Mpendwa rafiki,

Kuna vitu ambavyo huwezi kwenda kununua dukani hata kama una fedha, siyo kwamba kusema hivyo ndiyo  namaanisha fedha siyo muhima hapana bali fedha itaendelea kuwa mfalme na muhimu kila siku katika maisha yetu. Hakuna maisha ya wito wowote ambao utachagua kuishi na usihitaji fedha, bali kila wito ili uweze kukua na kustawi vizuri unahitaji fedha.

Kwenye kila maisha ambayo tunaishi kuna kitu ambacho kinaweza kununua kila kitu, siyo maisha ya ndoa, useja nakadhalika. Ni kitu ambacho kinanunua kila kitu ambacho kimekosekana ndani ya nyumba. Ukiwa na kitu hiko basi ndoa yako itang’ara, wito wako ulichochagua utang’ara na mambo yako mengi yataenda siyo tu katika maisha ya ndoa bali pia hata katika jamii iliyokuzunguka.

Tatizo kubwa

Ndoa haihitaji kuwa na ubinafsi yaani kinachopatikana katika maisha ya ndoa yawe ni mafanikio basi yanakuwa ni mali ya ndoa. Inakuwa ni mali ya wote na hakuna kusema hiki ni changu na hiko ni chako ndiyo maana ya umoja huo katika ndoa.  Kukiwa na umoja, ubinafsi hautakuwa na nafasi na watu wataishi vizuri sana tena kwa kushirikiana.

SOMA;Jinsi Wanandoa Wanavyobomoa Ndoa Zao

Fedha inayonunua kila kitu katika maisha ya ndoa siyo kitu kingine au ni kigeni masikioni mwako bali ni upendo. Upendo tunaohubiriwa kila siku ndiyo unaweza kununua vitu katika ndoa kuliko hata fedha, ukiwa na upendo basi utaweza kununua heshima ndani ya ndoa yako. Kwani heshima ni kitu ambacho huwezi kwenda dukani kununua lakini ukiwa na upendo utaweza kukinunua.

Kama wanandoa wakinunua upendo basi watakuwa ndoa bora sana, upendo huvumilia kila kitu na wala haubagui lakini changamoto yetu sisi binadamu tunakuwa na upendo wa vipimo na siyo upendowa asili kwani kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo.

Upendo utanunua kila kitu maisha ya ndoa utanunua amani, furaha, ushirikiano, utii, heshima, nidhamu , maelewano, kusikilizana, kuvumiliana na mengine mengi yanayohusiana na hayo.

Hatua ya kuchukua leo, kama unataka ndoa yako inadumu na iwe bora jitahidi ndoa yako iwe na upendo. Upendo ndiyo fedha inayonunua kila kitu katika ndoa, ukikosa upendo unapoteza maana ya kuwa mwanadamu unakuwa umepoteza hadhi yako na utakuwa hadhi ya mnyama.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FACTFULNESS (Maeneo Kumi Tunayokosea Kuhusu Dunia Na Kwa Nini Mambo Ni Mazuri Kuliko Unavyofikiri).

Hivyo basi, ili kuepuka migogoro mingi na ya kila siku ni vema wana ndoa wakanunua upendo na kuufanya kuwa kama fedha katika ndoa yao. Tukiwa na upendo tutaheshimiana na kuvumiliana kwa kila kitu lakini kama hatuna upendo tutakuwa tunaona mzigo mkubwa kuishi maisha tuliyochagua na kuona ugumu hata wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !