Kila mtu kuna mambo mengi ambayo anajifunza kwenye maisha ambayo anaishi. Mambo hayo anaweza kujifunza kutokana na maisha anayopitia, kutoka kwa wengine na hata kwa njia za kusoma.

Kila mzazi kuna mambo mengi ambayo anakuwa amejifunza kwenye maisha yake, ambayo kama akikaa chini ni kuwaandalia watoto wake yale aliyojifunza, atawasaidia sana kwenye maisha yao.

Lakini wazazi wengi tumekuwa hatufanyi hivi, tunayapoteza yale ambayo tumejifunza na kuwaacha watoto wetu warudie makosa yale yale ambayo sisi wenyewe tuliyafanya.

Mwekezaji Jim Rogers aliona umuhimu wa kuwapa mabinti zake wawili masomo ambayo amejifunza kwenye maisha na uwekezaji, na hapa ndipo alipoandika kitabu A GIFT TO MY CHILDREN. Kwenye kitabu hichi Jim amezungumzia mengi kuhusu maisha kwa ujumla na uwekezaji.

Somo kubwa sana kwenye kitabu hichi ni kujijua wewe mwenyewe kwanza na kuishi maisha ambayo ni halisi kwako badala ya kuishi maisha ya kuigiza.

Japokuwa Jim aliandika kitabu hichi kwa watoto wake, bado ni somo kubwa ambalo kila mtu anaweza kujifunza na kutumia kwenye maisha yake na yakawa bora sana.

Karibuni tujifunze kuhusu maisha na uwekezaji kupitia uzoefu wa Jim Rogers kwenye kitabu chake cha A GIFT TO MY CHILDREN.

gift to my childern

KIMBIA MBIO ZAKO MWENYEWE, USIKUBALI WENGINE WAKUSAIDIE KUFIKIRIA.

Maisha ni magumu kwa sababu watu wengi wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya. Watu wamekuwa wanafanya mambo ambayo hata hayana maana kwao kwa sababu tu kila mtu anafanya. Hii ni njia rahisi sana ya kushindwa kwenye maisha. Hapa Jim anatufundisha yafuatayo;

 1. Tegemea akili yako mwenyewe.

Unapofikia wakati wa kufanya maamuzi magumu na muhimu kwenye maisha yako, basi tegemea zaidi akili yako. Wapo watu watakaokupa ushauri wa kila aina, hata kama hujawaomba, lakini mwisho wa siku jua maamuzi unayofanya wewe ndiye utakayeyaishi, hivyo fikiri kwa kina kabla hujafanya maamuzi yoyote. Fanya maamuzi ambayo yatakuwa bora kwako sasa na siku za baadaye, na utaweza kubeba jukumu la matokeo utakayoyapata.

 1. Kama mtu akicheka wazo lako, ni kiashiria kwamba ni wazo bora.

Kama una wazo la kitu kikubwa ambacho ukikifanya kitafanya maisha yako kuwa bora, lakini watu wakakucheka, wakakuambia huwezi au haiwezekani, hivyo ni kiashiria kwamba ni wazo bora. Hivyo hakikisha unalitekeleza licha ya wengine kushindwa kuona ubora wake.

 1. Kuwa wewe, kuwa halisi.

Huwezi kufanikiwa kwenye maisha yako kama utajaribu kuiga maisha ya wengine, wewe ni wa pekee na wa tofauti kabisa, utafanikiwa kama utajijua na kuishi kulingana na uimara ulionao. Usikazane kuwa kama wengine, jijue na ishi maisha ya uhalisia wako.

 1. Kuwa na maadili ya hali ya juu.

Kwenye maisha utakutana na vishawishi mbalimbali vya kupitia njia ya mkato, vya kupata zaidi ya wengine, vya kuvuna kabla ya kupanda, epuka vishawishi hivi kwa sababu ni mtego unaowazuia wengi kufanikiwa. Kuwa na maadili ya hali ya juu, kuwa mwaminifu, kuwa mwadilifu, fanya yale ambayo ni sahihi, fuata taratibu na sheria za kila unapokuwepo.

 1. Weka akiba.

Kwenye maisha utakutana na watu ambao wanatumia kila fedha wanayopata halafu wanakopa ili kuendelea kutumia zaidi. Watakushawishi uwe na matumizi makubwa, ununue vitu ambavyo hutaki ili tu uonekane na wewe upo. Epuka watu wa aina hiyo, epuka maisha ya aina hiyo. Katika kila kipato unachoingiza, lazima sehemu ya kipato hicho iwe akiba.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Winning The Loser’s Game (Mbinu Zisizopitwa Na Wakati Za Kufanikiwa Kwenye Uwekezaji).

KAZANA NA KILE UNACHOTAKA.

Kwenye maisha, tunapata kile ambacho tunapigania, kile ambacho tunaweka mawazo na nguvu zetu muda mwingi. Hivyo kuishi maisha unayotaka, kazana na yale unayotaka na mengine achana nayo.

 1. Jitoe kwa kile unachopenda kwenye maisha.

Je mtu anawezaje kufanikiwa kwenye maisha? Jibu ni rahisi, kujaribu mambo mengi mapema, kujua yale ambayo anayapenda kweli, kisha kuweka nguvu zake zote kwenye yale anayopenda kufanya. Chochote unachopenda kweli, kisha ukaweka maisha yako yote kwenye hicho unachopenda, lazima utafanikiwa, hata kama hutakuwa na fedha nyingi, angalau utakuwa na maisha yenye kuridhika.

 1. Watu wanaopenda wanachofanya, hawafanyi kazi.

Huwezi kufanikiwa kwenye maisha kama unafanya kazi, kwa sababu kazi inachosha, kazi ni mzigo na kila mtu anapenda kukimbia kazi. Utafanikiwa kama unafanya unachopenda kufanya, na hapo inakuwa tena siyo kazi, bali inakuwa maisha yako. Huwezi kuchoka kufanya, kwa sababu ndiyo maisha yako yanategemea hicho. Wakati wengine wanafurahia mapumziko, wewe hujui hata kama kuna mapumziko.

TABIA NZURI ZA MAISHA NA UWEKEZAJI.

Zipo tabia ndogo ndogo ambazo zinawatofautisha wale wanaofanikiwa na wale wanaoshindwa kwenye maisha. Hapa kuna baadhi ya tabia hizo, zijue na kuziishi kila siku na kwa hakika utafanikiwa.

 1. Kuwa mtu wa kujituma.

Usisubiri mpaka uambiwe nini cha kufanya, angalia kipi hakipo sawa kisha kifanyie kazi kuhakikisha kinakuwa sawa. Kuwa mtu wa kujituma, kuwa mtu wa kutatua matatizo na changamoto na mara zote utakuwa na kazi nyingi za kufanya. Jim anatuambia baba yake alimpa kauli moja muhimu sana kuhusu kazi, popote ulipo, kuna kitu unachoweza kufanya. Hata kama hakuna kazi ya kufanya, fanya hata usafi.

 1. Kuwa makini kwenye kila unachofanya.

Chochote unachojihusisha nacho kwenye maisha, kijue kwa undani, kijua kwa umakini wa hali ya juu sana. Usifanye kitu chochote kwa mazoea, usifanye chochote kwa sababu wengine wanafanya, au kwa sababu kila mtu anafanya. Wewe kaa chini na jifunze na fanya kile unachojua, bila ya kujali wengine wanafanya nini. Hili litakutenganisha na wengi wanaoshindwa kwa kufanya kwa mazoea.

 1. Kwenye uwekezaji, jua kila kitu kabla ya kuwekeza.

Popote unapotaka kuwekeza fedha yako, hakikisha unafanya kazi moja kubwa ya kujua kila kitu kinachohusiana na pale unapowekeza. Usiwekeze kwa sababu watu wanasema ni uwekezaji mzuri, usiwekeze kwa sababu kila mtu anawekeza, bali jipe muda wa kujifunza kwa undani kuhusu uwekezaji wowote unaotaka kufanya.

Katika kitu ambacho unapaswa kuogopa kama ukoma kwenye uwekezaji, ni maoni ya wataalamu wa uwekezaji, usiwekeze kwa sababu kuna wataalamu wamesema ni uwekezaji mzuri, bali wekeza kwa sababu unajua kwa hakika, zaidi hata ya hao wataalamu. Ni fedha zako unawekeza, ni wajibu wako kuzilinda, hakuna atakayefanya hilo kwa ajili yako.

 1. Ishi maisha yenye ndoto kubwa.

Kama huna kitu kinachokusukuma kuamka asubuhi kitandani, utaenda na maisha kwa mazoea na hakuna makubwa utakayoweza kukamilisha. Unahitaji kuwa na ndoto kubwa kwenye maisha yako, na ndoto hizi zinaweza kubadilika kwa kila kipindi cha maisha yako. Kwa mfano wakati ukiwa shuleni inaweza kuwa kufaulu vizuri na kufika viwango vya juu, unapokuwa kazini inaweza kuwa kutoa huduma bora na kuwafikia wengi. Hakikisha kila wakati, ipo ndoto kubwa unayofanyia kazi kwenye maisha yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; When Breath Becomes Air (Safari Ya Mtu Mmoja Katika Kujua Maana Ya Maisha Na Kifo).

VITU VINAVYOONEKANA VYA KAWAIDA SIYO VYA KAWAIDA KIHIVYO.

Kuna vitu kwenye maisha huwa vinaonekana ni vya kawaida, kwamba kila mtu anajua na ndivyo inavyopaswa kuwa, unapochunguza vizuri kwa ndani, unagundua siyo vya kawaida kama wengi wanavyofikiri.

 1. Vitu vingi ambavyo watu wamezoea kufanya siyo sahihi.

Ni rahisi kukubali kufanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya, na kuona kwa kuwa wengi wanafanya basi ni sahihi. Ukweli ni kwamba, vitu vingi ambavyo watu wanaamini na kufanya siyo sahihi. Wewe chukua muda na anza kuchunguza kila kitu, utaona kwa namna gani vitu vingi siyo sahihi. Usiendeshwe na mazoea, badala yake dadisi na hoji kila kitu kupata ukweli.

 1. Vyombo vya habari huendesha propaganda na siyo ukweli.

Kama unaamini kila unachoona au kusikia au kusoma kwenye vyombo vya habari kwamba ndiyo ukweli, unaishi maisha ya kujidanganya sana. Sehemu kubwa ya habari na taarifa unazopata kupitia vyombo vya habari siyo sahihi, bali ni habari zilizotengenezwa kwa njia ambayo zitawavutia watu na vyombo hivyo viendelee na biashara. Kila habari unayoipata, kuwa na mashaka nayo na chunguza kwa makini, utagundua ukweli ni tofauti kabisa na habari ilivyokuwa.

 1. Taarifa nyingi zimekuwa kelele.

Kwenye karne ya 21, zama za taarifa, taarifa nyingi zimekuwa ni kelele. Tumekuwa na taarifa nyingi kuliko tunavyoweza kuzitumia, na sehemu kubwa ya taarifa hizi siyo sahihi. Kupata ukweli kwenye zama hizi unahitaji kuwa makini sana.

KWA NINI SIYO TAJIRI

ELIMU MUHIMU YA DUNIA INAYOPASWA KUWA NAYO.

Moja ya vitu unavyopaswa kujua kuhusu maisha ni kwamba, hakuna mwisho wa kujifunza, kila siku ni darasa na elimu haina mwisho. Yapo mengi sana unapaswa kufahamu kuhusu maisha na dunia kwa ujumla, yafuatayo ni muhimu kila mtu kujua kama ambavyo Jim ametushirikisha.

 1. Tembea kuiona dunia, usitegemee vitabu pekee.

Unaweza kujifunza mengi kwenye kusoma vitabu, lakini kuujua ukweli, tembelea maeneo mbalimbali. Safiri dunia na kaa na watu tofauti tofauti kwenye tamaduni tofauti. Utajifunza mengi ambayo hayaandikwi kwenye habari wala vitabu. Utajifunza kwamba watu ni wale wale na tabia za watu hazitofautiani licha ya kuwa na tofauti ya rangi, dini na hata tamaduni.

 1. Kuwa na mawazo chanya na kuwa raia wa dunia.

Usikazane kushikilia utamaduni wako na kuona wa wengine haufai. Kuwa tayari kujifunza kupitia wengine, hata kama wanaamini kinyume na unavyoamini wewe. Jua kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mtu, na kuwa raia wa dunia nzima, unayeweza kuchangamana na kila aina ya utamaduni, utajifunza mengi kuhusu watu na maisha.

 1. Jifunze falsafa, jifunze jinsi ya kufikiri.

Watu wengi wanaposikia falsafa basi hufikiri ni mpaka uwe mtu mwenye akili sana, unayekaa na kuwaza maswali magumu kuhusu maisha na dunia kwa ujumla. Ukweli ni kwamba, falsafa ni msingi ambao mtu unaishi, na unapokuwa na msingi, unaweza kufanya maamuzi kwa kufikiri badala ya mazoea. Hivyo chagua falsafa utakayoiishi na hiyo ndiyo itakuongoza kufanya maamuzi.

 1. Jifunze historia.

Kila kitu kinachotokea duniani kwa sasa, ni marudio ya yale ambayo yamewahi kutokea huko nyuma. Hakuna kitu ambacho ni kipya kabisa, bali mambo yale yale yanatokea kwa njia ambazo ni tofauti. Ukijifunza historia, utaona kwa nini mambo yanatokea na pia utaweza kujua hatua sahihi za kuchukua kabla hata mambo hayajatokea. Mfano kwenye uwekezaji, kila mara ambapo bei ya vitu inapanda, watu huvithamini zaidi na hivyo kuendelea kupanda, hili linasukuma uzalishaji wa vitu hivyo kuwa mkubwa na mwishowe uzalishaji unakuwa mkubwa kuliko uhitaji na bei inaanza kuporomoka. Ndiyo imekuwa inatokea kwenye dunia miaka nenda miaka rudi, lakini watu hawajifunzi.

 1. Jifunze lugha tofauti, na kichina kiwe moja ya lugha hizo.

Ili kuweza kujifunza kuhusu tamaduni za wengine, unahitaji kujifunza lugha tofauti na zile ambazo ni za asili kwako. Hakikisha unajifunza lugha ambazo zinaongelewa na watu wengi duniani, na hilo litakuwezesha kuweza kushirikiana na wengi zaidi.

Hakikisha unajifunza lugha ya Kiingereza na lugha ya Kichina, China ni taifa linalokua kwa kasi na baadaye litakuwa taifa namba moja kiuchumi duniani. Kujua lugha ya kichina, kutakuwezesha kuziona na kuzitumia fursa zinazopatikana kwenye taifa hili.

 1. Hii ni karne ya China.

Kila karne, kumekuwa na taifa ambalo linakuwa na nguvu kubwa kiuchumi na linaendesha dunia nzima. Karne ya kumi na tano ilikuwa ya Dola ya Roma, karne ya 16 ikawa ya Uhispania, karne ya 17 na 18 ikawa ya Ufaransa, karne ya 19 ikawa ya Uingereza, karne ya 20 ya Marekani, na sasa karne ya 21 ni ya China.

China ni taifa kubwa kiuchumi kwa sasa, ni taifa lenye watu wengi, na ni taifa lenye utamaduni ambao unawawezesha wengi kufanikiwa. Mfano wananchi wengi siyo watumiaji wakubwa na utamaduni wa kuweka akiba ni mzuri, kujitoa kwenye kazi ni kwa kiasi kikubwa. Hakikisha katika mipango yako ya uwekezaji, unaifikiria china kwa umakini mkubwa, ndiyo kiongozi wa dunia kwa karne hii ya 21.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Raising Positive Kids In A Negative World (Jinsi Ya Kulea Watoto Wenye Mtazamo Chanya Kwenye Dunia Hasi).

SIRI KUU YA UWEKEZAJI; JIJUE WEWE MWENYEWE.

Huwezi kufanikiwa kwenye uwekezaji kama hujijui wewe mwenyewe. Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kufanikiwa kwenye uwekezaji ni kujijua, kujua madhaifu yako, kujua uimara wako, kujua kipi kinakupa hofu na wasiwasi na kipi kinakupa amani ya moyo.

 1. Nini kinakusukuma wewe?

Ukisimama mbele ya kioo na kujiangalia, unaona nini ndani yako? Nini kinachokusukuma kufanya chochote unachotaka kufanya? Ni maeneo gani ambayo uko vizuri? Maeneo gani ambayo una udhaifu? Lazima ujijue vizuri ili kila hatua unayochukua iwe hatua sahihi kwako.

 1. Lengo siyo kuepuka makosa, bali kujifunza.

Kila mtu anakosea na utakosea mara nyingi kwenye maisha yako, lengo siyo kuepuka kukosea, bali kuhakikisha unajifunza kwenye kila kosa unalofanya ili usirudie tena kosa la aina hiyo. kuwa tayari kukubali pale unapokosea ili kuweza kujifunza na kuchukua hatua.

 1. Usihamaki, jifunze saikolojia.

Kwenye uwekezaji, watu ambao huwa wanapata hasara ni wale wanaohamaki na kuchukua hatua haraka. Kwa mfano, kama hisa fulani zinapanda bei, basi wengi hukimbilia kuzinunua wakiona ni fursa, hilo linafanya zipande bei zaidi, na hivyo kununua kwa bei juu zaidi. Hisa hizo zinapoanza kushuka bei, watu huhamaki na kuanza kuuza wakiona wanapata hasara, kadiri wengi wanavyokimbilia kuuza, bei inashuka zaidi. Hivyo kinachotokea, mtu ananunua hisa kwa bei ya juu na kuuza kwa bei ya chini. Haihitaji shahada ya biashara kujua kwamba ukinunua kitu kwa bei ya juu na ukakiuza kwa bei ya chini ni hasara.

Unahitaji kujifunza saikolojia ili kuweza kufikiri kwa umakini na siyo kuendeshwa kwa hisia na kufanya maamuzi ambayo ni hasara kwako.

TAMBUA MABADILIKO NA YAPOKEE HARAKA.

Kila kitu kwenye maisha kinabadilika, lakini watu huwa hatupendi mabadiliko. Hii ni kwa sababu mabadiliko hayana uhakika na watu wanapenda mazoea. Lakini kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, lazima uwe tayari kutambua mabadiliko na kuyapokea haraka kabla hata wengine hawajayaona.

 1. Kujua kitakachotokea kesho, angalia kilichotokea jana na kinachotokea leo.

Watu wanapenda mambo yaendelee kama yalivyo, kila kitu kiendelee kama ambavyo kimezoeleka. Lakini unapoangalia nyuma, unaona kuna vitu vilikuwa vizuri siku za nyuma ila kwa sasa siyo vizuri tena. Na hata ukiangalia sasa, utaona vyenye thamani sasa huko nyuma havikuwepo. Hii inakufanya uone kwamba unakokwenda, mengi yenye thamani sasa, hayatakuwa na thamani kabisa.

 1. Dunia itapitia mabadiliko makubwa siku zijazo.

Dunia tunayoishi sasa, siyo dunia itakavyokuwa miaka 100 ijayo. Kwa mfano kwa sasa kuna harakati kubwa za kupinga utawala wa mabavu na hata mamlaka ya eneo kubwa. Nchi nyingi zitagawanyika na kutengeneza mataifa madogo madogo na hakutakuwa na kitu kimoja kikubwa kinachoendesha dunia nzima, bali kila jamii itakuwa na vitu vyake.

Hili lilianza na kuvunjika kwa umoja wa kisovieti na unaendelea kuonekana kwenye maeneo yenye migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tunakoelekea, jamii ndogo ndogo zitakuw ana nguvu kuliko taifa zima kwa ujumla. Nchi ambazo ni kubwa kama Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, zitagawanyika kwenye mataifa madogo ya jamii zinazoendana badala ya taifa kubwa la jamii zinazovutana.

 1. Usijisumbue na vitu vinavyopotea.

Angalia mbele, angalia kesho, usikazane na vitu vilivyopita, mabadiliko yakishaanza, huwa hayarudi nyuma. Usisikitike kwamba siku za nyuma zilikuwa nzuri, badala yake angalia unatumiaje siku zinazokuja.

 1. Angalia kile ambacho wengi wanapuuza.

Mafanikio yapo kwenye yale mambo ambayo wengi wanapuuza, hivyo kama unataka kufanikiwa, usifuate kundi, badala yake angalia watu wanapuuza nini kisha ona kama kuna thamani ndani yake na chukua hatua.

 1. Kadiri kitu kinavyokuwa cha uhakika, ndivyo faida inavyokuwa ndogo.

Kwenye uwekezaji na hata maisha, vitu vyenye uhakika vina faida ndogo sana, kwa sababu havina hatari na hivyo kila mtu anaweza kufanya. Faida kubwa ipo kwenye vitu visivyo na uhakika, vitu ambavyo ni hatari, ambavyo wengi wanaogopa kufanya, hivyo wachache wanaofanya, wananufaika sana.

BAHATI INAWAENDELEA WALE WANAOWEKA JUHUDI.

Kuna watu ambao wanawaangalia wale waliofanikiwa na kusema watu hao wana bahati kweli. Labda ni kitu fulani kimetokea kwao, ambacho hakijatokea kwa wengine. Ukweli ni kwamba kile ambacho kinaitwa bahati, ni maandalizi makubwa ambayo yamekutana na fursa. Hivyo kuvutia bahati kwako, weka juhudi, jiandae vya kutosha.

 1. Timiza wajibu wako, la sivyo utapata hasara.

Chochote unachofanya, hakikisha unakijua kwa undani, la sivyo utapata hasara. Kadiri unavyojua kile unachofanya, ndivyo unavyojipa nafasi ya kukutana na bahati. Kwa kujua kwako na kuweka juhudi, utakutana na nafasi ambazo wengine hawawezi kuzitumia kwa sababu hawana maandalizi, na hiyo ndiyo itakuwa bahati kwako.

 1. Usisimame pale unapofanyia kazi ndoto za maisha yako.

Unapochagua ndoto kubwa ya maisha yako, na kuanza kuifanyia kazi, usikubali kitu chochote au mtu yeyote akusimamishe. Hata kama mambo yanakuwa magumu kiasi gani, hata kama kila mtu anakupinga na kukukatisha tamaa, kamwe usirudi nyuma, usifikirie hata kuacha, wewe endelea kusonga mbele na utakutana na fursa nzuri, ambayo wengine wataita ni bahati, kumbe uvumilivu wako ndiyo umetengeneza bahati hiyo.

Kila siku ya maisha yako ni siku ya kujifunza, tumia vizuri kila fursa unayokutana nayo, tumia vizuri yale unayoona kwa wengine na hakikisha kila siku unaishi maisha yako, unafanyia kazi ndoto yako kwa juhudi kubwa. Kwa njia hiyo, mafanikio yatakuja kwako, bila ya ugumu wowote.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji