Habari za leo rafiki yangu?
Karibu kwenye makala yetu nzuri ya leo, ambapo nakwenda kukushirikisha kitu muhimu sana kwa mafanikio yako. Kitu ambacho nimeona kimenisaidia mimi, na nina uhakika kitakusaidia wewe pia.
Katika kukushirikisha kitu hichi muhimu, nitaanza na hadithi ambayo nimejifunza kwenye kitabu THE SEVEN SECRETS OF MONEY MASTERY. Na hadithi hiyo inakwenda kama ifuatavyo;
Miaka 3,000 iliyopita, mkulima mmoja masikini aliyeitwa Adir aliishi na mke wake pamoja na watoto watatu, kwenye kijiji kidogo kilichokuwa umbali wa maili 59 kutoka mji wa Yerusalemu. Alikuwa ni mkulima mdogo, aliyefanya kazi kwa juhudi kubwa, lakini bado hakuweza kuwa na uhakika wa kuilisha familia yake.
Majirani zake Adir walikuwa masikini pia, japokuwa walimwonea wivu Adir kwa sababu alikuwa na kitu ambacho wao hawakuwa nacho, kitu hicho kilikuwa ni ng’ombe. Ng’ombe huyo hakuwa mkubwa kama tunaowajua sasa, alikuwa ni ng’ombe aliyekondeana sana. Lakini maziwa kidogo ambayo Adir aliweza kupata kutoka kwa ng’ombe huyo, yalimwezesha kupata mahitaji kidogo ya familia yake. Alishukuru sana kwa kuwa na ng’ombe huyu, na hakuwahi kufikiria kumuuza wala kumchinja, kwa sababu maisha yake yalitegemea kwenye ng’ombe yule.
Siku moja, kiongozi maarufu wa kiroho alitembelea kijiji alichokuwa anaishi Adir, akiwa na kikundi cha wafuasi wake. Kiongozi huyo alijulikana kama Ba’al Shem Tov. Adir alikuwa mtu wa kiroho, hivyo alifurahishwa sana na ujio wa kiongozi huyo wa kiroho kijijini kwao.
Alifurahishwa zaidi pale kiongozi huyo alipopita nyumbani kwake, lakini alishangazwa pale Ba’al aliposema yeye na wafuasi wake wamechoka, hivyo wangefurahi kama wangeweza kupumzika nyumbani kwake. Alipata huzuniko haraka, angewaweka wapi watu wote hao wakati yeye ni masikini mwenye nyumba ndogo tu.
Kabla hata hajatoa majibu, Ba’al akawa ameshaingia ndani.
Kitu kilichomuumiza Adir zaidi, ni pale kiongozi huyo alipouliza chakula gani kipo. Hapo Adir aliumia kichwa kwa sababu chakula cha familia yake tu ni shida, sasa itakuwaje kwa kuwalisha wanaume tisa? Alimwita mke wake washauriane, akitoa wazo la kumchinja ng’ombe wao. Mkewe akawa anakataa, akimwambia kama ng’ombe huyo ataondoka, maisha hayawezi kwenda tena. Lakini mwisho wa siku, hawakuwa na namna bali kumchinja yule ng’ombe.
Adir alijipa moyo kwamba, wakimchinja ng’ombe yule, wageni wangekula na wangebaki na nyama ya kuendelea kula siku mbili tatu. Lakini matumaini hayo yalizimika baada ya chakula kupewa wageni, kila nyama ililiwa na ilibaki mifupa pekee. Hakukuachwa chochote.
Baada ya kumaliza kula, Ba’al alimpa taarifa Adir kwamba, ameahirisha kupumzika pale, kwa sababu baada ya kula amepata nguvu na hivyo wataendelea na safari, baada ya kusema hayo, waliondoka mara moja. Kichwa cha Adir hakikuweza kutulia, mambo hayo yalitokea haraka sana, akiwa haelewi maisha yataendaje baada ya pale. Kwa kushindwa kutuliza mawazo yake, aliona bora aondoke nyumbani na kwenda msitu wa karibu apunguze mawazo yake.
Wakati anakatiza katikati ya miti, akifikiria familia itaendaje baada ya pale, huku ng’ombe aliyekuwa tegemeo akiwa hayupo tena, alisikia sauti mbele yake.
Aliposogelea ile sauti, alikuta ni mzee ameanguka na hawezi kuinuka. Kutokana na kuwa mtu wa imani, aliona ni wajibu wake kumsaidia mtu yule. Alienda kwenye mfereji uliokuwa karibu akaja na maji kwa ajili ya mzee yule kunywa. Wakiwa wamekaa pale walianza mazungumzo, kama ilivyo kawaida, walianza kwa kuambiana majina. Adir aliposikia jina la yule mzee, Mordekai, aligundua ni mtu ambaye alishamsikia. Alikuwa ndiye mtu tajiri sana kwenye ukanda mzima waliokuwa wanaishi. Alimuuliza iwapo ni kweli hadithi alizokuwa akisikia kwamba anaishi kwenye jumba la kifahari akiwa na wasaidizi wengi. Alimwambia ndiyo. Alimwambia ana bahati sana, Mzee yule akamwambia siyo kweli, kwa sababu pamoja na mali nyingi alizonazo, bado familia yake ilijali kuhusu fedha zake tu. Walikuwa wanasubiria afe ili wagawane mali zile. Akamwambia huenda watafurahi sana wakijua amefia huko porini. Adir aliyatafakari maisha yake na familia yake pamoja na majirani zake.
Pamoja na kwamba hawakuwa na mali, lakini waliishi maisha ya kujali kwa kila mmoja.
Adir alikazana kumsaidia mzee yule, wakafika eneo la jirani ambapo walipata punda na kuweza kumbeba mpaka mjini ambapo mzee yule alikuwa rahisi kufika nyumbani kwake. Wakati wanaagana, Mordekai alimwaga Adir akimwambia kwenye maisha yake, yeye ni mtu wa kwanza kumsaidia bila ya kujali fedha zake. Alimwambia hatomsahau kwenye maisha yake.
Miaka mitatu baada ya nabii yule Ba’ Al Shem Tov kupita kwenye kijiji cha Adir, alirudi tena akiwa na wafuasi wake, safari hii wakiwa wengi zaidi. Walipofika nyumbani kwa Adir walishangaa kuona maisha yake yamebadilika, akiwa na mali nyingi huku maisha yake yakiwa mazuri sana.
Wale wafuasi waliomjua miaka mitatu iliyopita, walishangazwa sana, wakimwuliza Adir nini kimetokea mpaka maisha yake kubadilika. Adir aliwaambia kwamba maisha yake yalibadilika baada ya Mordekai kufariki, aliacha sehemu kubwa ya mali zake kwa mtu pekee aliyemsaidia asife. Na mtu huyo alikuwa ni yeye.
Ba’ Al hakuonekana kusema mengi bali aliishia kutabasamu. Baada ya kuondoka, wafuasi wake walimuuliza kwa nini anatabasamu na kwa nini siku ile walipopita kwa Adir alifanya alivyofanya. Kwa sababu wafuasi wake hawakuwahi kumwona akila nyama nyingi kiasi kile, na wala hajawahi kuvunja ahadi yake. Lakini siku ile alikula kuhakikisha anamaliza na alipomaliza aliahirisha kulala na wakaondoka.
Walimwuliza kwa nini alikosa huruma kiasi kile kwa masikini?
Na yeye aliwajibu, Adir hakuwa masikini, bali kilichokuwa kinamzuia kuwa na maisha mazuri ni yule ng’ombe aliyekuwa amekonda, hivyo aliamua kuhakikisha ng’ombe huyo anaondoka ili wafikirie tofauti.
Yule ng’ombe aliyekuwa amekonda ndiyo kitu pekee alichokuwa anakifikiria, akiwa na matatizo anaangalia pale. Alichukulia maisha yake yote yanategemea kwenye ng’ombe yule, hivyo alipoondoka, ilimbidi afikiri tofauti na hapo ndipo alipokutana na fursa mpya. Isingekuwa kuondoka kwa ng’ombe, angeendelea kumfikiria ng’ombe yule kama kitu pekee cha kuendesha maisha yake.
Hadithi hii inakufundisha nini kwenye maisha yako?
Sasa ni wakati wa kuyaangalia maisha yako mwenyewe, na ona ni ng’ombe gani aliyekonda, ambaye ndiyo anakuzuia wewe kupiga hatua?
Je ni ajira uliyonayo, ambayo inakupa kipato kidogo lakini huthubutu kuachana nayo kwa sababu unaona maisha yatakuwa magumu sana?
Au ni biashara ambayo umekuwa unafanya, biashara ndogo, ambayo haipigi hatua, kwa sababu hiyo pekee ndiyo unafikiria inaendesha maisha yako?
Angalia hata tabia ulizonazo, je ni kitu gani ambacho unafanya kwa mazoea, ambacho umeshajijengea kwenye mawazo kwamba maisha yako hayawezi kwenda bila kitu hicho?
Mjue ng’ombe aliyekonda ambaye anakuzuia kuwa na maisha bora, na anza kuchukua hatua za kufikiria nje ya ng’ombe huyo. Siyo lazima umchinje mara moja, lakini hebu acha kumwangalia kwa muda, hebu fikiria kama asingekuwepo mambo yangeendaje?
Ukweli ni kwamba, mambo huwa hayawi mabaya kama ambavyo huwa tunafikiri.
Wapo watu ambao wanakuwa wanafikiria maisha yao hayawezi kwenda bila ajira zao, inatokea wanafukuzwa kazi na maisha yanakuwa bora zaidi hata ya walivyokuwa kwenye ajira.
Kitu kimoja ninachoweza kukuambia rafiki yangu ni hichi, chochote ambacho unategemea kwa sasa, chochote ambacho unakiri ndani ya nafsi yako kwamba maisha yako hayawezi kwenda bila hicho, ndiyo kikwazo cha mafanikio yako. Hata kama ni mtu, huyo ndiyo kikwazo. Anza kujaribu kufikiria nje ya kitu hicho, na utaona fursa nyingi unazoweza kutumia kupata kile unachotaka.
Usikubali maisha yako yawe magumu kwa sababu ya huyo ng’ombe aliyekonda, ambaye amekufanya uone hakuna maisha nje ya hapo. Maisha yapo, tena makubwa sana, ambayo ukiweza kuchukua hatua, utapiga hatua kubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.
