MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Ni siku nyingine nzuri sana ambapo tumepata nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Leo ndiye ile kesho ambayo uliisema jana, na ukitaka iwe kweli basi chukua hatua leo na usiseme tena kesho.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUFANYA KAZI YAKO (DO YOUR WORK).
Wote tunajua umuhimu wa kazi kwenye maisha yetu na mafanikio yetu,
Lakini hakuna kitu ambacho watu wanapenda kukikwepa na kukitoroka kama kazi.
Watu wengu hawapendi kuchoka wala kuumiza akili zao, hivyo hutumia muda mwingi kukwepa na kutoroka kazi kuliko muda wanaotumia kufanya kazi hasa.
Sasa kukwepa na kutoroka kazi hakujawahi kumwacha mtu salama,
Badala yake kumepelekea watu…
Kupata msongo wa mawazo kupitia kazi wanayofanya.
Kuona kazi yao haifai bali ya wengine ndiyo nzuri.
Kuwa na changamoto za kipato.
Kuanza kukosoa wengine kwenye kazi zao wanazofanya.
Kuona maisha hayana maana bali kuteseka tu.
Wakati wowote unapopitia hali kama hizo hapo juu, jiulize ni kazi gani unayokwepa au kutaka kutoroka.
Iwapo utafanya kazi yako, kwa kuifanya hasa, hutapata muda wa hayo yanayokusumbua sasa. Kwa sababu kazi yako itakuwa kipaumbele kikuu na utapata matokeo bora sana kwako.
FANYA KAZI YAKO, USIJARIBU KUIKWEPA AU KUTOROKA, UTAUMIA ZAIDI.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.