MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUIVUKA SIKU YA TATU…
Rafiki, watu wengi wamekuwa wanajaribu kubadili au kujenga tabia,
Wanapanga kabisa hatua watakazochukua ili kufikia kile wanachotaka,
Wanakuwa na hamasa kubwa ya utekelezaji na wanaanza kutekeleza.
Haichukui siku nyingi wanakata tamaa na kuacha,
Na mara nyingi hili hutokea kuanzia siku ya tatu.
Katika kubadili au kujenga tabia, siku ya kwanza huwa ni raha na furaha, unaona umeweza kufanya, unajisifu na kuona kumbe siyo vigumu kama ulivyokuwa unadhani.
Siku ya pili maumivu unaanza kuyasikia, lakini siyo makubwa sana na bado una matumaini ya kuweza kufanya.
Siku ya tatu maumivu yanakuwa makubwa mno, unakuwa na kila sababu kwa nini usiendelee, utajishawishi kwamba unajitesa na pia kuona una haki ya kwenda taratibu zaidi. Wanaokuzunguka nao watachangia yao, kukuambia usijisumbue sana, au umebadilika na hupo tena kama zamani.
Hii ndiyo siku ambayo unasaliti mipango yako, unaacha na kurudi kwenye maisha yako ya zamani, kufanya kile ambacho umeshazoea kufanya.
Hili huwa linatokea kwenye kila tabia unayotaka kujenga au kuvunja, iwe ni ufanyaji wa mazoea, kuamka asubuhi, kusoma vitabu, kujali muda, kuacha ulevi na kadhalika.
Hivyo rafiki, unachohitaji kukazana kufanya, ni kuivuka siku ya tatu.
Hata maumivu yawe makubwa kiasi gani, usikubali kabisa kurudi nyuma.
Yaani ndani ya akili yako usiwe kabisa na wazo kwamba upo uwezekano wa kuacha.
Na pale maumivu yanapokuwa makali, na sababu zinapokuwa kubwa za kuacha, ndiyo unahitaji kung’ang’ana na kuendelea.
Ukiweza kuvuka siku hiyo ya tatu, ukaweza kuendelea licha ya maumivu, unakuwa umeushinda mwili wako na kuweza kujijengea nidhamu muhimu sana ya mafanikio yako.
Kazana kuivuka siku ya tatu, na kila siku endelea kuvuka kila kikwazo ili kufika kule unakotaka kufika.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.