Mambo mengi yapo katika mfumo wa biashara hivyo vitu vingi ni biashara katika dunia hii ya leo, siasa, dini, shule nk ni biashara kama biashara nyingine.
Asili ya ndoa ni upweke, kadiri ya maandiko siyo vema mtu huyu abaki peke yake. Kwa dhana hiyo tunaona kuwa neno siyo ndiyo limebeba ujumbe wa upweke. Ndiyo maana utawasikia watu wengine wakiambiana kuwa amechoka maisha ya upweke hivyo anataka kuwa na mwenza. Upweke ni tatizo katika ndoa nyingi na watu wengi siku hizi wanasahau hilo.
Hata hawa alishawishiwa na shetani kwa sababu ya upweke wa adamu, kutokuwepo tu kwa adamu alitumia kama njia ya kupata kile anachotaka na shetani alifanikiwa kumdanganya hivyo kwa zama hizi usipolinda hali ya kuziba upweke katika ndoa yako unajiandalia hatari yako. utawezaje kuziba upweke katika ndoa yako kama wewe mnakutana likizo kwa likizo? Hapo ndiyo unakua umeoa au kuolewa lakini unasaidiwa majukumu ya ndoa na watu wengine.
Kwa mfano, wewe ni mwandoa mke wako yuko kagera wilaya fulani na wewe uko arusha wilaya fulani je kwa namna hiyo hapo kuna kusudi la ndoa?
Hakuna kusudi la ndoa kwa sababu ile dhana ya kuziba pengo la upweke linakuwa halipo. Ndiyo maana unawakuta watu wanadondoka katika maisha ya uzinzi mara nyingi. Kusudi la ndoa siyo kukaa maisha ya mbali, bali ya karibu ili muweze kusaidiana. Watu wengine wameoa kama vile hawajaoa na wengine wameolewa kama vile hawajaolewa.
Ni ndoa za siku hizi ambazo watu wanakutana kwa mwaka mara moja tu wakati wa likizo. Tumekuwa na ndoa za Bluetooth nyingi ambazo zinaa matatizo mengi ya ndoa katika jamii yetu. Ndoa zinafungwa baada ya muda watu wanatengana kwa sababu wanakosa kuishi misingi ya ndoa.
SOMA; Kitu Chenye Nguvu Kubwa Katika Maisha Ya Ndoa
Kila kitu kina misingi yake hapa duniani na ukishindwa kuifuata lazima utaanguka katika mchezo huo. Fedha nayo ina misingi yake ukishindwa kuifuata lazima utaanguka vibaya kifedha. Unatakiwa kuheshimu misingi ya kitu unachofanya na kwenda kinyume na misingi ni adhabu.
Kumbuka kila mchezo una adhabu yake, hivyo ukishindwa kwenda sambamba na sheria zake lazima utapatiwa adhabu kama fundisho kwako. Dunia ina namna ya kumuadhibu mtu pale anaposhindwa kuishi maisha yake na kutimiza wajibu wake kiufasaha.
Kama uko katika maisha ya ndoa hebu jiulize tu, je hilo ndiyo kusudi la ndoa yako? hicho unachofanya ambacho siyo sahihi unafikiri ni salama kwako? Umechimba kisima chako mwenyewe halafu unahangaika na visima vya watu sasa ulichimba cha nini kisima chako? Kunywa maji ya kisima chako mwenyewe ndiyo salama acha visima vya watu hujui nani amepita.
Matatizo mengine ni ya kujitakia kabisa, mtu anajua anachofanya siyo sahihi lakini anafanya mambo yanapoenda hovyo ndiyo akili inarudi sasa. Kuwa na uaminifu katika ndoa yako, uadilifu, upendo ,furaha na amani. Jinsi unavyojilinda na hatari nyingine basi na wewe ilinde ndoa yako vivyo hivyo.
Kwanini ndoa ni biashara?
Ndoa ni biashara kwa sababu iko katika mfumo wa biashara na katika biashara kuna mteja hivyo na wateja wa ndoa yako ni mke na mume. Kama wewe ni mume basi mke wako ndiyo mteja wako namba moja na kama wewe ni mke basi mume wako ndiyo mteja namba moja. Uko katika biashara hivyo unatakiwa kumjali mteja vizuri na kumpatia huduma nzuri anazostahili kupatiwa mteja anapokuja katika biashara yako.
Shida inaanzia pale wawili hao wanaposhindwa kuhudumiana. Mume au mke wanashindwa kuhudumiana vizuri. Kama unavyojua mambo ya mteja, usipomhudumia vizuri hawezi kuendelea kung’ang’ania kwako wakati kuna huduma bora ambayo anaweza kuipata sehemu nyingine. Mteja anataka kupata kile anachotaka hivyo sasa akiingia katika ndoa ambayo hapati kile anachotaka hakika hawezi kuendelea kukaa katika ndoa hiyo kwa muda mrefu.
SOMA; Fedha Inayonunua Kila Kitu Katika Maisha Ya Ndoa
Kumbuka hatujaumbwa kuja kuvumilia maisha ya ndoa bali, kufurahia. Hujaumbwa maisha yako yote kuingia katika mahusiano ili kuteseka bali kufurahia, sasa utafurahia wapi raha ya ndoa? Ukiwa umekufa au? Maisha ni sasa, ishi vile unavyopenda na ishi kusudi uliloitwa.
Mwenza wako ndiyo mfalme wa ndoa yenu. Yeye ndiyo mteja mkuu hivyo mfanye awe mteja wako wa kudumu na hakikisha unamlea vizuri kiasi kwamba hatopatwa na hisia za kujaribu kufikiria sehemu nyingine ila wewe tu.
Hatua ya kuchukua leo; mfanye mwenza wako awe wako tu, huyo ndiyo mteja wako mpatie huduma bora ili azidi kubaki na wewe. Usipomjali atakwenda kwa watu wanaojua kujali na kuhudumia vizuri.
Kwahiyo, dhana ya kumpatie mteja kile anachotaka itumike sahihi. Siyo mke au mume wako anataka kitu ambacho siyo sahihi na wewe unampatia kwa sababu ni mteja wako unaogopa asije kwenda kwa mwingine. Simamia misingi ya ukweli na siyo vinginevyo.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na mwalimu wako,
Deogratius Kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net
Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti hii hapa www.mtaalamu.net/kessydeo .
Asante sana na karibu sana!