Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora kwa kila mmoja wetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.


Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, huu ni msingi wa maisha ya mafanikio kwenye kila nyanja ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu LIPI BAYA KABISA LINALOWEZA KUTOKEA?
Rafiki, ili kupata matokeo tofauti na unayopata sasa, lazima ufanye vitu tofauti na unavyofanya sasa. Lazima ubadilike.
Lakini ipo changamoto kubwa kwenye kubadilika, ambayo ni hofu ya mambo kwenda vibaya.
Mabadiliko hayana uhakika na lolote baya linaweza kutokea. Hili ndiyo linawatisha watu na kuendelea kubaki pale walipo sasa, wakifanya kile ambacho wameshazoea kufanya na angalau kuwa na uhakika wa matokeo yake.

Ili kuvuka hofu hii, unapaswa kujiuliza swali moja, LIPI BAYA KABISA LINALOWEZA KUTOKEA?
Kwa kila unachotaka kubadili lakini unakuwa na hofu ya matokeo utakayopata, jiulile lipi baya kabisa linaloweza kutokea.
Iwapo utachukua hatua ya tofauti, je matokeo mabaya kabisa yanayoweza kutokea ni yapi?
Hapo unafikiria pale kila kitu kimeenda hovyo, utapata matokeo gani?
Baada ya kupata picha hiyo angalia je unaweza kuishi na matokeo hayo?
Kama kweli mambo yataenda vibaya kama ulivyofikiri, je utaweza kuishi na matokeo hayo?

Mara nyingi majibu ni ndiyo, kwamba utaweza kuishi na matokeo mabaya kabisa unayoweza kupata.
Kitu ambacho kitakupa sababu ya kufanya, hata kama unayo hofu ya kufanya.

Kufikiri hivi siyo kuwa na mtazamo hasi, bali kuiandaa akili yako na mambo usiyoyategemea na kuona kama itaweza kwenda nayo.
Na muhimu zaidi, mambo huwa hayawi mabaya kama tunavyofikiria yanaweza kuwa, wala pia huwa hayawi mazuri sana kama tunavyotarajia.

Hivyo kwa vyovyote vile, fanya, jaribu mambo mapya, kuwa mbunifu. Kama hutakufa kwa kubadili kitu, basi utakuwa bora zaidi ya ulivyo sasa. Na maamuzi mengi kwenye maisha yetu siyo ya KUFA AU KUPONA, ni maamuzi yanayoweza kufanya hali kuwa ngumu kwa kipindi fulani, lakini baada ya hapo mambo yanakuwa mazuri.

Swali la kutafakari asubuhi hii;
Je ni jambo gani umekuwa unataka kufanya lakini unahofu ya kulifanya kwa sababu unaona mambo yanaweza kwenda vibaya?
Na je ikiwa yataenda vibaya kabisa, utakufa? Kama hutakufa, ni vyema ukaanza kuchukia hatua hizo, hata kama ni kwa hatua ndogo.

Nakutakia siku njema sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info