Huwa najisikia furaha na amani moyoni pale ninapokutana na wewe na kuniambia kuwa umeshaanza kuchukua hatua kufikia lengo, nafarijika sana ninapopokea simu yako na kuniambia kuwa umeshafanikisha malengo yako na sasa umeamua kusonga mbele zaidi, lakini huwa nahamasika kuwafariji na kuwasaidia zaidi pale ninapowaona baadhi ya marafiki wanashindwa kuendelea mbele kwa sababu mbalimbali zinazowakabili katika kufikia malengo yao kwa wakati, sisi ni wamoja, tunatembea na kusafiri pamoja, kwetu jambo muhimu ni kuhakikisha kila mmoja wetu anafikia lengo kwa uhakika zaidi.Leo nitazungumzia namna ya kuepuka changamoto za nyufa ambazo nimekutana nazo pale nilipowatembelea na kukutana na marafiki mbalimbali na wadau muhimu kwenye maeneo yao ya ujenzi, wengi wa marafiki nimegundua kuwa changamoto zao za nyufa chanzo kikuu ni kushindwa kukabiliana na hali ya udongo wa mfinyanzi kabla na wakati wa ujenzi. Zipo sababu nyingi sana zinazo sababisha nyufa kwenye majengo lakini leo nimesukumwa kuzungumzia udongo wa mfinyanzi kutokana na kiasi kikubwa cha madhara na idadi kubwa ya watanzania wanashindwa kufurahia nyumba zao kutokana na kukosa kumudu mazingira ya udongo wa mfinyanzi.

Kwenye taaluma ya sayansi na uhandisi ujenzi tafiti za udongo ni jambo linalopewa kipaumbele sana ili matokeo ya usanifu wa majengo uweze kuhimili ubora kutokana na mazingira yaliyopo. Miundombinu yote yakiwemo majengo hujengwa juu ya uso wa ardhi ambayo ina aina tofauti za udongo ambao nao una tabia tofauti za kimaumbile. Mfinyanzi ni aina ya udongo ambao una tabia ya kusinyaa pale unapokuwa mkavu na kutanuka, kuvimba na kuteleza pale unapokuwa katika hali ya unyevunyevu. Hali hii ya udongo hutokana na majira mbalimbali ya mwaka ambayo wakati wa mvua husababisha udongo kutanuka na wakati wa jua udongo kukauka na hatimaye kusinyaa. Udongo huu huteleza sana wakati wa mvua na husinyaa sana wakati wa jua na kutengeneza nyufa kwenye ardhi mithili imetokana na tetemeko la ardhi.

Mabadiliko haya ya udongo husababisha madhara ya miundombinu yakiwemo majengo kutikiswa, kuinuliwa na kutitia, hali ambayo husababisha majengo na miundombinu kupasuka. Kuta, sakafu, nguzo na msingi wa nyumba huwa katika hatari kubwa, hii ndiyo sababu kuu inayowasukuma wataalamu wa ujenzi kuutambua udongo wa mfinyanzi kuwa ni aina ya udongo hatarishi sana kwenye majengo.

Zipo mbinu kuu mbili za kupambana na aina hii ya udongo ili nyumba yako iwe salama wakati wote wa majira ya mwaka.

Mbinu ya kwanza ni kuuondoa udongo wote wa mfinyanzi usigusane na muhimili wa aina yoyote wa jengo, hakikisha unachimba msingi wako wa nyumba unakuwa mpana mara mbili ya msingi wa kawaida na unatakiwa kuwa na kina kirefu mara mbili Zaidi ya msingi unaohitaji kuutumia. Urefu na upana wa ziada uliochimba unapaswa uwekwe udongo mbadala wa ule ambao umeutoa na kuuweka unaofaa zaidi kwa kuushindilia vema na kuumwagia maji ya kutosha. Hapa utakuwa umeuondoa msingi wako wa nyumba kwenye vita dhidi ya mfinyanzi na kuuweka udongo rafiki utakao pendekezwa na mtaalamu wako kutokana na uwezo wa upatikanaji wake.

Na mbinu ya pili ni kuzuia udongo wa mfinyanzi uliopo kwenye msingi wa jengo lako usiathiriwe na maji au jua ambalo ni matokeo ya majira tofauti ya mwaka ili kutoleta matokeo tofauti ya kitabia au matokeo ya kibinadamu ambayo ndiyo huleta madhara kwenye majengo. Mbinu hii inagharimu zaidi fedha kuliko mbinu ya kwanza, mbinu hii huzingatia zaidi kutoweka mazingira rafiki ya udongo wa mfinyanzi kupata unyevu wa hali na kiwango tofauti ili uweze kuhimili hali yake ya kitabia wakati wote. Kutoruhusu maji ya mvua yamwagikie karibu na msingi wa nyumba, kutopanda miti na maua karibu na kuta za msingi wa nyumba kwa sababu mizizi ya miti hunyonya maji ardhini jambo likalosababisha udongo kusinyaa na nyumba kutitia upande mmoja, pia maua huhitaji maji na endapo utamwagilia utasababisha udongo kutanuka na kuinyanyua nyumba upande mmoja, kutojenga nyumba karibu na mifereji ya maji na kusakafia eneo lako lote kuzunguka nyumba ili kutoruhusu maji kuingia ardhini karibu na nyumba yako.

Pamoja na mbinu hizo, pia zipo njia nyingine zinazosaidia kuiweka nyumba yako kuwa salama na imara dhidi ya udongo wa mfinyanzi. Njia hizo ni kama ifuatavyo:
Hakikisha msingi wako unauzungushia mkanda wa zege la kiwango kizuri na nondo zilizosukwa vizuri ili kupunguza madhara ya kutikiswa kwa nyumba. Msingi wenye zege lenye nondo ni imara zaidi kuliko msingi wa matofali na mawe pekee.

Ujenzi wa majengo kwenye ardhi yenye udongo wa mfinyanzi ni lazima ufanyike wakati wa majira ya jua na ukiwa katika hali ya ukavu na kusinyaa. Hii itasaidia kupunguza madhara ya kutitia ambayo ndiyo huwa na athari kubwa endapo hautazingatia miiko ya ujenzi.

Kama una uwezo wa kuchimba na kuuondoa udongo wote wa mfinyanzi kwenye eneo lako la ujenzi ni vema ukafanya hivyo, mara nyingi udongo wa mfinyanzi huwa hauzidi kina cha mita mbili (mita 2) kuelekea ardhini. Ni vema ukafanya uchunguzi na kutambua kina halisi cha ukomo wa mfinyanzi. Na kama kina ni kifupi hakikisha msingi wako wa nyumba unasimama baada ya kuupita udongo wa mfinyanzi.

Kwa majengo makubwa ni vema ukatafuta namna yoyote ya kukwepa udongo wa mfinyanzi, maana udongo huu ukipata maji huwa dhaifu kubeba uzito wa kiwango kikubwa, wataalamu wa ujenzi walishauri kuwa uzito wa muhimili wa jengo usizidi tani tano (tani 5) kwa mita moja ya mraba. Endapo utazidi hapo na udongo ukapata maji kidogo tu, wala hautafanikiwa kuona au kufanya chochote kwa namna muhimili wa jengo utakavyoanguka na kuleta madhara na hasara ya kujitakia.

Rafiki, ni muhimu sana kuchukua tahadhari sana wakati wa ujenzi ili kuepukana na hatari mbalimbali zikiwemo za nyufa, Haijalishi unajenga kwa lengo gani la kimatumizi, muhimu ni kufahamu vizuri hicho unachokwenda kukifanya ili kisije kukuletea hatari na hasara siku usiyoitarajia. Jitihada zangu ni kuona watanzania wote tunafanya ujenzi ulio bora na salama kwa maisha yetu yote. Inasikitisha sana kuona nyumba hata kupauliwa bado lakini nyufa zimeenea kote na mbaya zaidi zimekata msingi hadi bimu za kuta. 

Nyufa ni hatari sana kwa usalama wa watumiaji wa majengo, pia ni njia ya kupitisha na kuhifadhi wadudu hatari ndani ya nyumba, nyoka, tandu, mchwa na wengine wanaofanana hao. Jitahidi kadri uwezavyo ili ufurahie jasho na damu yako ambayo uliitumia kufanikisha katika kumiliki nyumba ya ndoto yako.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com