Hakuna awezaye kubisha kwamba tunaishi kwenye dunia ambayo ni hasi. Dunia ambayo ukisoma gazeti, kuangalia TV, kusikiliza redio au kuperuzi mitandao ya kijamii, kipaumbele kikubwa ni habari mbaya na zenye kutia hofu.

Tunaishi kwenye dunia ambayo matumizi ya madawa ya kulevya, ulevi na matendo ya ngono na ubakaji yanazidi kuwa mengi.

Dunia hii imekuwa changamoto mno katika malezi ya watoto. Na kwa kuwa hakuna darasa lolote linalofundisha njia bora ya kulea watoto hatua kwa hatua, wazazi wengi wamekuwa wanalea watoto wao kwa mazoea, kitu ambacho ni hatari kwa mazingira ya sasa.

Zig Zigler ambaye alikuwa mwandishi na mhamasishaji mkubwa enzi za uhai wake, aliandika kitabu hichi cha How To Raise Positive Kids In A Negative World, ambapo toleo la kwanza lilitoka mwaka 1985. Lakini changamoto za kipindi hicho, mpaka sasa zipo na zinazidi kuwa kubwa zaidi.

Zigler, kupitia kitabu hichi, anatupa darasa muhimu la kuwalea watoto wetu, ili waweze kuwa na maisha mazuri na yenye mafanikio. Lakini Zigler anaweka nguvu nyingi ya kutusaidia sisi wazazi kuwa na mafanikio kwanza kwa sababu, watoto wanajifunza kwa kuiga yale wazazi wanafanya kuliko wanayosema.

Hichi ni kitabu ambacho kila mtu mwenye mtoto au anayetarajia kuja kuwa na watoto anapaswa kukisoma. Kila ukurasa wa kitabu hichi una madini muhimu kwenye malezi ya watoto.

raising positive kids

Karibu sana kwenye uchambuzi huu wa kitabu hichi kizuri cha malezi, pamoja na uchambuzi huu, pata kitabu hichi na kisome.

 1. Mtazamo wa wazazi unaathiri mtazamo wa watoto.

Watoto wanajifunza kwa kuiga tabia za wazazi kuliko kusikia kile wanachowaambia. Iwapo wewe kama mzazi utakuwa na mtazamo hasi, huo ndiyo mtazamo ambao mtoto ataubeba kwenye maisha yake. Haijalishi utampa moyo kiasi gani na kumwandaa kuwa chanya, kama wewe mwenyewe haupo chanya, unajisumbua.

Hivyo usipoteze muda wako kumwandaa mtoto kuwa chanya kama wewe upo hasi. Na wala usiseme unataka kulea watoto wako wawe na mafanikio wakati wewe hujafanikiwa. Kuyajenga maisha yako katika msingi wa mafanikio kutawanufaisha sana watoto wako.

 1. Malezi ya watoto yanahitaji viungo vingi.

Tofauti na wazazi wengi wanavyolea watoto kwa mazoea, malezi bora ya watoto yanahusisha viungo vingi ambavyo kila mzazi lazima awe navyo. Baadhi ya viungo hivyo ni upendo, nidhamu, uadilifu, kusamehe na vingine. Vyote hivi lazima viwe kwa kila mzazi ili kuweza kuwasaidia watoto kuwa watu bora.

Kwa maana hii, kulea watoto chanya na watakaokuwa na mafanikio makubwa, siyo zoezi rahisi ndiyo maana wengi hukata tamaa na kuacha watoto waende tu kama wanavyoenda.

 1. Misingi miwili muhimu ya kulea watoto chanya.

Msingi wa kwanza; upo hapo ulipo na hivyo ulivyo kutokana na kile ambacho umejifunza siku za nyuma. Ukitaka kuwa tofauti na ulivyo sasa, lazima ubadili kile kinachoingia kwenye akili yako. Kadhalika kwa watoto, kile wanachoingiza kwenye akili zao, kinajitokeza kwenye matendo yao.

Msingi wa pili; maisha ni magumu kwa kila mtu, lakini ukiwa mgumu kwako binafsi, maisha yanakuwa rahisi kwako. Hili linahitaji nidhamu ya hali ya juu sana, na ni muhimu kila mzazi kuwaandaa watoto kwa hilo. Watoto waelewe kwamba dunia siyo rahisi, hata kama wana nafasi kubwa kiasi gani.

 1. Kuna kitu kikubwa ndani ya kila mtoto.

Kila mzazi anapenda mtoto wake awe na malezi mazuri na baadaye aje afanikiwe. Wazazi wengi wanajitahidi sana kuhakikisha watoto wanapata malezi hayo bora, lakini bado maisha yao yanakuja kuwa magumu. Hii ni kwa sababu wengi wanakuwa hawajajua nini kipo ndani ya watoto wao. Wanakuwa hawajajua uwezo wake mkubwa na kuuendeleza, badala yake wanawalazimisha kuwa watu wengine tofauti.

Katika kuwalea watoto wako kuwa chanya na wenye mafanikio, kwanza jua uwezo mkubwa ambao upo kwa kila mtoto, kisha msaidie kwenye kufikia uwezo huo. Atakuwa na maisha bora sana.

 1. Ulimwengu hasi ukoje?

Ulimwengu hasi umejawa na kauliza kushindwa na kukata tamaa. Hizi ni kauli ambazo mzazi anaweza kuwa anatumia kila siku, kwa mazoea lakini zinajenga mtazamo hasi kwa mtoto na anaiona dunia kwa mtazamo wa tofauti.

Kila kitu kinachukuliwa kwa hali ya kutisha na ya hatari. Kila taarifa ya habari ina habari za kifo, wizi, ajali na kadhalika. Na kila mtu anapotaka kufanya jambo, anaanza kwa kujiambia kwamba hawezi au atashindwa.

Haya yote yanazalisha watu ambao wapo hasi na hawawezi kufanikiwa kamwe.

SOMA; Ifahamu Sehemu Iliyogeuka Kuwa Kimbilio La Wazazi Wengi Katika Malezi Ya Watoto.

 1. Kuangalia TV kusikodhibitiwa ni sumu kwa mtoto.

Iwapo mtoto anaangalia TV anavyojisikia yeye mwenyewe, bila ya usimamizi wa mzazi, mtoto huyo yupo kwenye hatari kubw aya kuharibika, hasa kwa wale wadogo ambao wanapenda kujaribu kila wanachojifunza.

Huwezi kuangalia TV za kawaida ikapita dakika kumi watu hawajagombana, kufanya mapenzi, kunywa pombe au jambo lolote hasi kutokea.

Ni wajibu wako mzazi kuchagua vipindi gani mtoto anaweza kuangalia, ambavyo vina maadili na mtoto anajifunza kadiri ya umri wake.

 1. TV pia zinaharibu afya za watoto.

Mtoto anapotumia muda mwingi kuangalia TV, hapati muda wa kutosha wa kucheza na wengine. Hivyo anakosa ule uchangamfu wa utoto, muda wote amekaa na hata afya yake inakuwa siyo nzuri, anaweza kuwa na uzito unaopitiliza, hasa pale anapoangalia TV huku akila.

Ni jukumu la mzazi kumfanya mtoto apende michezo inayohusisha mazoezi ya viungo, hii pia itamsaidia kujenga ushirikiano na wengine. Na wakati mwingine, wewe mzazi cheza na watoto wako.

 1. Njia bora ya kumlinda mtoto dhidi ya wabakaji na walawiti.

Matukio ya watoto kutekwa, kubakwa na kulawitiwa yanazidi kuwa mengi katika nyakati hizi. Matukio haya yanafanywa na watu ambao ni wa karibu kabisa kwa mtoto au wenye mamlaka ambayo watoto hawawezi kuyapinga.

Njia bora ya kuepusha hili ni kujua kila wakati mtoto wako yuko wapi, yuko na nani na anafanya nini. Usiruhusu kabisa mtoto wako kuwa eneo ambalo hujui, hata kama yupo na ndugu au mtu unayemwamini kiasi gani. Wengi wanaoharibu watoto ni watu wanaoaminika sana.

Kitu kingine muhimu ni kujenga ukaribu na mtoto ili asikufiche kitu chochote cha ajabu ambacho ameambiwa au ametaka kufanyiwa. Hili litakusaidia kukatisha mapema jaribio la kuharibiwa kwa mtoto, maana wengi wanaoharibu watoto, huanza kidogo kidogo ili kujenga uaminifu kwa watoto.

 1. Jua kuna vitu huwezi kuwafanyia watoto wako.

Kosa kubwa ambalo limekuwa linafanywa na wazazi, hasa wale ambao wana mafanikio makubwa, ni kufikiri wanaweza kufanya kila kitu kwa watoto wao. Hivyo hujaribu mpaka kununua matatizo ya watoto wao, wakiona wanawasaidia wasipate shida.

Lakini ukweli ni kwamba lazima watoto wajue maisha ni magumu na dunia ina changamoto. Lazima wajue wataumizwa, wataumwa, watakatishwa tamaa. Pia lazima wajue kwamba wakikosea dunia itawaadhibu kwa njia yoyote ambayo ni sahihi. Kwa kuwafundisha hayo, unawaandaa kukumbana na hali halisi ya dunia.

 1. Kama mafanikio yako yataharibu watoto wako, haina haja ya kufanikiwa.

Kumekuwa na jambo la kushangaza sana kwenye maisha ya zama hizi, watu wanakimbizana na mafanikio, hasa ya mali na fedha na kusahau kabisa kuhusu watoto wao. Wanafanya hivyo wakiamini kwamba wanawasaidia watoto kwa kuwa na maisha mazuri. Kumbe wanawaharibu zaidi watoto.

Watoto wanahitaji uwepo wa wazazi wao katika kipindi cha ukuaji wao kuliko kitu kingine chochote kile. Hivyo kama mafanikio kwako yanamaanisha kuwa mbali na familia yako, kukosa muda kabisa na watoto wako, mafanikio hayo hayatakuwa na maana yoyote kwako wala watoto wako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Boys Of Few Words (Jinsi Ya Kuwalewa Watoto Wa Kiume Wawe Na Mawasiliano Bora Na Mahusiano Mazuri Na Wengine.)

 1. Kama unampenda mtoto wako mpe MUDA.

Mapenzi kwa watoto ni muda na siyo kitu kingine chochote. Mtoto anapopata muda wako, hasa pale anapokuhitaji kweli, anafarijika mno. Mtoto anapoingia duniani, hasa pale anapoanza shule, anakutana na changamoto nyingi kila siku. Anahitaji mtu wa kumshirikisha changamoto hizo, ambaye atazielewa na kumsaidia kuzitatua. Kwa bahati mbaya mzazi anakuwa hayupo karibu, yupo bize na kazi na hata muda mchache anaopata, hawezi kutenga wa kukaa na watoto.

Hili linapelekea watoto kupata ushauri wao kwa watu wabaya, ambao wanawaharibu kwa kuwabaka, kuwalawiti, kuwafundisha ulevi na hata tabia nyingine mbaya.

 1. Tabia za mafanikio mtu unaweza kujifunza na kuwafundisha watoto.

Tabia zozote ambazo tunaziona kwa watu waliofanikiwa, tunaweza kuzijenga kwetu binafsi na pia kuwasaidia watoto wetu kuwa nazo pia. Lakini hili linahusisha kazi kubwa na hivyo lazima mzazi uwe tayari kwa kazi hii. Ukitaka kupeleka malezi kama wengi wanavyopeleka, ya kuacha mtoto aende anavyoenda, mtoto anakosa msingi muhimu wa maisha ya mafanikio.

Kwa kujifunza tabia hizi za mafanikio, unamsaidia mtoto kuweza kutambua na kutumia uwezo mkubwa ambao upo ndani yake.

 1. Watoto wanahitaji msingi imara wa maadili.

Bila ya maadili, watoto hawawezi kuwa na maisha mazuri, wataishia kwenye ulevi au jela. Dunia ina changamoto nyingi, mtoto akilelewa kwamba anaweza kwenda kama anavyotaka yeye, kupata kila anachotaka bila ya kipingamizi, ataishia pabaya mno.

Ni wajibu wa mzazi kumjengea mtoto msingi imara wa maadili ambao unahusisha uaminifu, kuheshimu sheria, kujali wengine na uvumilivu.

Katika kuwafundisha watoto maadili haya, tukumbuke kwamba watoto wanatuangalia kuliko wanavyotusikiliza. Kama unamfundisha mtoto kwamba uaminifu ni msingi muhimu kwenye maisha, halafu dakika chache baadaye anakusikia ukiongea na simu na kusema upo kazini wakati upo nyumbani, mtoto atabeba kile ulichofanya, kwamba kudanganya siyo jambo baya.

 1. Tabia nzuri ni usalama na mtaji wa kutosha.

Msingi muhimu sana ambao mzazi anapaswa kumjengea mtoto ni katika kujenga tabia nzuri. Mafanikio yoyote kwenye maisha, yanategemea zaidi kwenye tabia ambayo mtu anayo.

Mtoto anapolelewa kwa kujengewa tabia nzuri, kila mtu anamwamini na unakuwa usalama wake kwenye kazi na hata biashara. Pia tabia nzuri ni mtaji, kwa sababu watu wanathamini tabia nzuri kuliko kitu kingine chochote. Hakuna mtu mwenye tabia nzuri, mwaminifu ambaye amewahi kukosa kazi ya kufanya na akawa masikini kabisa.

 1. Wafundishe watoto kulinda majina yao na sifa zao.

Jina linabeba maana kubwa sana kwenye maisha ya mtu. Jina la mtu linapotajwa mahali, kuna picha ambayo watu wanaipata, hata kama mtu huyo hayupo.

Lazima watoto wafundishwe kulinda majina yao, kwa kuhakikisha yanaendana na sifa nzuri. Jina linapotajwa mahali, watu wawe na amani na kupata picha ya mtu mwaminifu na anayeweza kutegemewa.

Jina linaweza kumfanya mtu kuaminiwa na kupewa kitu ambacho wengine hawawezi kupewa. Wasaidie watoto kujenga na kulinda majina yao.

Katika kulinda majina yao, wasijihusishe kabisa na watu wenye sifa mbaya, wala kujaribu kufanya jambo lolote ambalo litaharibu sifa na majina yao.

 1. Angalia kitu kuzuri kilichopo kwa kila mtoto.

Wakati mwingine wazazi wanakata tamaa na kuona watoto hawawezi kuwa chanya na wenye mafanikio. Hili linatokana na mtoto kuwa na mapungufu mengi, labda anafeli shuleni, ni mtundu, hasikii na mengine mengi.

Lakini pamoja na yote hayo, kila mtoto ana kitu kizuri ambacho kipo ndani yake. Hata kama darasani anakuwa wa mwisho, kipo kitu ambacho anaweza kukifanya vizuri. Hapo ndipo mzazi unapotakiwa kuanzia katika kumlea mtoto mwenye mtazamo chanya na atakayefanikiwa.

Unapokazana kuangalia kitu kizuri ambacho kipo ndani ya mtoto, unaziona fursa nyingi za kumsaidia kuwa bora zaidi. Na hilo linampelekea yeye kuwa hasi, kuona kuna vitu anaweza na hata kufanikiwa kwenye maisha.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wazazi Wa Kizazi Kipya (Kama Una Miaka Chini Ya 40 Soma Hapa).

 1. Kumpuuza mtoto kuna matokeo mabaya kuliko kumkatisha tamaa.

Mwaka 1984 utafiti uliofanywa na Family Concern, ulihusisha watoto wa shule 60, ambao waligawanywa kwenye makundi matatu na kupewa majaribio ya mtihani wa hesabu kula siku kwa siku tano. Kundi la kwanza walikuwa wanasifiwa kila siku kwamba wana akili na wanafanya vizuri. Kundi la pili walikuwa wanakatishwa tamaa na kukosolewa kila siku. Na kundi la tatu waliachwa tu, hawakuambiwa chochote.

Matokeo sasa, wale waliosifiwa kila siku, matokeo yao yalikuwa yanakuwa bora zaidi kila siku. Wale waliokuwa wanakosolewa walionesha kuwa bora, lakini siyo sana ukilinganisha na waliosifiwa. Ila wale ambao hawakuambiwa chochote, matokeo yao hayakuwa na mabadiliko yoyote.

Utafiti huu unaonesha namna gani kuwapuuza watoto kunawafanya wakate tamaa na wasione uhitaji wa kuwa bora zaidi. Na hili ndilo linafanywa na wazazi walio wengi. Watoto wanakazana kufanya yao na wazazi wanafanya yao, hakuna msaada wa karibu watoto wanapata kutoka kwa wazazi, hasa kwenye masomo na changamoto nyingine.

 1. Kuwa chanya ni kazi ya kila siku, kama kuoga.

Inashangaza namna ambavyo watu wanachukulia kirahisi swala la kuwa chanya. Watu wanafikiri kwa kusoma kitabu kimoja, au kuhudhuria semina moja, basi wanatosha kuwa chanya na kufanikiwa.

Hivi ukioga mara moja ndiyo umetakata milele, au ukila mara moja basi umeshiba milele? Kama ambavyo tunaoga na kula kila siku, tunapaswa kujifunza kuwa chanya kila siku, kwa kusoma na kusikiliza vitu chanya kila siku. Kwa sababu kila siku dunia inatulazimisha kuwa hasi.

Tengeneza msingi huu kwa watoto wako pia, wawe tayari kujifunza kila siku na kuwa chanya.

 1. Njia ya uhakika ya kuwafanya watoto wako wasikose kazi.

Wajengee msingi wa kufanya zaidi ya wanavyolipwa. Dunia nzima inafanya kazi kwa uvivu, watu wanataka kupata zaidi ya kile wanachowekwa, na hili limesababisha wengi kukosa kazi, na hata wakianzisha biashara zinakufa. Ukitaka watoto wako wapate kazi wakati wote, na hata wakijiajiri wafanikiwe, basi wajengee msingi wa kufanya zaidi ya wanavyolipwa. Wawe tayari kwenda hatua ya ziada. Wakazane kutoa thamani zaidi badala ya kuangalia wanalipwa nini kwanza.

Ni sheria ya asili kwamba, pale mtu anapofanya zaidi ya anavyolipwa, wanafikia hatua ya kulipwa zaidi ya wanavyofanya. Dunia inaenda kinyume na sheria hii, wajenge watoto wako waende nayo vizuri.

 1. Malezi ya mtoto hayana kuchelewa.

Wakati sahihi wa kutoa malezi bora kwa mtoto wako ni wakati wowote ambao upo na mtoto wako. Na kama mtoto bado yupo chini yako, hujachelewa kwenye kumjengea misingi ya maisha ya mafanikio.

Japo kama watoto wameshakua na kujenga misingi tofauti, zoezi litakuwa gumu, lakini linawezekana. Hata kama hutafanikiwa kwa asilimia 100, kipo kitu ambacho utakijenga kwa watoto wako.

Hivyo usijiambie umechelewa, tumia nafasi uliyonayo kuhakikisha watoto wako wanakuwa chanya na kufanikiwa kwenye maisha yako.

 1. Utatu katika malezi ya mtoto.

Sisi binadamu tumegawanyika kwenye utatu wa mwili, akili na roho. Wazazi wengi wamekuwa wakikazana na maeneo mawili, moja zaidi la akili, na kidogo kwenye mwili lakini kusahau kabisa kwenye roho.

Kwenye akili, hakikisha mtoto anapata elimu bora kabisa kwake, anajifunza mambo chanya na yenye msaada.

Kwenye mwili hakikisha mtoto anapata chakula chenye afya na kufanya mazoezi ya viungo, pia msaidie kujikinga na magonjwa.

Kwenye roho, msaidie mtoto kukua kiimani, Sali naye pamoja, nenda naye nyumba ya ibada na pia msaidie kujua maana ya maisha na kusudi lake hapa duniani.

Mtoto akikua katika utatu huu, lazima atakuwa na mafanikio makubwa.

 1. Muda wa wazazi unahitajika kwa malezi bora ya watoto.

Kwa zama tunazoishi, ambapo asilimia kubwa ya wazazi wote wawili wanafanya kazi, jukumu la malezi ni kama limekodishwa kwa vituo vya kulelea watoto, wasaidizi wa ndani au shule za bweni.

Kwa aina hii ya maisha tunawanyima watoto wetu fursa ya kuwa na misingi mizuri ya maisha, kwa sababu yeyote tunayemkodishia kazi hiyo, kwa sababu sisi tupo bize, hana muda wa kutosha kwa watoto wetu.

Ni vyema pamoja na ubize wa zama hizi, kila mzazi atenge na kulinda muda wa malezi kwa watoto. Hili ni jukumu ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

 1. Watoto wanaolelewa na wazazi wawili wana nafasi ya kufanikiwa kuliko wanaolelewa na mzazi mmoja.

Tafiti nyingi zimekuwa zinaonesha kwamba watoto wanaolelewa na mzazi mmoja, hasa mama, wamekuwa wakidhurika zaidi kuliko wanaolelewa na wazazi wawili. Watoto wengi wa mtaani utakuta wamelelewa na mzazi mmoja au mzazi alipewa ujauzito na kutekelezwa. Watoto wengi wanaoishia kwenye ulevi, matumizi ya madawa, wizi na hata ukahaba, wanatoka kwenye familia ya kulelewa na mzazi mmoja.

Ni muhimu sana kwa wazazi kuhakikisha wanashirikiana kuwalea watoto wao ili kupata msingi mzuri wa maisha ya mafanikio.

 1. Mtazamo wa mtoto unajengwa na mambo makuu matatu;

Moja; imani, watoto wengi wanaanza kujenga imani kwa wazazi wao. Lazima uwawezeshe kujenga imani nzuri ya kiroho na kwao binafsi.

Mbili; matumaini, chochote ambacho tunafanya kwenye maisha, ni kwa matumaini, mjengee mtoto uwezo wa kutumaini kwenye lolote wanalofanya.

Tatu; upendo, upendo ndiyo unatawala kila kitu, mtoto anapokuwa na upendo, maisha yanakuwa bora sana kwake.

 1. Malezi ya watoto ni kazi, tena ambayo ni muhimu mno.

Wapo wazazi ambao wanafanya kazi na kukosa muda wa kulea watoto wao, ambapo ukipiga mahesabu vizuri, unakuta wanapoteza fedha nyingi kuliko wanazopata kupitia kazi wanazofanya. Lakini wazazi wa aina hii, wanaona kazi ni muhimu kwa sababu wakiacha na kuelea watoto, watadharaulika.

Zoezi la kulea watoto linadharaulika kwenye jamii na kuonekana ni la watu ambao hawana elimu au hawawezi kupata kazi. Na hii imechangia kuharibika sana kwa maadili ya watoto. Wewe kama mzazi, kama unaona ni muhimu kwa watoto wako kupata malezi bora kutoka kwako, na hivyo kupunguza kazi unazofanya au  hata kuacha kama yupo mwingine anayefanya kazi, usiogope na kuona utachukuliwa ni mtu wa chini. Zoezi la kulea watoto ni kubwa na muhimu. Uwekezaji unaofanya sasa, utakulipa sana mbeleni kwa kuwa na familia bora ya watoto wenye mafanikio.

Kama ambavyo tumejifunza kwenye uchambuzi huu mfupi, zoezi la malezi kwa watoto siyo rahisi, lakini linawezekana hasa pale wazazi wanapojitoa na kushirikiana. Kama wewe ni mazazi au unapanga kuwa na watoto baadaye, soma kitabu hichi. Kupata kitabu hichi bure kabisa, jiunge na kundi la AMKA MTANZANIA telegram. Bonyeza maandishi haya kujiunga.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz