisha kila ulichopanga na kwa muda uliopanga, utapata muda wa kupumzika na kufanya yale yasiyohusu kazi. Lakini kama utakuwa mtu unayegusa vitu na kuacha bila kumaliza na kwenda kwenye kitu kingine utajikuta muda wote upo bize na hakuna ulichokamilisha, hutapata hata muda wa kupumzika.

  1. SOMA MAGAZETI.

Barnum anasema chagua magazeti ambayo yanaaminika, na yatumie kujua yale yanayoendelea ulimwenguni na hata kwenye kile unachofanya. Kupitia vyombo vya habari ndiyo unapata fursa ya kujua yanayoendelea na nafasi nyingine nzuri kwako kutumia.

  1. KUWA MAKINI NA ‘KAZI ZA NJE’

Wapo watu ambao wanachagua kufanya kazi au biashara halali, wanaifanya vizuri na wanapata mafanikio makubwa. Mafanikio haya yanakuwa tatizo kwao kwa sababu wanaanza kujidanganya kwamba wanaweza kufanya chochote. Na wale wanaowazunguka ndiyo wanawapoteza zaidi, kwa kuona mtu ana mafanikio basi kila mara wanakuja kwake na fursa nyingi za kutengeneza fedha zaidi. Mtu anachukua fedha zake alizozipata kwa njia sahihi anakwenda kuziweka kwenye kitu asichokijua vizuri na mwishowe anakipoteza.

Jihusishe na vile vitu unavyovijua kiundani, kama kitu hukijui achana nacho, hata kama kila mtu anakuambia kinalipa sana na unakosa fedha. Ukifuata msingi wa 11, hutakuja kupoteza fedha wala kutapeliwa.

  1. USIMDHAMINI MTU BILA AMANA.

Mtu anapokuja kwako akitaka umdhamini au akitaka umkopeshe fedha, usikubali kumwamini tu kwa sababu mna mahusiano fulani. Badala yake hakikisha mtu huyo ana amana inayoendana na kiasi anachotaka umdhamini. Hii siyo tu itakusaidia wewe, bali itamsaidia huyo anayetaka umdhamini pia. Kwa sababu kama mtu hana amana inayoendana na kiasi unachotaka umdhamini au kumkopesha, basi hata kiasi hicho akikipata, kitakuwa matatizo kwake.

Wafanye watu wajue thamani ya fedha kwa kuifanyia kazi, na siyo kuipata kirahisi na ikaishia kupotea kirahisi.

  1. TANGAZA BIASHARA YAKO.

Hata uwe na bidhaa au huduma bora kiasi gani, kama hutangazi biashara yako, hutapata wateja wa kununua kile unachouza. Na njia ya kwanza ya kutangaza ni kuhakikisha unakuwa na ubora wa hali ya juu. Mfanye mtu aone fedha aliyoitoa imelipia thamani sahihi na atakuwa tayari kukuzungumzia kwa wengine.

Pia kutangaza hakufanyiki mara moja, bali ni zoezi endelevu. Mtu anapokutana na tangazo mara ya kwanza analipuuza, anapokutana nalo kwa mara ya pili analiangalia lakini haweki maanani, kwa mara ya tatu analisoma, mara ya nne anaangalia bei, mara ya tano anaongea na mwenza wake, mara ya sita anakuwa tayari kununua na kwa mara ya saba ndiyo ananunua. Hivyo inamchukua mtu mara saba kuona tangazo lako ndiyo anunue, ndiyo maana unapaswa kutangaza kila mara.

  1. KUWA MPOLE NA MKARIMU KWA WATEJA WAKO.

Upole na ukarimu ni mtaji bora sana unaoweza kuwekeza kwenye biashara yako. Ukubwa wa biashara na hata matangazo mengi hayatakuwa na maana kama wewe au wafanyakazi wako hawatawajali wateja. Kama mteja hajaliwi ataenda kule ambapo anajaliwa.

Pia wateja watakukimbia kama unachojali ni faida yako tu na siyo wao kuwa bora zaidi. Usiwahudumie wateja wako kama vile hutawaona tena, kwa sababu kweli hutawaona tena. Mhudumie kila mteja kama vile atakuwa mteja wako wa milele, na wengi watakaa na wewe kwa muda mrefu.

  1. TOA MSAADA.

Unapaswa kutoa misaada kwa wenye uhitaji, ni wajibu na pia ni kitu kizuri kufanya. Lakini pia kuwa makini kwa wale unaowapa msaada, wawe kweli wanastahili msaada huo. Wasaidie wale ambao wapo tayari kujisaidia wao wenyewe, hawa ndiyo ambao msaada wako utawanufaisha. Lakini wale wanaotaka msaada tu kama msaada, kuwapa msaada hakuwasaidii kutoka pale walipo.

  1. USIWE MPAYUKAJI.

Barnum anasema kuna watu wana tabia ya kijinga ya kueleza kila kitu kuhusu maisha yao. Wakipata fedha basi kila mtu anajua wana fedha, wakiishiwa basi kila mtu anajua. Chochote kinachotokea kwenye maisha yao, hawawezi kutulia nacho. Barnum anatuambia tusiwe wapayukaji, hatupaswi kueleza kila kitu kuhusu maisha yetu kwa kila mtu. Kadiri wachache wanavyojua kuhusu maisha yako, ndivyo matatizo yako yanakuwa madogo pia. Lakini pale wengi wanapojua kuhusu maisha yako, ndivyo unakaribisha matatizo mengi pia.

  1. TUNAZA UADILIFU WAKO.

Uadilifu wako una thamani kubwa kuliko almasi na rubi, usifanye chochote cha kuharibu uadilifu wako, kwa sababu ukishauchafua, ni vigumu kuusafisha. Watu wakishajua kwamba wewe siyo mwadilifu, hawatakuamini tena. Na hakuna hukumu mbaya kama hukumu ya umma.

Fanya mambo yako kwa uadilifu na uaminifu, na simamia hilo kama sheria kwako. Hata kama utakosa fedha kwa kusimamia uadilifu, kosa tu, kwa sababu hata ukiipata, kuna wakati utairudisha na itaacha madhara makubwa sana kwako kwa sababu hutaaminika tena.

Rafiki, hii ndiyo misingi 20 ambayo P. T Barnum aliiandika kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, lakini kila msingi ni muhimu sana kwenye maisha ya sasa. Tuiishi misingi hii katika kuelekea kwenye mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

#2 MAKALA YA JUMA; ISHINDE TABIA YA KUAHIRISHA.

Kupanga ni rahisi, kila mtu anaweza kupanga na wengi huwa tunapanga mambo mengi na makubwa tunayotaka kufanya. Lakini inapofika wakati wa utekelezaji ndiyo kama dunia nzima inasimama kuhakikisha hatutekelezi tulichopanga.

Tabia ya kuahirisha mambo ndiyo adui wa kwanza wa mafanikio kwa wengi. Hivyo ukiweza kuishinda tabia hii, utaweza kufanya mengi na makubwa.

Juma namba 48 nilikushirikisha njia tano za kuishinda tabia ya kuahirisha mambo. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ile, basi unaweza kuisoma sasa hapa; Njia Tano (05) Za Kuishinda Tabia Ya Kuahirisha Mambo Na Kuweza Kufanya Kila Ulichopanga Kwa Wakati Wake.

Pia kila siku tembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA na kuna makala nzuri za kujifunza.

 

#3 TUONGEE PESA; KUWASHWA NA PESA.

Kuna watu ambao fedha huwa zinawawasha, yaani wakipata fedha kidogo hawawezi kutulia mpaka ziishe. Hawa ni watu ambao wanafanya safari yao ya mafanikio na hata ya maisha kwa ujumla iwe ngumu sana. Kwa sababu kama huwezi kutulia pale unapopata fedha, watu watakujua na watakuwa wanakulaghai kila wanapojua una fedha.

Unapaswa kujijengea tabia za kifedha ambazo hazikufanyi uonekane kwa kila mtu wakati ambapo una fedha na wakati ambapo huna. Kwa kujijenga tabia za aina hii, utajiepusha na matatizo mengi kwenye maisha yako.

Unapopata fedha zaidi ya ulivyozoea kupata, jifunze kutulia kwanza kabla hujafanya chochote, jifunze kuchukulie kama hujapata fedha hizo na yafanye maisha yako yaende kama yalivyokuwa yanaenda. Ukishakuwa umetulia vizuri, hapo sasa unaweza kupanga kipi cha kufanya na fedha zako.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; UKOCHA BINAFSI.

Kuna kitu kimoja ambacho najifunza kwa wale ninaowakochi moja kwa moja, kitu hiki ni kwamba watu wengi huwa wana mipango mizuri sana, na wanajua nini wanataka na watapataje. Lakini kwa kuwa hakuna anayefanya kama wanachotaka kufanya, basi wanahofia kufanya kwa sababu watashindwa au wengine watawapinga. Lakini unapowasimamia watu hawa kwa karibu, basi wanafanya na wanafanikiwa sana.

Hiki ndiyo nataka nikusaidie wewe rafiki yangu, najua ndani yako kuna kitu kikubwa sana, kuna ndoto kubwa sana. Lakini umekuwa unakatishwa tamaa na wengine kwamba haiwezekani au utashindwa, na wewe ukawaamini.

Mimi nina kitu kimoja ninachotaka kukuambia, UNAWEZA KUWA CHOCHOTE UNACHOTAKA KUWA. Na ili uweze kufika huko, unahitaji usimamizi wa karibu na mtu wa kukupa moyo na kukuzuia usikate tamaa na kurudi nyuma. Unahitaji kuwa na kocha na hapo ndipo mimi naingia kwenye maisha yako.

Natoa huduma ya ukocha binafsi kwa wale wenye ndoto kubwa lakini wamekwama kwenye kuzitekeleza. Karibu tufanye kazi pamoja ili kukuhakikishia mafanikio yako.

Kama unahitaji huduma ya ukocha binafsi basi tuwasiliane kwa wasap namba 0717396253. Karibu sana.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; SIKU INAYOKURIDHISHA.

“Look at a day when you are supremely satisfied at the end. It’s not a day when you lounge around doing nothing, it’s when you’ve had everything to do and you’ve done it.” – Margaret Thatcher

Iangalie siku ambayo imekuridhisha sana, siyo siku ambayo umeimaliza bila kufanya chochote, bali siku ambayo ulikuwa na mengi ya kufanya na umefanya yote.

Ile siku ambayo ulikuwa na majukumu mengi na ukapambana mpaka kuyamaliza ni siku ambayo inakuridhisha na unaithamini sana. Hivyo ili kuwa na maisha bora, tengeneza siku zako kwa namna ambayo una mengi ya kufanya na unayakamilisha kuyafanya ndani ya siku hiyo. Hayo mengi yasiwe tu mengi, bali mengi yenye maana kwako.

Unapoimaliza siku ukiwa huna makubwa uliyokamilisha, unajisikia vibaya na kuona siku hiyo umeipoteza. Usikubali hii iwe ndiyo hali yako kila siku, utakuwa umeyapoteza maisha yako.

Hizi ndiyo tano za juma namba 48, tano ambazo nakusihi uondoke na kitu cha kwenda kufanyia kazi mara moja kwenye maisha yako ili uweze kupiga hatua zaidi.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu