Mauzo ni kitu muhimu sana kwenye maisha ya kila mtu, hii ni kwa sababu kila mtu kuna kitu anauza. Iwe ni kwenye biashara, kazi au maisha ya kawaida, kuna kitu ambacho mtu unataka wengine wafanye, hayo ndiyo mauzo.

Sehemu kubwa ya maisha ni sisi wenyewe kuuza mwonekano wetu na hoja au sera zetu, hili ndiyo zoezi la kujiuza. Ili watu waweze kukubaliana na wewe kwenye kile unachouza, unahitaji kuwa na mbinu bora kabisa za mauzo.

Napoleon Hill, aliyekuwa mwandishi wa kitabu maarufu cha falsafa ya mafanikio, THINK AND GROW RICH, alikuwa pia akifundisha kuhusu mbinu za mauzo. Kwenye kitabu SELLING YOU, mhariri amechambua kazi za Napoleon na kutushirikisha yake maarifa yanayohusiana na kuuza, hasa kujiuza binafsi na kuuza huduma ambazo mtu unatoa.

SOMA; selling you

Kwa kuwa mauzo ni sehemu ya maisha, na kwa kuwa kila wakati wa maisha yako kuna kitu utakuwa unauza, unapaswa kujifunza na kuwa na mbinu bora za mauzo. Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, uweze kuifunza mbinu hizi, uzifanyie kazi na uwe bora sana.

MOJA; KILA MTU ANAUZA.

Kila mtu anauza kila wakati, haijalishi wewe ni nani, kila unapokutana na mtu mwingine, unapoelezea wazo lako, unapotoa maoni yako, unauza kitu muhimu sana, ambacho ni wewe mwenyewe. Kama unatafuta kazi unajiuza wewe ili uajiriwe, na unahitaji kuendelea kujiuza kila siku ili kazi yako iendelee.

 1. Sifa kuu tano za muuzaji mzuri.

Ili uweze kufanikiwa kwenye maisha lazima uwe muuzaji mzuri, kwa sababu kila mtu anauza. Zifuatazo ni sifa kuu tano za muuzaji mzuri, unapaswa kujijengea sifa hizi ili kufanikiwa;

Moja; uthubutu, lazima uwe tayari kuuza hata kwenye mazingira ya ushindani mkali.

Mbili; kujenga taswira ya mafanikio, kabla hujamuuzia mtu kitu, lazima ujenge taswira ya mafanikio katika mauzo yako, lazima uwe tayari umeshamwona mteja akinunua kwenye akili yako, hilo linakufanya uwe na uthubutu zaidi.

Tatu; kuongea kwa kujiamini. Jinsi unavyoongea na sauti unayotumia inapaswa kuwa ya kujiamini na ya kushawishi. Sauti dhaifu inaonesha kutokujiamini na haitamshawishi mtu.

Nne; afya imara. Mwonekano wa nje una athari kubwa sana kwenye mauzo. Mtu mwenye afya imara na mwonekano mzuri anawavutia watu kununua zaidi.

Tano; kufanya kazi kwa bidii, hichi ndiyo kitu pekee kitakachobadili mafunzo ya mauzo kuwa fedha. Bila ya kuweka juhudi, hakuna chochote kinachoweza kukamilisha mauzo.

 1. Tabia mbili ambazo kila muuzaji anapaswa kuondokana nazo.

Zipo tabia ambazo zinawazuia watu wasiwe wauzaji wazuri, unapaswa kuondokana na tabia hizi ili kufanikiwa kwenye mauzo;

Moja; tabia ya kuahirisha mambo, unahitaji kuwa mtu wa kuchukua hatua kama ulivyopanga na kamwe usiahirishe ulichopanga kufanya.

Mbili; hofu. Hofu ni tabia inayomzuia mtu kuchukua hatua. Zipo aina sita za hofu ambazo ni mbaya sana, hofu ya umasikini, kukosolewa, magonjwa, kupoteza unayempenda, uzee na hofu ya kifo ni kizuizi cha wengi kufanikiwa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; A Gift To My Children (Zawadi Ya Baba Kwa Watoto Wake, Masomo Ya Maisha Na Uwekezaji).

MBILI; WATU WANANUNUA UTU/HAIBA.

Kitu cha kwanza kuwavutia watu kuja kununua unachouza, siyo kile unachouza, bali wewe mwenyewe. Watu wananunua kwa wale watu ambao wana haiba nzuri, zinazowavutia na kwendana nao. Hivyo kabla hujafikiria chochote kuhusu mauzo, unahitaji kutengeneza haiba ambayo inawavutia watu na kuwafanya wakubaliane na wewe.

 1. Jukumu kuu la maisha yako.

Jukumu kuu la maisha yako ni kufanikiwa, kupata kile ambacho unakitaka hasa, bila ya kuingilia haki za wengine. Ili uweze kufanikiwa lazima uwe na haiba ambayo inawavutia na kuwafanya wengine wakubaliane na wewe na kuondoa misuguano au wivu.

Ili kuweza kuuza vizuri, unahitaji kuwa mtu wa thamani kwa wengine, kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine.

 1. Madhaifu sita kwenye mauzo.

Wale wanaoshindwa kufanya mauzo makubwa, huwa wanakuwa na madhaifu haya sita;

Moja; kushindwa kujua msukumo wa mteja kununua.

Mbili; kukosa ung’ang’anizi kwenye mchakato wa mauzo.

Tatu; kushindwa kumjua vizuri mteja na kujua kama ana uwezo wa kununua.

Nne; kushindwa kubadili mtazamo wa mteja kutoka mtazamo hasi mpaka mtazamo wa kawaida.

Tano; kushindwa kutengeneza taswira ya mafanikio.

Sita; kukosa hamasa kwenye kile ambacho mtu anauza.

TATU; KUJITENGENEZEA MAONI KWENYE FIKRA ZAKO.

Yapo maoni ambayo tunayapata kutoka kwa wengine, yapo maoni ambayo tunajipa sisi wenyewe na yapo maoni ambayo yanajitengeneza kwenye fikra zetu. Haya maoni yanayojitengeneza kwenye fikra zetu, yana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yetu kimaisha.

 1. Kujitengenezea maoni ni hamasa binafsi.

Vile unavyofikiri upo na kile unachojiambia kila mara ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako. unapojitengenezea maoni mazuri ya mafanikio, ndivyo unavyohamasika kufanikiwa zaidi kwenye mauzo na kwenye maisha yako kwa ujumla.

 1. Tumia hisia chanya kuwauzia wengine.

Watu wananunua kwa hisia na siyo kwa kufikiria, hivyo kama unataka watu wanunue, unahitaji kutumia hisia chanya zinazowasukuma kuchukua hatua. Zipo hisia chanya saba muhimu unazoweza kutumia kwenye mauzo. Hisia hizo ni hisia za mapenzi, upendo, matumaini, imani, hamasa, chanya na hisia za uaminifu.

 1. Hisia hasi saba za kuepuka kwenye mauzo.

Kama hisia chanya zinawasukuma watu kununua, hisia hasi zinawazuia watu kununua. Hivyo kama muuzaji unahitaji kuzijua hisia hasi za kuepuka kwenye mauzo yako.

Hizi hapa ni hisia saba unazopaswa kuziepuka; hasira, hofu, tamaa, wivu, kisasi, chuki, ushirikina.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutafiti, Kuandika Na Kuuza Kitabu Bora Kabisa Ndani Ya Mwaka Mmoja. (Hatua Sita Muhimu Kwa Kila Anayetaka Kuandika Kitabu Kuzijua).

NNE; KUWA NA KUSUDI KUU.

Ili ufanikiwe kwenye jambo lolote unalofanya, unahitaji kuwa na kusudi kuu ambalo unalifanyia kazi. Kusudi hili ndiyo linakusukuma uweze kufanya makubwa zaidi. Kwenye mauzo pia unahitaji kuwa na kusudi kubwa linalokusukuma.

 1. Usitawanye nguvu zako.

Wanasema mshika mawili moja humponyoka, sasa huenda moja lisikuponyoke, lakini ukashindwa kuyashika hayo mawili vizuri. Unapotaka kufanikiwa kwenye maisha na kwa kile unachouza, unahitaji kujua kile kikubwa hasa unachotaka, kisha kuweka nguvu zako zote kwenye kukipata. Usikubali mambo yasiyo muhimu yaingilie lile kusudi kuu unalofanyia kazi.

 1. Ung’ang’anizi ni muhimu.

Kuwa na kusudi kubwa unalofanyia kazi haimaanishi unalifikia moja kwa moja. Utakutana na changamoto mbalimbali ambazo zitajaribu kukurudisha nyuma. Ung’ang’anizi ni muhimu sana kama unataka kufikia kusudi kubwa ulilonalo. Kabla hujafanikiwa utashindwa mara nyingi. Kabla hujakutana na atakayenunua utakutana na wengi watakaokataa kununua. Usipokuwa mvumilivu, utaishia njiani.

TANO; WASHIRIKA MUHIMU.

Wewe mwenyewe kama mtu mmoja huwezi kujua kila kitu na huwezi kufanya kila kitu. Hivyo ili kufanikiwa, unahitaji kuwa na washirika muhimu ambao watakuwa tayari kutoa kile ambacho wewe huna. Washirika hawa siyo tu washauri, bali ni watu ambao wanajua kwa kina kile unachofanya na wanakusaidia kupiga hatua zaidi.

 1. Jinsi ya kupata washirika muhimu.

Ili kupata washirika muhimu, kwanza unahitaji kujua ni nini hasa unataka, kisha kujihusisha na watu ambao wanataka kama unachotaka wewe. Unahitaji kujihusisha na watu ambao wana malengo kama yako, tabia kama zako na wanaopenda kukuona unafanikiwa.

Usichague watu kwa sababu tu unawajua au kwa sababu unawapenda. Wanaweza kuwa muhimu kwako kwa mambo mengine, lakini siyo kama washirika muhimu.

 1. Washirika muhimu wanaweza kubadilika.

Kadiri unavyokwenda kwenye maisha yako, yale malengo yako makuu yanabadilika. Hivyo basi hata wale washirika muhimu wanapaswa kubadilika. Pia watu wenyewe wanaweza kubadilika wakawa tofauti na ulivyowachagua mwanzo. Hivyo unapochagua washirika muhimu, usiogope kuwabadilisha pale hali inapowataka wabadilike.

SITA; HAIBA NA TABIA.

Kama tulivyoona, kitu cha kwanza kinachowasukuma watu kununua ni haiba ya muuzaji. Na haiba ya mtu inatokana na tabia ambazo mtu anazo. Ili kufanikiwa kwenye jambo lolote, unahitaji kuwa na tabia nzuri ambazo zinawafanya watu kukubaliana na wewe. Kumbuka ndege wanaofanana huruka pamoja, hivyo kuwavutia watu wa aina fulani, lazima uwe kama wao.

 1. Mauzo ni maonesho.

Mwonekano wako una mchango mkubwa sana kwenye mauzo, hivyo wauzaji wenye mwonekano wa kuvutia wanauza zaidi kuliko wengine wasio na mwonekano wa kuvutia. Mwonekano, uongeaji, kujiamini kote kunachangia kumshawishi mtu kununua au kutokununua kwa anayemuuzia.

SOMA; UMEAMUA KUWAPOTEZA HAWA WATEJA MILIONI SITA?

SABA; HAMASA NA KUJIDHIBITI.

Mauzo ni kuhamisha hamasa kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuaji. Hii ina maana kwamba kabla hujauza lazima wewe mwenyewe uwe na hamasa kubwa, kisha uweze kuihamisha hamasa hiyo kwenda kwa mnunuaji, yaani kumhamasisha mpaka achukue hatua ya kununua.

 1. Vitu vitatu vinavyopima hamasa yako.

Kama muuzaji, mnunuaji anaweza kupima hamasa yako kupitia njia hizi tatu;

Moja; kile unachosema na jinsi unavyokisema. Haijalishi unasema nini, unahitaji kukisema kwa kujiamini na kwa ushawishi. Unahitaji kuweka hisia na hamasa kwenye kila unachoongea.

Mbili; kile unachofanya. Unachosema na unachofanya vinapaswa kuwa kitu kimoja, matendo yana nguvu kuliko maneno. Kama unauza simu za iphone, lakini wewe mwenyewe unatumia samsung, utahitaji kutumia nguvu kubwa sana kuwashawishi watu, na wengi hawatakuelewa. Chochote unachouza, hakikisha wewe mwenyewe unakitumia.

Tatu; kile unachofikiri. Watu wengi wamekuwa wanafikiri fikra zao ni siri, kwamba hakuna anayewaona nini wanafikiria kwenye akili zao. Lakini kile unachofikiri ndiyo kinachotokea kwenye matendo yako. Hivyo kama fikra zako ni hasi, hutakuwa na hamasa kubwa ya kumshawishi mtu anunue.

 1. Udhibiti wa hamasa.

Hamasa inaweza kuwa kitu kizuri, lakini pia hamasa ikizidi sana inakuwa kitu kibaya. Hivyo mtu unahitaji kuwa na udhibiti wa hamasa ambao ni kuweza kujidhibiti wewe mwenyewe. Unahitaji kuweza kujidhibiti ili kuondokana na kelele nyingine zote ambazo hazikusaidii kukamilisha mauzo yako.

NANE; KUJIJENGEA TASWIRA KWENYE MAWAZO.

Kila kitu ambacho kinaonekana sasa, kilianza kama wazo kwa mtu, kisha wazo hili likajengewa taswira ya kitu kilichokamilika, halafu mtu akachukua hatua ya kukamilisha taswira hiyo. Ili uweze kupata matokeo makubwa, juhudi pekee hazitoshi, bali unahitaji kujiona tayari umeshafanikiwa kwenye akili yako.

 1. Kila kitu kikubwa kinaanzia kwenye mbegu ndogo.

Mbuyu unaanzia kwenye mbegu ndogo, kuku wanaanzia kwenye mayai, na mafanikio yako makubwa yanaanzia kwenye mawazo yako. Unahitaji kuwa na wazo la nini unataka, kisha kuona kile unachotaka kwa namna ambayo kimeshakamilika, na kuanza kuchukua hatua kufikia kile unachotaka. Usiogope kwa sababu unaanza kidogo na una taswira kubwa, nguvu ya wazo ni kubwa kama itafanyiwa kazi.

TISA; KUJIAMINI.

Kama muuzaji, unahitaji kujiamini wewe mwenyewe kabla watu wengine hawajakuamini. Na kama tulivyoona kwenye hamasa, watu wanakununua wewe kabla hawajanunua unachouza. Mtu anayejiamini anawafanya wengine nao wamwamini. Mtu asiyejiamini anawafanya wengine wasimwamini pia. Kwa chochote unachouza au kufanya, jiamini kwa kiwango kikubwa.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

KUMI; KUJITUMA NA UONGOZI.

Bila ya kujituma wewe mwenyewe, ni vigumu kufanikiwa. Wapo watu ambao wanasubiri kuambiwa cha kufanya na wanafanya, lakini wale wanaofanikiwa sana, hawasubiri kuambiwa cha kufanya, wao wanafanya kila kinachopaswa kufanywa. Pia uongozi ni muhimu sana, kujiongoza wewe mwenyewe na kuweza kuwaongoza wengine ni hitaji muhimu la mafanikio kwenye mauzo na maisha kwa ujumla.

 1. Viongozi bora ni wauzaji wazuri.

Viongozi wote bora na wakubwa ni wauzaji wazuri, na wauzaji wazuri ni viongozi bora. Hawa wanaelewa jinsi ya kuwashawishi watu, jinsi ya kuwafanya watu wachukue hatua na kushirikiana nao.

Viongozi bora na wauzaji wazuri wote wanatumia falsafa moja kwa mafanikio yao, wanawauzia wafuasi wao chochote wanachotaka kuwauzia kwa kuwajengea imani juu yao kwanza.

 1. Jifunze kuchukua hatua haraka.

Hatua ya kwanza muhimu ya kujijenga kama kiongozi mzuri na mtu anayejituma ni kujijengea tabia ya kufanya maamuzi na kuchukua hatua haraka. Kiongozi anayesitasita kufanya maamuzi na kuchukua hatua huwa anaishia kutokufanya chochote. Pia kiongozi anayebadili maamuzi yake haraka, ni kiongozi ambaye huishia kutokuwa na wafuasi.

 1. Nenda hatua ya ziada.

Msingi mkuu wa kujituma, msingi mkuu wa kulipwa zaidi ya unavyolipwa sasa ni kwenda hatua ya ziada. Kwenye kila kitu unachofanya, angalia namna unavyoweza kutoa thamani zaidi, angalia namna unavyoweza kufanya zaidi ya unavyolipwa, na haitachukua muda mrefu, utaanza kukipwa zaidi ya unavyofanya. Usisubiri mpaka ulipwe zaidi ndiyo ufanye zaidi, anza kufanya zaidi na utalipwa zaidi.

KUMI NA MOJA; UNG’ANG’ANIZI.

Mambo hayatakuwa rahisi, hata baada ya kujua nini unataka, hata baada ya kujitoa kufanya, kujiamini na kwenda hatua ya ziada, utakutana na magumu na utashindwa. Bila ya kuwa king’ang’anizi, hutaweza kufika kule unakotaka kufika.

 1. Chukulia changamoto kama hatua ya kukua zaidi.

Utakapokutana na changamoto kwenye kile unachofanya, na utakutana nazo, usichukulie kama ndiyo mwisho wa kufanya, badala yake jua ni hatua ya wewe kukua zaidi. Jua kwa kuvuka changamoto hiyo utakuwa bora zaidi ya ulivyokuwa kabla ya changamoto hiyo. Na kila changamoto unayokutana nayo ni maandalizi ya mafanikio yako. Usikubali chochote kukuzuia kufika unakotaka kufika.

KUMI NA MBILI; KUFANYA MAUZO.

Baada ya kujiandaa kwa yote ambayo tumejifunza, ambayo ni maandalizi ya kufanya mauzo, unahitaji kukamilisha mauzo. Na hapa ndiyo muhimu, kwa sababu ndiyo unakutana na mteja na kumshawishi kununua kile unachouza. Kuna mambo mawili muhimu unapaswa kuyafanya kwenye kukamilisha mauzo, kujua kama mteja ni sahihi na kubadili fikra za mteja kutoka hasi mpaka chanya.

 1. Jinsi ya kumpima mteja kama ni sahihi.

Kabla hujatumia muda mwingi kumshawishi mteja kununua, unahitaji kujua kama ni mteja sahihi wa kile unachouza. Hivyo unahitaji kumpima kwa vigezo vifuatavyo;

Je ni fedha kiasi gani mteja yupo tayari kutumia kwenye kile unachouza?

Je mazingira ni sahihi kwa mnunuaji kufanya maamuzi ya kununua?

Je mnunuaji anaweza kufanya maamuzi mwenyewe au mpaka ashirikiane na mtu mwingine?

Kama mnunuaji anahitaji kushirikiana na mtu mwingine kufanya maamuzi ya kununua, je unaweza kuwepo kwenye ushiriki huo ili umshawishi na huyo mwingine pia?

Katika kumjua vizuri mnunuaji na kujua njia za kumshawishi, lazima umpe nafasi kubwa ya kuongea na wewe kusikiliza kwa makini huku ukiuliza maswali muhimu.

 1. Kubadili fikra za mnunuaji.

Kama mnunuaji ana fikra hasi, hakuna kiasi cha hamasa kitakachomfanya anunue kama hajabadili fikra zake kwanza. Hivyo ni kazi yako muuzaji kujua fikra alizonazo muuzaji na kisha kufanya kazi ya kuzibadili.

Kujua kama fikra za mnunuaji zipo sahihi kwa ajili ya kununua, unahitaji kuangalia vitu vitatu;

Moja; mnunuaji anamwamini muuzaji na anajiamini yeye mwenyewe.

Mbili; mnunuaji ameonesha kuvutiwa na kile ambacho muuzaji anauza.

Tatu; muuzaji ana hamasa ya kununua, kwa kuona umuhimu na uhitaji wa kinachouzwa.

Rafiki, maisha ni mauzo na mafanikio yoyote kwenye maisha yanategemea uwezo watu wa kuuza. Kila siku, kazana kuwa muuzaji bora zaidi, jijenge kuwa mtu bora, jiamini, weka juhudi na weza kuwashawishi wengine kuchukua hatua zaidi. Mafanikio yako ni matokeo ya mauzo yako. Kazana kuuza zaidi na zaidi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji