Ukitumia muda wako mwingi kuangalia, kusikiliza au kusoma habari utaondoka na hitimisho moja, dunia ni mbaya na inazidi kuwa mbaya kila siku. Utaona kwenye habari jinsi habari za vita na mapigano zinavyopewa kipaumbele, jinsi ambavyo umasikini unazidi kukua kwa kasi, hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa na hata matishio ya magonjwa na vitendo vya kigaidi. Ukiwa mfuatiliaji mzuri wa habari, na ukawa mtu mzuri wa kushiriki mijadala na wengine, utakubali kabisa kwamba dunia ni mbaya na inazidi kuwa mbaya.

Lakini sivyo ambavyo aliyekuwa mwandishi na daktari wa binadamu Hans Rosling ambaye alitenga maisha yake yote ya kazi kuielewa dunia, alivyoiona dunia. Kupitia takwimu na kusafiri karibu kila eneo la dunia, Hans anatuambia kwamba dunia haijawahi kuwa nzuri kama sasa. Yaani hakuna kipindi ambacho maisha yamekuwa bora hapa duniani kama kipindi hichi tunachoishi.

Umasikini unapungua, afya zinaimarika, vifo vinapungua, vita na mapigano vinapungua na hata magonjwa hatari yamedhibitiwa sana. Kupitia takwimu mbalimbali, Hans anatuonesha jinsi ambavyo dunia imepiga hatua na mambo yanakuwa mazuri.

Hans anatuonesha pia kwamba watu wengi hawayaoni maendeleo makubwa yanayotokea duniani, kwa sababu wanafikiria kwa kutumia takwimu na uzoefu wa nyuma. Kupitia maswali yake ambayo amekuwa akiuliza watu kwenye maeneo mbalimbali, watu wamekuwa wakitoa majibu yasiyo sahihi, ikionesha kwamba watu hawana uelewa sahihi wa dunia.

Kwenye kitabu chake hichi cha mwisho, FACTFULLNESS, Hans anatuonesha maeneo kumi ambayo tunakosea kuhusu dunia na kwa nini mambo ni mazuri kuliko unavyofikiri.

factfullness

Bill Gates, mmoja wa watu matajiri sana duniani, na ambaye kwenye kitabu hichi ametajwa kama mmoja wa watu waliochangia maisha kuwa bora sana hapa duniani, hasa kwa upande wa afya, anasema kitabu hichi, FACTFULLNESS, ni kitabu ambacho kila mtu anapaswa kukisoma.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, tuweze kuona wapi tunakosea kuhusu dunia na kuweza kujua ukweli na hatua sahihi za kuchukua.

ENEO LA KWANZA TUNALOKOSEA; SILIKA YA MGAWANYIKO WA DUNIA KWENYE MAKUNDI MAWILI.

Kila mtu anapozungumzia au kufikiria dunia basi hufanya hivyo kwa kufikiria makundi mawili. Kundi la kwanza ni nchi tajiri, au nchi zilizoendelea au nchi za magharibi au nchi za dunia ya kwanza kama inavyotumiwa na wengi. Na kundi la pili ni nchi masikini, au nchi zinazoendelea au nchi za mashariki na kusini au nchi za dunia ya tatu.

Watu wengi wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea huwa wanaona dunia nzima ni masikini isipokuwa wao. Mwandishi anakataa mgawanyiko huu wa dunia kwenye makundi mawili. Mwandishi anasema njia bora ya kuigawa dunia ni kwenye makundi manne, ambazo ni ngazi za kimaendeleo ambazo kila nchi imepitia.

Zifuatazo ni ngazi nne za kimaendeleo, ambazo kwenye kila nchi kuna watu kwenye kila ngazi, na ukweli ni kwamba watu wengi wapo katikati na siyo masikini sana au matajiri sana.

 1. Ngazi ya kwanza; kipato cha dola moja kwa siku (sawa na shilingi 2500 kwa siku).

Hii ndiyo ngazi ya chini kabisa ya kipato, ambapo familia inaishi kwa dola moja kwa siku. Katika ngazi hii maisha ni magumu sana. Chakula ni duni, usafiri ni kutembea kwa miguu na muda mwingi watu wanatumia kutembea kwenda kutafuta maji au kuni kwa ajili ya kupika. Chakula kinacholiwa ni kile kile muda wote. Watu waliopo kwenye ngazi hii hawawezi kumudu au kufikia huduma za kiafya mapema na hivyo vifo vinakuwa vingi na afya dhoofu.

Kwa makadirio watu bilioni moja wanaishi kwenye ngazi hii duniani kote, na kwa sehemu kubwa wapo bara la Afrika na Asia.

 1. Ngazi ya pili; kipato cha dola 4 kwa siku (sawa na shilingi elfu 10 kwa siku).

Kwenye ngazi ya pili ya kipato, angalau mambo ni nafuu kidogo, kipato hakiishii kwenye chakula tu, bali familia inaweza kumudu kupata mavazi na malazi, inaweza kubadili chakula angalau siyo kimoja wakati wote. Pia usafiri kwenye ngazi hii ni baiskeli, hivyo zoezi la kutafuta maji halichukui muda mwingi wa siku.

Kwenye ngazi hii maisha yanaweza kuonekana ni bora kidogo, lakini bado siyo ya uhakika, changamoto moja ya kiafya inayohitaji gharama kubwa za matibabu inaweza kuirudisha familia kwenye ngazi ya kwanza.

Kwa wastani, watu bilioni tatu wanaishi kwenye ngazi hii dunia nzima, wengi Afrika na Asia.

 1. Ngazi ya tatu; kipato dola 16 kwa siku (sawa na shilingi elfu 40 kwa siku).

Hapa kidogo maisha yanaonekana kuwa mazuri, mtu anafanya kazi maeneo tofauti, masaa 16 kwa siku na siku saba za wiki. Ana uwezo wa kuweka akiba, kubadili chakula na kuwa na mavazi na malazi. Ana uwezo wa kuwa na bomba nyumbani hivyo muda haupotei kutafuta maji, na anaweza kumudu jiko la gesi hivyo muda haupotei kutafuta kuni. Usafiri ni pikipiki ambayo inamwezesha mtu kwenda kazini eneo ambalo ni mbali na nyumbani.

Ngazi hii ipo bora kiafya na kielimu kwa sababu kipato kinawezesha watoto kusoma na akiba kuwepo pale inapotokea changamoto ya kiafya. Kwa wastani, watu bilioni mbili wapo kwenye ngazi hii dunia nzima.

 1. Ngazi ya nne; kipato dola 64 kwa siku (sawa na shilingi laki moja na nusu kwa siku).

Hii ni ngazi ya juu ya kipato, ambapo mtu anaweza kumudu chochote anachotaka, chakula ni kizuri, mavazi, makazi na malazi ni bora, usafiri ni gari na huduma za afya ni bora kabisa. Kwenye ngazi hii mtu ana zaidi ya miaka 12 shuleni, una uwezo wa kuwa na maji ndani ya nyumba, na kusafiri maeneo ya mbali kwa mapumziko na familia.

Kwa wastani watu bilioni moja wanaishi kwenye ngazi hii duniani kote, na wengi nchi za magharibi na kaskazini yaani Amerika na Ulaya.

 1. Ngazi za vipato ni hatua ambazo kila nchi imepitia.

Kama ambavyo tumeona kwenye ngazi hizo nne, katika watu bilioni saba waliopo duniani, bilioni moja wapo kwenye umasikini wa kutupwa na bilioni moja wapo kwenye tajiri, kuna watu bilioni 5 ambao hawapo kwenye umasikini wa kutisha, lakini pia hawapo kwenye utajiri, hawa huwa hawaonekani tunapoigawa dunia kwenye kundi la masikini na matajiri.

Hivyo silika ya kugawa dunia kwenye makundi mawili inatufanya tusione ukweli kuhusu dunia. Tunaweza kuona watu bilioni moja ndiyo matajiri na wengine wote ni masikini lakini siyo kweli. Hata kwenye nchi masikini kabisa duniani, kuna watu kwenye kila ngazi, mpaka ngazi ya nne.

Kwa mfano Tanzania inawekwa kwenye kundi la nchi masikini, lakini kama unasoma hapa, ina maana upo kwenye ngazi ya tatu au ya nne, na siyo chini ya hapo. Mtu aliyepo ulaya na hajawahi kufika Tanzania, anaweza kufikiri watu wote wana maisha magumu na wanaishi kwa dola moja kwa siku, kitu ambacho siyo sahihi.

Kwa kujua mgawanyiko sahihi wa utajiri kwa watu duniani, inasaidia kujua hatua sahihi kuchukua.

Kwa mfano, umasikini unaendana na afya mbovu kitu ambacho kinasababisha vifo kuwa vingi, hivyo kujua yale maeneo yenye umasikini wa kupindukia kutasaidia kuboresha afya na kupunguza vifo.

 1. Jinsi ya kuondokana na silika ya kugawa dunia kwenye makundi mawili.

Ili kuondokana na silika hii ya kugawa dunia kwenye makundi mawili, ambayo siyo sahihi, fanya yafutayo;

Moja; kuwa makini na mlinganisho na wastani, kwa wastani vitu vinaweza kuonekana kuwa kwenye makundi, lakini kwa kuangalia kitu kimoja kimoja, utagundua vinatofautiana.

Mbili; kuwa makini na kuchukua kwenye ncha. Wengi hupenda kuangalia juu kabisa na chini kabisa na kusahau katikati, vitu vingi huwa havipo juu kabisa wala chini kabisa, huwa vinakuwa katikati.

Tatu; kuwa makini unapoangalia ukiwa juu. Ukiwa juu ya ghorofa, nyuma zote ambazo siyo ghorofa huwa zinalingana, lakini ukishika chini utakuta nyumba hizo hazilingani. Kadhalika unapokuwa juu unaweza kuona walio chini wote ni sawa, ni mpaka ufike kule walipo ndipo utaona wanatofautiana.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Raising Positive Kids In A Negative World (Jinsi Ya Kulea Watoto Wenye Mtazamo Chanya Kwenye Dunia Hasi).

ENEO LA PILI TUNALOKOSEA; SILIKA YA KUFIKIRIA UPANDE HASI.

Ukiangalia habari, ukisikiliza watu na kutembelea mitandao utakutana na kila aina ya ujumbe mbaya kuhusu mambo mabaya yanayotokea duniani. Ajali, mapigano, vita, mtu kumuua mwingine, magonjwa ya mlipuko na vitu vingine vinavyotishia usalama wetu.

Lakini je huu ndiyo uhalisia? Ni kweli kwamba dunia inazidi kuwa mbaya kadiri siku zinavyokwenda? Hans anatuambia hapana, dunia inazidi kuwa bora zaidi, lakini sisi binadamu tunapenda habari hasi kuliko habari chanya.

Kwa mfano watu wengi wanasafiri kwa ndege, meli, magari na kufika salama kila siku, hutaona hayo kwenye habari, ila ikitokea ajali moja basi siku nzima itajadiliwa ajali hiyo na kuonesha kwa jinsi gani ajali zinazidi kuwa mbaya. Wakati ukichukua kwa ulinganisho, ajali zinazidi kupungua kadiri siku zinavyokwenda.

 1. Ukweli kuhusu dunia.

Hans anatuonesha kupitia takwimu na uhalisia wa dunia kwamba;

Vita vikubwa vimepungua duniani, tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia, hakuna vita kubwa ambayo imeshasumbua dunia mpaka sasa. Ukiondoa hali ya vita kwenye mataifa kama Syria na mengine, kwa ujumla dunia ipo salama kuliko kipindi kingine chochote.

Matukio ya kigaidi yamepungua sana duniani, japo bado yapo, lakini hakuna mauaji mengi kama ambavyo wengi wanafikiri.

Miaka 20 iliyopita, asilimia 29 ya watu duniani walikuwa wanaishi kwenye umasikini uliopitiliza, ngazi ya kwanza, sasa hivi ni asilimia 9 tu ya watu duniani wanaoishi kwenye ngazi hiyo ya kwanza.

Kwa ujumla, dunia inapiga hatua, japo nyingi ni kidogo kidogo, lakini watu tunapenda kuona mabaya machache na kuona ndiyo dunia ilivyo.

 1. Vitu vitatu ambavyo vinachochea silika ya kuangalia mambo hasi.

Haitokei tu kwa bahati mbaya kwamba watu tunapenda kufuatilia mambo hasi kuliko chanya, kuna vitu vitatu vinavyochochea watu kuangalia mambo hasi zaidi ya chanya;

Moja; kusahau nyuma. Watu wengi huamini siku za nyuma mambo yalikuwa mazuri kuliko sasa, lakini ukweli ni kwamba wanakuwa tu wamesahau jinsi ambavyo mambo yalikuwa magumu ukilinganisha na sasa. Kumbuka miaka kumi iliyopita ilikuwa rahisi kiasi gani kwako kuwasiliana na mtu aliyepo mbali, au kupata huduma ya afya.

Mbili; uchaguzi wa vyombo vya habari. Biashara ya vyombo vya habari ni kupata watu, na watu wanapenda mambo yanayosisimua na kuibua hisia, hivyo vyombo vya habari vinapopata habari ya kusisimua na kuibua hisia, ambazo ni habari hasi, vinatumia habari hiyo vizuri kuwapata watu. Ndiyo maana kurasa za mbele za magazeti na hata habari mpasuko huwa ni za mambo mabaya yanayotokea.

Tatu; kujisikia vibaya kusema mambo ni mazuri. Ukweli ni kwamba siyo kwamba kila kitu kinaenda sawa duniani, lakini pia siyo kila kitu ni kibaya. Wengi wanaogopa kusema dunia inakuwa nzuri kwa sababu bado kuna mambo mabaya yanaendelea.

 1. Jinsi ya kuondokana na silika ya kuangalia upande hasi.

Ili kuondokana na silika hii ya kuangalia upande hasi zaidi, tegemea kukutana na habari mbaya, halafu;

Moja; jifunze kutofautisha nzuri na mbaya, kwamba hata kama mambo ni mabaya kiasi gani, bado kuna uzuri fulani ndani yake.

Mbili; habari nzuri siyo habari. Katika kila habari mbaya unayoiona kwenye vyombo vya habari, jua kuna habari 100 nzuri zimetokea pia, lakini hutaziona kwenye vyombo vya habari, kwa sababu siyo habari.

Tatu; maendeleo madogo siyo habari pia. Kuna maendeleo madogo madogo yanayofanyika kwenye kila eneo duniani, lakini pia hutayaona kwenye habari.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The 67steps (Njia Rahisi Ya Kuwa Na Maisha Mazuri).

ENEOLA TATU TUNALOKOSEA; SILIKA YA MSTARI NYOOFU.

Ipo dhana inayoaminiwa na wengi kwamba idadi ya watu duniani inaendelea kuongezeka siku hadi siku. Kwamba ukiweka takwimu kwenye ghafu, basi itakupa mstari nyoofu, ikimaanisha kwamba watu wataendelea kuongezeka mpaka itafika hatua dunia haiwezi kuwatosha tena watu.

Huu siyo ukweli, hakuna mstari wowote unaoendelea kuwa nyoofu, na kwa idadi ya watu duniani, haiwezi kuendelea kuongezeka bila kikomo. Itafika mahali na kufikia ukomo ambao hauwezi kuongezeka tena.

 1. Kadiri watu wanavyoondoka kwenye umasikini, ndivyo idadi ya watoto inavyopungua.

Umasikini unahusishwa na idadi kubwa ya watoto, ni masikini duniani lote ambao utakuta wana watoto watano na kuendelea. Wanafanya hivi kwa sababu mbalimbali, na sababu kubwa ni umasikini wenyewe.

Mtu anapokuwa masikini, huduma za afya kwake zinakuwa ngumu, hivyo watoto wengi anaozaa wanakufa wakiwa wachanga, hili linamfanya azae wengi zaidi ili hata wakifa abaki na wachache. Pili kwa kuwa mtu ni masikini, basi anazaa watoto wengi akiamini watakuja kumsaidia baadaye.

Mtu anapoondoka kwenye umasikini, hasa wa ngazi ya kwanza, anaweza kumudu huduma za afya, anaweza kupata elimu na pia anakuwa na kipato cha juu kidogo. Vyote hivi vinasababisha watu kuzaa watoto wachache zaidi.

Njia pekee ya kupunguza idadi ya watu duniani na kuyafanya maisha ya watu kuwa bora zaidi, ni kuondoa umasikini kwa watu.

 1. Jinsi ya kuondokana na silika ya mstari nyoofu.

Vitu vingi kwenye dunia havifuati mstari nyoofu, kuna mistari iliyopinda, mistari inayopanda na kushuka na mistari inayopanda kisha kufika ukomo. Kadiri maisha ya watu yanavyozidi kuwa bora, ndivyo idadi ya watu inazidi kupungua duniani.

ENEO LA NNE TUNALOKOSEA; SILIKA YA HOFU.

Sisi binadamu hatuna muda wa kutosha kuweza kuchunguza kila kitu kwa undani, hivyo kujiepusha kuingia kwenye matatizo na vitu tusivyovijua, huwa tunakuwa na hofu na vitu hivyo. Ndiyo maana watu wengi wamekuwa hawapendi kubadilika, kwa sababu hawana uhakika na mabadiliko wanayopaswa kuchukua.

Hali hii ya hofu imekuwa inatuzuia pia kuona ukweli na kuona jinsi ambavyo dunia inapiga hatua. Vyombo vya habari pia vimekuwa vinatumia hofu zetu kama mtaji wao, vinasambaza zaidi habari zinazoibua hofu kuliko habari zisizo na hofu.

 1. Hofu inatufanya tusione hatari halisi.

Mwaka 2015 kwa siku 10 walikufa watu elfu 9 kutokana na kimbunga. Hii ilikuwa habari kubwa ambayo ilipewa uzito mkubwa duniani na kila mtu alikuwa na hofu ya nini kitatokea. Vyombo vya habari vilikuwa vinarusha mubashara kila kinachoendelea huku dunia nzima ikiangalia kwa hofu. Katika kipindi hicho hicho, watoto elfu 9 walikufa dunia nzima kwa ugonjwa wa kuharisha, kwa kutumia maji ambayo siyo safi na salama. Lakini hakuna chombo hata kimoja cha habari kiliripoti vifo vya watoto hao, ambavyo vingeweza kuzuilika kwa urahisi zaidi. Hofu inawafanya watu kuangalia eneo moja na kupuuza maeneo mengine ambayo ni hatari zaidi.

 1. Hofu inaweza kuleta vifo kuliko hata kile kinachohofiwa.

Kumekuwa na habari mbalimbali ambazo zinaonesha vitu fulani kuwa hatari, kwa mfano habari zinazohusu kemikali za sumu, ambapo watu wanaacha kutumia vitu fulani kwa kuhofia vinasumu. Pia hofu za milipuko au matukio ya ugaidi zimefanya watu kukimbia au kuhama maeneo ambayo mambo hayo huwa hayatokei.

 1. Jinsi ya kuishinda silika ya hofu.

Hofu ni kitu kizuri, iwapo inatufanya kujua vizuri kitu kabla ya kuchukua hatua, lakini kama hofu inatuzuia kuchukua hatua kabisa, au tunachukua hatua ambazo ni mbaya kwetu, basi hofu inakuwa siyo nzuri tena kwetu.

Kudhibiti silika hii ya hofu unahitaji kukokotoa kiwango cha hatari halisi, angalia ni kwa kiasi gani uhusika wako moja kwa moja unahatarisha hali yako kwenye kile unachohofia. Pia tulia kabla hujafanya maamuzi ukiwa kwenye hofu, kwa sababu hofu inapokutawala huwezi kufanya maamuzi sahihi.

ENEO LA TANO TUNALOKOSEA; SILIKA YA UKUBWA.

Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kuona vitu kwa ukubwa ambao siyo halisi, huwa tunaona vitu ni vikubwa kuliko vilivyo au vidogo kuliko vilivyo kwa uhalisia, na hilo linatuzuia kuona ukweli wa dunia.

 1. Njia bora ya kupunguza vifo ni kuzuia magonjwa na siyo kuyatibu.

Mwandishi anatushirikisha kwamba wakati akiwa daktari pekee kwenye wilaya ya Nacala nchini Msumbiji, alijifunza kitu kimoja, inamchukua daktari mmoja muda mwingi kumtibu mtoto mmoja anayeharisha na kwa kuwa vifaa ni duni anaishia kufa. Lakini daktari huyo huyo akitoa elimu ya afya kwenye jamii, anazuia watoto wengi kupata magonjwa kama ya kuharisha.

Hivyo kama daktari atatumia muda mwingi kutoa elimu kuliko kutibu, atapunguza vifo. Lakini hilo huwa halionekani, kwa sababu vifo vichache vinavyotokea kwenye hospitali vinafanya watu waone ni tatizo kubwa, kumbe kuna wengi wanakufa kabla hata ya kufika hospitali.

 1. Jinsi ya kudhibiti silika ya ukubwa.

Kuepuka kuviona vitu kwa ukubwa ambao siyo halisi, unahitaji vitu viwili;

Moja; linganisha, unapopewa takwimu ya aina fulani, usiichukue yenyewe kama yenyewe, bali linganisha na takwimu nyingine inayoendana nayo. Na hapo utaona kama kweli kitu ni kikubwa au kidogo kama unavyofikiri.

Mbili; gawanya. Ukisema vifo vya ajali za pikipiki vimeongezeka mwaka huu kuliko mwaka jana, unaweza kuona upo sahihi. Lakini ukichukua vifo hivyo na ukagawa kwa idadi ya waendesha pikipiki, utagundua mwaka huu kuna waendesha pikipiki wengi kuliko mwaka jana, hivyo ongezeko linaloonekana kwenye idadi ya vifo, ukigawanya na idadi ya waendesha pikipiki utakuta idadi ya vifo kwa kila mwendesha pikipiki inapungua na siyo kuongezeka.

SOMA; Mitazamo Hii Mitano (05) Kuhusu Kipato Ndiyo Inakufanya Uingie Kwenye Matatizo Ya Kifedha, Ijue Na Hatua Za Kuchukua Ili Kuondoka Kwenye Umasikini.

ENEO LA SITA TUNALOKOSEA; SILIKA YA KUJUMUISHA.

Kwa kuwa hatuna uwezo wa kukutana na kila mtu na kujua kila kitu kuhusu kila mtu, huwa tuna tabia ya kuwaweka watu kwenye makundi na kuwajumuisha wote kuwa sawa, kitu ambacho kinatuzuia kuona uhalisia.

Makundi yaliyozoeleka kwenye kuwajumuisha watu ni hali ya kipato, uraia, rangi, dini, elimu na jinsia.

 1. Kuwa makini unaposema wengi.

Ni rahisi kutumia neno wengi, kwamba wengi wanafanya hivi au wengi wapo hivi. Lakini wengi inaweza kumaanisha chochote, asilimia 51 ni wengi na hata asilimia 99 ni wengi. Hivyo unaposema wengi wanafanya kitu fulani, au wengi wapo kwenye hali fulani, ni vyema kutumia namba halisi ili kuona uhalisia, kuliko kujumuisha kwenye wengi.

 1. Usifanye maamuzi kwa kutumia mfano mmoja kwenye kundi.

Kitu kimoja kinapokuwa na matatizo, basi huwa tuna tabia ya kuona vitu vyote ambavyo vinafanana na hicho vina matatizo pia. Ni sawa na gari moja kupata ajali kisha ukaona magari yote ni mabaya. Au mtu wa dini fulani kufanya jambo baya na ukaona watu wote wa dini hiyo ni wabaya. Ukweli ni kwamba, mtu mmoja au wachache kufanya kitu fulani haimaanishi kundi zima linafanya hivyo, fikiria kwa mifano zaidi na utaona kwamba kujumuisha watu au vitu kunakuzuia kuiona dunia kwa uhalisia wake.

 1. Jinsi ya kudhibiti silika ya kujumuisha.

Moja; angalia tofauti ndani ya kundi, usiangalie kundi zima kwa ujumla, gawa kwenye makundi madogo madogo kulingana na tofauti zilizopo.

Mbili; angalia ufanano baina ya makundi, wakati unasema kundi fulani lipo hivi, hebu angalia kama tabia unayoona kwenye kundi hilo haipo kwenye makundi mengine pia.

Angalia tofauti baina ya makundi, pia makundi tofauti yanakuwa na tofauti pia, kwa kuangalia hilo utaweza kuona kitu kimoja kikifanyika kwenye kundi moja ni sawa, ila kwenye kundi jingine siyo sawa.

ENEO LA SABA TUNALOKOSEA; SILIKA YA HATIMA.

Huwa tunapenda kuona kwamba kila kitu kina hatima yake, kwamba hakuna juhudi zinazoweza kubadili hatima ya kitu. Kwamba masikini wataendelea kuwa masikini kwa sababu ndiyo hatima yao, na matajiri wataendelea kuwa matajiri. Hii siyo sahihi, kwa sababu hakuna kisichobadilika.

 1. Afrika inapiga hatua.

Kwa kipindi kirefu Afrika imekuwa inaitwa bara la giza, bara ambalo haliwezi kuendelea na watu wake ni wajinga na masikini. Mataifa yaliyoendelea yalishakata tamaa na Afrika, wakiona hatima yake ni umasikini.

Lakini kidogo kidogo Afrika inapiga hatua. Idadi ya watu inaongezeka, wengi wanaondoka kwenye umasikini, wengi wanapata elimu na maendeleo na teknolojia inawafikia Waafrika wengi, kitu kinachowafanya kuweza kushindana na dunia na pia kuwa soko kubwa la vitu vingi.

Mataifa kama China yaliona hili haraka na kulitumia vizuri ndiyo maana bidhaa za china zina soko kubwa Afrika.

 1. Mambo yanabadilika, hata kama ni kidogo kidogo.

Ni rahisi kuona mambo yapo vile vile kwa sababu mabadiliko yanatokea kidogo sana. Lakini ukweli ni kwamba mambo yanabadilika, mambo hayapo kama yalivyokuwa mwanzo.

Chochote unachojua kuhusu dunia leo, miaka kumi ijayo kitakuwa siyo sahihi, hivyo uelewa uliokuwa nao kuhusu dunia miaka 10 iliyopita, sasa hivi siyo sahihi. Hivyo kila mara hakikisha unajifunza na kuona mambo yanavyokwenda.

 1. Jinsi ya kudhibiti silika ya hatima.

Kudhibiti silika ya hatima kumbuka kwamba mabadiliko madogo bado ni mabadiliko, hivyo;

Fuatilia kila mabadiliko yanayotokea, hata kama ni madogo.

Jifunze vitu vipya na teknolojia mpya zinazokuja.

Angalia ushahidi wa mabadiliko ya kiutamaduni, ambayo yanatokea kwenye kila utamaduni.

ENEO LA NANE TUNALOKOSEA; SILIKA YA MTAZAMO MMOJA.

Ni tabia yetu binadamu kupenda kutafuta njia rahisi ya kuelewa kitu, na hili linatupelekea kuwwa na mtazamo mmoja pekee kwenye kila kinachotokea. Tunapenda kuona kwamba matatizo yote yanasababishwa na kitu kimoja ambacho tukiweza kukishinda basi maisha yatakuwa rahisi. Huwa pia tunaona matatizo yote yana suluhisho moja, ambalo tukilifikia basi maisha yanakuwa bora kabisa. Mtazamo huu wa tatizo moja au suluhisho moja umekuwa unatuzuia kuona dunia kwa uhalisia.

 1. Kuwa tayari kujikosoa wewe mwenyewe.

Mara nyingi tunapokutana na tatizo au changamoto, huwa tuna kitu ambacho tunakihisi ndiyo kimesababisha au kuna kitu tunafikiria ndiyo kitatatua. Tukishaweka mawazo yetu hivyo, hatuwezi kujifunza tena njia mbadala za kusababisha au hata kutatua. Hivyo unahitaji kuwa tayari kujikosoa wewe mwenyewe, kujiambia kwamba unachofikiri siyo pekee na hivyo kufikiri zaidi, na kuona njia unayofikiri ni suluhisho siyo ili uweze kuona njia nyingine zaidi.

Unapokuwa tayari kujikosoa mwenyewe na ukajipa nafasi ya kujua kitu kwa undani zaidi, utaona ukweli wenyewe.

 1. Namba pekee hazitutoshi kuona ukweli wa dunia.

Tunapotaka kuielewa dunia, sehemu ya kwanza tunayoangalia ni namba, takwimu mbalimbali, kama za kipato, vifo, huduma za afya na kadhalika. Hatuwezi kuielewa dunia bila ya namba, lakini pia namba pekee hazitoshi kuona ukweli wa dunia.

Tunaweza kupima afya na magonjwa kwa namba, lakini dhumuni la mwisho ni watu kuwa na maisha bora na uhuru, kitu ambacho ni kigumu kupima kwa namba, ila kinachoweza kuonekana kwa macho.

 1. Hata demokrasia siyo suluhisho pekee.

Tumekuwa tunafikiri kwamba kama nchi ikiwa na demokrasia ya kweli basi maisha ya wananchi wake yanakuwa bora sana, lakini demokrasia pekee haitoshi, nchi nyingi ambazo zimeweza kupiga hatua kubwa kiuchumi ni nchi ambazo hazina demokrasia ya wazi. Hivyo demokrasia inaweza kuchangia maisha kuwa bora, lakini siyo jawabu pekee.

 1. Jinsi ya kudhibiti silika ya mtazamo mmoja.

Badala ya kuwa na nyundo na kila unachoona kikawa msumari, unahitaji kuwa na box la zana zote muhimu. Unahitaji kufikiria vitu vingi zaidi ya kukubali maelezo rahisi unayokutana nayo. Chochote unachofikiria ni sababu au suluhisho, kipime kwa vitu vingine vingi na utaona ukweli ulivyo na siyo kupofushwa na mtazamo mmoja.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Psychology Of Selling (Jinsi Ya Kuuza Zaidi, Kwa Urahisi Na Haraka Kuliko Unavyodhani.)

ENEO LA TISA TUNALOKOSEA; SILIKA YA LAWAMA.

Jambo lolote baya linapotokea, huwa tunatafuta mtu mmoja wa kumlaumu. Na jambo zuri linapotokea, huwa kuna watu wanapenda kuchukua sifa kwamba wao wamesababisha. Ukweli ni kwamba hakuna mtu au kitu kimoja kinachosababisha kitu kibaya kutokea au kitu kizuri kutokea. Kila kinachotokea, kuna michango ya watu wengi na vitu vingi.

 1. Mchezo wa kulaumu.

Huwa tunashiriki mchezo wa kulaumu, kwa kuangalia mtu wa kumnyooshea kidole ambaye anahusika na kile ambacho kimetokea. Lakini kwenye kila tunacholaumu, tunajionesha sisi zaidi kuliko hata wale tunaowalaumu. Tunapenda kuwaangalia wengine kama sababu, ili kudhibitisha imani ambazo sisi tunazo juu ya wengine. Hivyo unapolaumu, jua shida siyo yule unayemlaumu, bali wewe unayelaumu ndiye mwenye shida, hasa kama hujaelewa vizuri kile kilichotokea.

 1. Tunawapa watu nguvu wasizostahili.

Katika mchezo wa kulaumu, huwa tunawapa watu nguvu kubwa ambazo hawastahili. Huwa tunaona viongozi ndiyo waliosababisha kitu fulani, kizuri au kibaya kutokea. Lakini unapochunguza kwa undani, unagundua viongozi hao hawana hata uhusika mkubwa. Wakati mwingine mambo yanabadilika yenyewe, ambapo hata kama viongozi hao wasingekuwepo, bado yangebadilika.

Na kwa sehemu kubwa, mifumo inafanya kazi kubwa kuliko mtu yeyote mmoja. Kwenye nchi nyingi, raisi anaweza kuonekana ndiyo anafanya kazi, lakini mengi anayosifiwa nayo, yangeweza kutokea hata kama asingekuwa raisi. Kwa sababu ipo mifumo ambayo inahakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

 1. Jinsi ya kudhibiti silika ya lawama.

Kuondokana na silika ya lawama, acha kutafuta mbuzi wa kafara,

Kwenye jambo lolote linalotokea, usiangalie mtu mmoja au kitu kimoja kilichosababisha, bali angalia mwingiliano wa vitu ambao umesababisha kilichotokea kutokea.

Pia usiangalie shujaa mmoja, angalia mfumo. Vitu vingi vinatokea kwa sababu kuna mifumo imara na siyo kwa sababu ya maamuzi ya mtu mmoja.

ENEO LA KUMI TUNALOKOSEA; SILIKA YA UHARAKA.

Huwa tunadanganyika kwamba kuna fursa zinatupita iwapo hatutachukua haraka, katika kuharakisha huko tunachukua hatua ambazo siyo sahihi na hivyo kukosea.

 1. Siyo lazima ufanye kitu kila wakati.

Kunapokuwa na hatari fulani, huwa tunasukumwa kuchukua hatua yoyote, ili mradi tu tuonekane kuna kitu tunafanya. Sasa hatua nyingi tunazochukua pale tunapokabiliwa na hatari, huwa ni hatua ambazo zinakuwa na madhara makubwa baadaye.

Hivyo tunapokuwa kwenye hatari, kabla hatujakimbilia kuchukua hatua, kwa kuona tunachelewa, tunahitaji kuchukua muda na kutafakari matokeo ya hatua tunazochukua.

Mwandishi anatupa mfano wa ugonjwa ambao ulitokea kwenye wilaya aliyokuwa anatibu, wakati anaongea na mkuu wa wilaya akamuuliza kama ugonjwa huo ni wa kuambukizwa, akamwambia hapana, mkuu wa wilaya akamwambia wanahitaji kuchukua hatua fulani, vipi kama wakizuia watu wasitoke kwenye eneo hilo ili kuondoa hatari kama ikiwa ni wa kuambukizwa na haijajulikana, mwandishi akakubaliana na mkuu wa wilaya. Basi safari kwenye eneo hilo zikasitishwa, lakini watu walitaka kufika sokoni na kupata mahitaji yao, kwa kuwa njia zilifungwa, waliamua kutumia usafiri wa boti za wavuvi, ambazo hazikuwa salama, na zilizama na wengi kufa. Hatua za haraka zilizochukuliwa zilipelekea wengi kufa kwa ajali kuliko kufa kwa ugonjwa husika.

 1. Haimaanishi usiwe na hofu, bali epuka kelele.

Kuepuka kufanya maamuzi kwa haraka haimaanishi usiwe na hofu kabisa, wala haimaanishi uamini kila kitu kitakuwa sawa, bado unahitaji kuona hatari iliyopo, lakini unahitaji kuepuka kelele ambazo zinakusukuma kuchukua hatua zitakazoleta madhara zaidi. Tuliza mawazo yako, angalia uhalisia wa kinachotokea, tafakari matokeo ya hatua utakazochukua ndipo uchukue hatua. Usikimbilie kuchukua hatua kwa sababu unataka kuonekana unafanya kitu, italeta madhara makubwa kuliko hali yenyewe ingeachwa ilivyo.

 1. Kudhibiti silika ya uharaka.

Kujiepusha na silika ya kuchukua hatua za haraka, chukua hatua ndogo ndogo.

Pumua na jipe muda wa kutafakari, usione kwamba unahitaji kuchukua hatua haraka, jua kwanza nini kinaendelea.

Angalia data zinasemaje, kama kitu ni muhimu na haraka basi kinapaswa kupimwa, hivyo kuwa na takwimu sahihi zinavyoonesha hali ilivyo.

Pia epuka watu wanaotabiri kwamba mambo mabaya zaidi yatatokea, utabiri ni kama ulivyo, ni utabiri, hakuna mwenye uhakika, hivyo usifanye maamuzi ya haraka kwa utabiri.

Rafiki, hayo ni maeneo kumi ambayo tumekuwa tunakosea kuhusu dunia kila wakati na kutuzuia kuona maendeleo makubwa yanayotokea duniani. Tujifunze kuangalia uhalisia wa dunia mara zote, tukitafuta takwimu sahihi na pia kutembea na kuona kwa macho yetu. Pia tuwe na matumaini kwamba dunia inazidi kuwa sehemu salama ya kuishi na kila mmoja wetu atimize majukumu yake.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji