Nyufa ni utengano wa muhimili wa jengo ambao hapo awali ulikuwa umeungana kwa namna ambavyo umekusudiwa kukidhi vigezo vya ubunifu na usanifu wa majengo na miundombinu mingine unayohusu ujenzi. Nyufa ni tatizo mtambuka kwenye majengo, ni tatizo ambalo limekuwa la kawaida kuonekana kwenye majengo duniani kote.

Tatizo la nyufa ni miongoni mwa magonjwa sugu yanayosumbua majengo pamoja na miundombinu mingine kwenye ujenzi, haijalishi jengo lako ni jipya au la kale tatizo hili linaweza kukutokea, mbaya zaidi ni kwa wakati huu wa sasa ambao mambo mengi ya kitaalamu yanaendeshwa kisiasa na kiuchumi. Teknolojia ya Utengenezaji wa malighafi viwandani, gharama za ujenzi na aina ya ubunifu na usanifu majengo ni mambo ambayo yanaathiriwa sana na sera za siasa na uchumi duniani.

ufa

Linapotekea tatizo la nyufa kwenye majengo hupaswi kupaniki wala kulaumu sana jambo lolote kabla hujafahamu chanzo sababishi. Wakati mwingine nyufa hutokea kwa namna ambayo ni vigumu sana kuzuilika kutokana na mazingira au muundo wa ubunifu na usanifu wa muhimili wa jengo ulivyo. Kuna aina mbili za kukabiliana na nyufa kwenye majengo, aina ya kwanza ni kuzuia nyufa isitokee na aina ya pili ni kutibu nyufa iliyotokea. Leo nitazungumzia sababu kuu za nyufa na namna ya kuepukana nazo kwenye majengo ambayo yamejengwa kwa malighafi za mawe, matofali na zege.

KUTITIA KWA MAJENGO

Ni kawaida sana kutitia kwa majengo hasa yale ambayo hayana muda mrefu baada ya kujengwa, lakini hali hii inapozidi kiwango huwa ni hatari sana kwa matumizi ya majengo hayo. Kutitia kwa majengo husababishwa na udhaifu wa msingi kushindwa kuhimili uzito wa jengo, tabia ya kusinyaa na kutanuka kwa udongo uliobeba msingi wa jengo, kuoza kwa baadhi ya mimea au viumbe vilivyopo chini ya ardhi, kukua au kuoza kwa mizizi ya miti na mabadiliko ya hali ya hewa kutegemea asili ya mazingira husika. Nyufa hutokea zaidi pale upande mmoja wa jengo linapotitia na upande mwingine kubaki katika hali yake. Tatizo hili la kutitia hutegemea ubora na umakini wa matokeo halisi ya upembuzi yakinifu wa kisanifu kabla ya ujenzi. Ni muhimu sana kufanya uchunguzi wa kisanifu kwenye eneo lako kabla hujaanza ubunifu na usanifu wa kile unachokwenda kujenga ili kuepukana na nyufa baada ya ujenzi.

SOMA; Fahamu Umuhimu Wa Kuilinda Nyumba Yako Dhidi Ya Mchwa.

KUTOKIDHI VIGEZO VYA USANIFU NA UBUNIFU MAJENGO

Sekta ya ujenzi haina tofauti sana na sekta nyingine kuhusu viwango tofauti vya ubora, uzoefu na utendaji wa wataalamu wake. Mabadiliko ya haraka ya teknolojia ya uhandisi yanayoendelea kutokea duniani yanawaacha nyuma baadhi ya wataalamu wa ujenzi, hali ya uchumi na ubora wa vitendea kazi ni vikwazo kwa baadhi ya wataalamu wa ujenzi, hali ya ubabaishaji na kutokuwa na nidhamu ya kazi inawatesa baadhi ya wataalamu wa ujenzi, lakini hatari zaidi ni baadhi ya watu maarufu kama “makanjanja wa ujenzi” kuingia kufanya kazi za kitaalamu pasipokuwa na ujuzi wa jambo husika. Ubunifu na usanifu majengo ni jambo mtambuka linalohitaji uwezo na ujuzi wa hali ya juu sana tofauti na wengi tunavyofikiri, ubunifu na usanifu majengo ni muongozo wa utendaji na  utekelezaji wa maamuzi kwenye kila hatua wakati wa ujenzi. Kutokidhi vigezo vya ubunifu na usanifu majengo ni rahisi sana kutengeneza matatizo kwenye majengo yatakayokuwa yanajengwa ikiwamo kutokea kwa nyufa. Hivyo ni muhimu sana kwa wataalamu kuzingatia sana viwango na hatua zote za ubunifu na usanifu majengo ili kukidhi viwango bora ikiwemo kuepukana na nyufa.

TABIA ZA KIMAZINGIRA KWENYE ENEO LA UJENZI

Tabia ya mazingira ya mahali husika huwa na athari kwenye malighafi zilizotumika kwenye ujenzi wa majengo, maeneo yenye mabadiliko ya jotoridi kwa kiwango kikubwa husababisha kupata unyevunyevu au kukauka kwa kiwango kilichopitiliza, hali ya kunyonya majimaji na kukauka husababisha kusinyaa na kutanuka kwa baadhi ya malighafi kwa viwango tofauti matokeo yake ni kupasuka kwa muhimili wa jengo, mara nyingi kuta za nje, jikoni, bafuni na sehemu zenye matumizi ya namna tofauti ndizo zinazoathirika na tabia hizi za kimazingira. Matetemeko ya ardhi, mitikisiko ya vitu vizito kama mashine zilizohifaziwa ndani na mtikisiko unaosababishwa na upitaji wa magari mazito karibu na majengo. Maeneo yenye unyevunyevu kwa muda mrefu husababisha kuoza kwa nondo, kuta na malighafi nyingine hali inayosababisha kudhoofika kwa muhimili wa jengo jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa nyufa. Ni muhimu sana ukafanya utafiti wa aina na tabia ya udongo uliopo na majira tofauti ya hali ya hewa ili kuzingatia vigezo vya kisanifu na ubunifu kabla na wakati wa ujenzi.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuepuka Nyufa Kwenye Nyumba Yako Pale Unapokutana Na Udongo Wa Mfinyanzi.

UBORA WA MALIGHAFI ZILIZOTUMIKA

Kwenye ujenzi wa majengo ni muhimu sana kuzingatia ubora wa malighafi ambazo ungependa kuzitumia. Fikiria kuhusu viwango bora vya mawe, matofali, zege, nondo na saruji kama zimekidhi viwango vya kisanifu ili kukidhi ubora na usalama wa majengo ikiwamo kuepukana na nyufa. Malighafi dhaifu hazina uwezo mkubwa wa kuhimili ubora na usalama wa majengo kwa mda mrefu, baadhi ya nyufa kwenye majengo ni  matokeo ya maamuzi yetu kwenye matumizi ya malighafi dhaifu. Zege dhaifu hupitisha maji na kuozesha nondo, matofali dhaifu hupitisha maji, hupasuka na kuchakaa haraka matokeo yake muhimili wa jengo kushindwa kuhimili usanifu wake wa kimuundo. Umakini wa masoko kwenye malighafi za ujenzi ni muhimu sana kuwekewa mkazo kama utakuwa umedhamiria kupata matokeo mazuri kwenye ubora wa kile unachojenga.

UBORA WA MAFUNDI NA WASIMAMIZI WAKATI WA UJENZI

Uwezo na ujuzi wa mafundi na wasimamizi wa majengo huathiri ubora na muundo wa kisanifu kabla na wakati wa ujenzi. Mbinu za kisanifu kabla ya ujenzi, mbinu zinazotumika wakati wa ujenzi na maamuzi ya matumizi ya malighafi ndizo huamua matokeo halisi ya ubora wa majengo. Usanifu usiokidhi viwango vya ubora na mbinu dhaifu za kiutendaji zinazotumika wakati wa ujenzi husababisha kutokea kwa nyufa kama ishara ya taarifa kuwa kuna tatizo linalotokana na utendaji dhaifu. Wataalamu bora na makini mara zote huchukua tahadhari ya namna ya kuepuka hatari ya kupata nyufa kwa namna watakavyoona inafaa kutokana na mazingira yaliyopo ili kukidhi viwango bora vya kisanifu. Ni muhimu sana ukajiridhisha na aina ya watendaji wako ambao watakamilisha lengo lako la kuwa na nyumba nzuri itakalokidhi ubora na usalama wakati wote.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com