Mpendwa rafiki yangu,

Kabla ya kuingia kwa teknolojia watu wengi tangu zamani walikuwa wanawasiliana kwa njia ya barua. Licha ya kukua kwa teknolojia bado barua inatumika kama mfumo rasmi wa wa mambo ya kazi lakini kama unataka kusalimiana siku hizi huna haja ya kumwandikia barua tena mtu badala yake unamwandikia tu ujumbe kupitia simu zetu za mikononi, barua pepe, mitandao ya kijamii nakadhalika. Hakika dunia imeunganishwa na kuwa kitu kimoja kupitia mfumo wa Tehama yaani teknolojia ya habari na mawasiliano kiujumla.

Kama ukiingia katika ofisi mbalimbali baadhi ya ofisi utakuta wamebandika cheti cha heshima kwa kupongezwa baada ya kufanya vizuri katika eneo fulani kadiri ya asili ya kazi hiyo. Kwahiyo lugha ya maandishi bado inaendelea na itaendelea kudumu daima ni fasihi nzuri sana ambayo watu hutumia kuwasilisha ujumbe.

Je utawezaje kumwamasisha mwenza wako au mtu yeyote yule? Kila aina ya maisha yanahitaji hamasa, iwe ni maisha ya ndoa au hata wito mwingine unahitaji hamasa ili uendelee kustawi vizuri. Muda mwingine watu wanapoteza hamasa hata katika kazi lakini kwa kupitia njia hii nayo kwenda kukushirikisha leo itakusaidia kumwamasisha mwenza wako pale ambako unaona hayuko katika mstari.

Walioshindwa

Rafiki, njia ya kumwamasisha mwenza wako au mtu yeyote yule ni kumwandikia barua. Kama mke au mume wako kuna mambo anafanya vizuri jaribu siku kukaa chini andika barua bila ya yeye kujua halafu mfanyie kumshangaza kumpatia hiyo barua. Elezea hisia zako zote kuhusu yeye, mweleze ni jinsi gani amekuwa msaada kwako, jinsi gani anagusa maisha yako. Mpongeze kwa yale anayofanya hata kama kuna sehemu unaona amekosa hamasa basi mwamasishe kupitia barua hiyo mtie nguvu hakika akija kukaa chini na kusoma na kutafakari atashukuru na utakuwa kama umewasha moto ndani yake wa kwenda kufanya makubwa zaidi.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinachoitwa LETTERS From A SELF-MADE MERCHANT To His SON.

Tunaona hata katika maeneo yetu ya kazi, mtu akifanya vizuri akiandikiwa barua na mkuu wake wa kazi kwa kufanya vizuri inamwamasisha zaidi kuliko hata maelezo. Kwa mfano, ikitokea leo unaandikiwa barua na raisi kwa kukupongeza kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya hata kama ulikuwa unataka kuishia njiani hutokubali utaendelea kukaza mwendo kwani ile barua ya pongezi imekuwa ni kama kichocheo cha kumpa nguvu. Kama wewe ni bosi waandikie wafanyakazi wako  barua ya kuwapongeza kadiri ya mazuri wanayoyafanya kwa kufanya hivyo utawarudishia nguvu na kuona kuwa unawathamini na unajali mchango wao kuwa yeye ni mtu muhimu hapo katika kampuni au taasisi.

Hata siku unapokuwa hauko duniani, mwenza wako akiwa anasoma zile barua ulizokuwa unamwandikia kwa kumwelezea ni namna gani amekuwa shujaa kwako itaendela kumpa faraja. Maandishi yana mfanya mtu atafakari zaidi na kukaa kichwani kwa kile ulichomwandikia. Hata kama unataka kumkosoa ni vema ukaanza na mazuri halafu pia ukamwandikia kuna mambo fulani moja ,mbili naomba uyafanye hivi badala ya kufanya vile.

Una mtu wako ambaye amekuwa sehemu ya maisha yako, ni shujaa wako katika eneo fulani la maisha yako, unavutiwa na maisha yake basi kaa chini na mwandikie barua hii itamwongezea hamasa na kuonesha kuwa kuna watu wanajali kile wanachofanya hivyo ataongeza juhudi kutoa kile ambacho anapaswa kutoa ili kufanya maisha ya wengine kuwa bora.

SOMA; Jinsi Wanandoa Wanavyoharibu Familia

Hatua ya kuchua leo, una mwenza wako au mtu yoyote unataka umwamasishe juu ya kitu fulani? Kama jibu lako ni ndiyo basi kaa chini na mwandikie barua na mpatie kama  barua ya pongezi. Unapomwandikia mtu barua inakuwa ina nguvu kuliko kumwambia kwa mdomo.

Hivyo basi, hakuna binadamu ambaye hapendi kuthaminiwa. Kila binadamu anapenda kuona akithaminiwa kwani ni hitaji la kwanza la kila mmoja wetu kuthaminiwa. Unapomwandikia rafiki, ndugu, mwenza, mfanyakazi, bosi, kiongozi fulani kumpongeza juu ya kitu fulani unakuwa umeonesha ishara chanya ya kumthamini.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !