Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza sehemu ambayo imegeuka kuwa kimbilio la wazazi wengi katika malezi ya watoto. Je unaijua sehemu hiyo? Karibu tujifunze

Tokea zama hizi za taarifa ziwepo basi falsafa ya niko bize ndiyo imekuwa ni habari ya mjini. Watu wamekuwa wakisingizia kila kitu kuwa niko bize na hata wengine wamekuwa wakitumia vibaya kukwepa majukumu yao kama mzazi au wazazi au walezi.

Kuna sehemu ambayo ndiyo imekuwa kimbilio la wazazi wengi katika malezi ya watoto. 

Sehemu ambayo wazazi wanaamua kuwapeleka huko kwa kisingizio cha wao wako bize na kutafuta maisha ambapo wao wanadai mafanikio. Mafanikio ya kwanza ni familia yako kuwa bora lakini kama familia yako ni mbovu hata juhudi zako unazoweka haziwezi kuzaa matunda unakuwa unapata laana na siyo Baraka kutoka kwa watoto wako au familia yako.

Rafiki, ukiwa nje watu wanakuona wewe safi kabisa lakini ukirudi ndani ya familia yako unaonekana wewe ni kama vile mwiba unaowachoma mioyo yao. Vilio vya watoto kupitia manung’uniko wanayoyapata au mapito wanayopata kwa sababu ya wewe kushindwa kuwapa muda, basi juhudi zako zinageuka kuwa tasa. Ni kama kuchanganya mafuta na maji kila kitu kinajitenga hata uchanganye kiasi gani kila kitu kinarudi mahali pake.

Watoto wanakosa mengi katika familia zetu. Magomvi ya baba na mama katika familia hasira zao zinamaliziwa kwa watoto wao. Watoto wanapigwa bila sababu za msingi, wanaonewa na bila kupewa nafasi za kujielezea. Watoto wakiwaona wazazi wanaona kama vile paka na panya mtoto anaona ni bora hata nisingekuwa na mzazi huyu yote ni kwa sababu hapati au haoni ladha ya uwepo wa baba au mama yao hapa duniani.

Basi rafiki, sehemu ambayo wazazi wameona ndiyo sehemu kubwa ya kimbilio lao la kukwepa majukumu yao ni kuwapeleka shule watoto wadogo kabisa shule za bweni . Ni maajabu mtoto mdogo chini ya miaka 5, kumi yuko shule ya bweni tena ukimuuliza mzazi mtoto wako umempeleka wapi yuko shule ya bweni bwana ni nzuri sana kule kuna walimu wazuri wa kuwalea tena ni shule ya dini wanapata kila kitu kule. Yeye anaona ni ufahari kumpeleka mtoto mdogo shule za bweni kumbe ni ujinga mkubwa.

Mzazi anaona raha kula starehe nyumbani yuko huru mtoto yuko bweni. Swali la kujiuliza wewe ulisoma shule za bweni ukiwa bado mdogo? Kama ni hapana kwa nini unampa mtoto mzigo mkubwa hivyo? Kule shule unafikri mwalimu ataweza kumudu majukumu ya malezi ya mtoto wako? Hujui ya kuwa mwalimu wa kwanza katika malezi ya watoto ni wewe? Mtoto atakuja kujifunza nini kutoka kwako? Mtoto atajivunia nini kutoka kwako huna hata mguso wowote wa kiupendo uliompa. Watoto wanahitaji sana lugha ya mguso kutoka kwa wazazi wao kama vile kumkumbatia au kumbusu( physicala touch language).

Ndugu mpendwa, kwanza hata katika taaluma ya ualimu hakuna hicho kitu cha kuwapeleka watoto wadogo kabisa shule ambao bado wanahitaji uangalizi wa wazazi. 

Kuwapeleka watoto wadogo shule ndiyo imekuwa kama fasheni wengine hata hawajui madhara yake wanaiga tu kwa sababu jirani amewapeleka watoto wake shule ngoja na yeye apeleke ili asije akaonekana anapitwa na fasheni. Waacheni watoto wakuwe vizuri , wacheze kwa maendeleo ya ukuaji wa ubongo watoto wanakuja kuchukia shule kwa sababu ya kuanzishwa mapema unamnyang’anya haki yake ya msingi na unapaswa kujiuliza ukimnyang’anya sasa hivi atakuja kufanya lini?

Hatua ya kuchukua leo, wazazi mnatakiwa kuwalea watoto vizuri na msikubali kuendeshwa na fasheni au mabadiliko ya teknolojia. Upendo kwa watoto ndiyo karama kubwa kuliko kitu kingine. Usikwepe majukumu yako kwa kufurahia umempeleka mtoto mdogo shule za bweni lakini kuwapeleka watoto wadogo wa mwaka mmoja, miwili shule ni kukwepa majukumu tu kama ukichunguza sababu halisi badala ya kuweka sababu nzuri ya niko bize.

Tuna masa 24 tu katika maisha yetu ya siku nzima huwezi kukosa hata saa moja kukaa na familia au watoto wako. Watoto wanapata shida katika hizo shule za mabweni, hata wengine wanakuwa malesbiani na wengine mashoga halafu baadaye unakuja kulalamika kwa nini mtoto wangu yuko hivi na hapo ndipo utakuja kuona kuwa mafanikio uliyokuwa unayatafuta hayana maana yoyote kama familia yako ni mbovu.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi. Asante sana.