Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Ni imani yangu kwamba umeianza siku hii vyema kabisa, ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kufanya vitu nusu nusu.
Kumekuwa na tabia ya watu kuanza kufanya kitu lakini hawakikamilishi. Wakati wanafanya kitu, wanapata wazo jingine, wanaachana na kile ambacho wanafanya na kwenda kufanya kitu kingine kipya. Huko nako pia hawakamilishi bali wanaishia njiani na kuanza kitu kingine mapya.
Unapokuwa mtu wa kufanya vitu na kuishia njiani, basi unakuwa na sifa zifuatazo;
- Hujajua nini hasa unataka kufanya kwenye maisha yako, bado unaendelea na majaribio ambayo yanakupotezea muda na maisha pia.
- Hujawa na vipaumbele kwenye maisha yako, hivyo lolote linalojitokeza mbele yako unalifanya.
- Unapenda kutafuta njia rahisi na ya mkato ya kupata kile unachotaka.
Yote hayo hayawezi kukusaidia wewe kuwa na maisha bora na ya mafanikio.
Unapokuwa mtu wa kuanza vitu na kuishia njiani, unapoteza muda mwingi, kwa sababu vitu vingi unavyoishia njiani huji kuvifanya tena.
Na hata pale unapoanza kitu kipya, bado sehemu ya mawazo yako inakuwa kwenye kile ulichoishia njiani.
Njia ya kuondokana na hili ni kuweka vipaumbele vya maisha yako, kuchagua mambo machache ambayo utayafanya kweli, kwa kuanza mpaka umalize kuyafanya. Usikubali kujaribu kila kitu halafu ukaishia njiani.
Ni bora kufanya vitu viwili na kukamilisha kabisa, kuliko kufanya vitu kumi vyete ukawa umefanya na kuishia njiani.
Chagua kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwako, na kifanye mpaka kikamilike. Pia pale unapochagua na kukubali kufanya kitu, basi kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana mpaka ukikamilishe, usikubali kuishia njiani.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.