Mpendwa  rafiki,

Kwa asili ndoa haina shinda ila watu ndiyo wanashida vivyo hivyo hata kwa akili zetu kwa asili ni safi ila sisi wenye ndiyo tunaingiza uchafu katika akili zetu. Tunaingiza kila kitu bila hata kuchuja ndiyo maana kile kimuingiacho mtu ndicho kimtokacho. Huwezi kutoa mazuri kama unaingiza mabaya katika akili yako hivyo kile unachoingiza ndicho kitakachotoka nje. Hata kile unachokula ndicho kinakufanya uonekane hivyo ulivyo sasa.

Kuna tabia za kushangaza kwa baadhi ya wazazi au wanandoa wanaounda familia. Hizi tabia ndiyo zinaleta mpasuko, kugawa familia na mwisho wake ni kuharibu familia. Kwa mfano, mzazi au mwandoa mmoja anajifanya kuwapenda watoto kuliko mwenzi wake. Tena utakuta mzazi huyo mmoja anasema watoto wangu ndiyo kila kitu hivyo thamani kubwa katika familia wanapewa watoto kuliko mmoja wa wanandoa. Huenda ikawa baba ndiyo anajifanya anaupendo wa kweli sana kwa watoto hata haoni thamani ya mke wake.

malezi bora
silhouette of parents and their children on the beach

Rafiki, sasa kama baba anawapenda watoto na kumdharau mama wa hao watoto inakuwa ni kitu cha kushangaza mke unayemdharau au mume unayemdharau ndiyo chanzo au kisababishi cha hao watoto unaojidai unawapenda kweli.  Hakuna mzazi ambaye ni bora kuliko mwingine wote ni muhimu ndiyo maana wakaitwa wazazi, kila mmoja ana thamani  na nafasi yake katika familia.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; A Gift To My Children (Zawadi Ya Baba Kwa Watoto Wake, Masomo Ya Maisha Na Uwekezaji).

Unakuta tena baadhi ya wazazi wanamwaga sumu kwa watoto kila mmoja anamsemea  vibaya kwa watoto na watoto wanakuwa wanapokea vitu ambavyo haviwahusu kabisa, mara baba au mama yako ana changamoto hii hivyo watoto wanakuwa wanaathirika kiakili kwa sababu ya wazazi kuwashirikisha changamoto zao za ndoa.

Baba na mama mnatakiwa kuwa kitu kimoja, siyo mama au baba kuegemea kwa watoto na kumuona mwenzako wa ndoa hana maana. Kabla hujaanza kumuona mwenzako wa ndoa hana maana jiulize wewe peke yako ungeweza kuwapata hao watoto unaoringa nao kwa sasa? Wazazi wanatakiwa kupeana heshima kila mmoja ampe mwenzake heshima kuwa kwenu kitu kimoja ndiyo kumesababisha kuwa na watoto.

Kauli za ubinafsi unakuta zinatawala kama vile hawa ni watoto wangu badala ya kusema hawa ni watoto wetu utafikiri alishiriki kuwapata peke yake. Kuna tabia za ajabu sana katika baadhi ya familia baba au mama anakuwa sumu katika familia badala ya kuleta amani ndiyo anakuwa mwiba wa kuchoma familia.

SOMA; Jinsi Ya Kumfundisha Mtoto Kuwa Mfikiriaji Bora Na Mwenye Uwezo Mkubwa Akili

Hatua ya kuchukua leo, wazazi au wanandoa mnaalikwa kuacha tabia ya kudharauliana na kuwaona watoto ndiyo bora kuliko mwenza wako wa ndoa. Bila ndoa kuwa bora haiwezi kuzaa familia bora na bila kuwa na familia bora hatuwezi kuwa na jamii bora.

Kwahiyo, si vema wazazi kuonesha tabia hasi kwa watoto kwani wazazi ndiyo kiini cha malezi na watoto wanaiga na kujifunza vitu vingi kutoka kwao. Kama wazazi mnakuwa mna migogoro yenu tafadhali malizaneni nyie kwa nyie lakini siyo kuonesha kwa watoto inakuwa ni picha hasi.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu  kwa kutembelea tovuti  hii hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !