MAKIRITA AMANI:
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri ya leo.
Ni siku mpya ya wiki mpya ambapo tuna masaa 168 mbele yetu.
Ushauri wangu muhimu kwako ni huu, tumia sehemu kubwa ya masaa hayo kwenye kazi, na usipoteze hata dakika moja kwa mambo yasiyo muhimu.

Ianze wiki hii ukiwa na mpango mkubwa wa kupiga hatua kwenye maisha yako ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa na kupata matokeo bora sana.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu HOFU NA CHUKI…
Hizi ni hisia mbili ambazo zimebeba nguvu hasi inayoweza kufanya uharibifu mkubwa mno.
Watu watakudhuru na kukushambulia kwa sababu ya hisia hizo mbili, hofu na chuki.
Watu watagombana na kushambuliana kwa sababu ya hofu na chuki.
Hofu kwamba anachofanya mtu kitawaharibia wengine mambo yao.
Na chuki inayotokana na mambo ambayo mtu alifanya au kutokufanya huko nyuma.
Wakati mwingine hofu na chuki wala haina msingi wowote, ni basi tu watu wana mtazamo hasi wa kushindwa, na hawataki kushindwa peke yao.
Hivyo kuwa makini na watu wanaosukumwa na hofu au chuki katika kufanya maamuzi yao, mara zote huwa siyo maamuzi bora.
Kwa upande wako, kazana sana kudhibiti hisia hizo mbili, usikimbilie kufanya maamuzi yoyote kwa kusukumwa na hofu au chuki,
Kwa vyovyote vile maamuzi hayo hayatakuwa bora na baadaye yatakugharimu mno.
Kwa sababu mambo yote hasi huwa yana tabia ya kujirudia na kile unachowafanyia wengine, ndicho watakachokufanyia pale wanapopata nafasi.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.