Rafiki yangu mpendwa,
Hongera kwa siku hii nzuri sana ya leo, siku ya mafanikio, siku ya kufanya makubwa na siku ambayo tunakwenda kujifunza gharama kubwa ya uhuru unayopaswa kulipa ili kufanikiwa.
Kabla ya kujifunza gharama hii, tupate kwanza kisa kifupi cha mbwa na mbwa mwitu.
Siku moja mbwa katika pitapita zake alikutana na mbwa mwitu. Mbwa mwitu yule alikuwa amechoka sana, afya yake imedhoofu na haonekani kuwa na maisha mazuri. Kwa upande wake mbwa alikuwa na afya nzuri, amenenepa na hajachoka maana siku nzima alikuwa amepumzika.
Mbwa akamuuliza mbwa mwitu, vipi rafiki yangu? Mbwa mwitu akamjibu mambo ni magumu, mawindo yamekuwa adimu, tunahangaika siku nzima kupata mawindo lakini hayapatikani. Pia ushindani umekuwa mkubwa kwani mbwa mwitu tumekuwa wengi.
Mbwa kwa masikitiko akamwambia mbwa mwitu, sisi wenzako hatuna shida kabisa, tunakula chakula kizuri ambacho tumeandaliwa, hatuhitaji kuzunguka siku nzima ili kupata chakula. Na hata kazi zetu siyo ngumu, ni kubweka mara chache usiku ili ujulikane upo na uonekane kweli ni mkali, hapo utaendelea kulishwa vizuri na kupata sehemu nzuri ya kuishi.
Mbwa akaendelea kumwambia mbwa mwitu, nakushauri rafiki yangu uje kwenye upande huu wa maisha, upande ambao hutakuwa na shida wala matatizo kama uliyonayo sasa.
Mbwa mwitu akiwa amepata tamaa, huku mate yakimtoka kwa habari za vyakula vizuri alivyosikia, alimwangalia mbwa kwa muda kisha kama akashtuka, aliona mnyororo ambao mbwa anao shingoni kwake. Akamuuliza na huo mnyororo shingoni kazi yake nini?
Mbwa akauangalia na kujibu, huwa wanautumia kunifunga ili nikae pale wanapotaka nikae. Mbwa mwitu akapatwa na butwaa, akaongeza, kwa hiyo pamoja na hayo yote mazuri unafungwa mnyororo? Wacha nikimbie na nitaendelea kukimbia maisha yangu yote, uhuru wangu ni mkubwa kuliko chakula na malazi.
Na mpaka leo mbwa mwitu anaendesha maisha yake mwituni kwa uhuru wake mwenyewe, na mbwa anaendelea kufugwa na binadamu, akilishiwa kwa wakati anaopangiwa na kufungwa mnyororo ili akae wanapotaka akae.
Hichi ni kisa kifupi, kisa cha zamani sana ambacho kinaelezea gharama kubwa unayopaswa kulipa ili uwe huru.
Kabla sijafafanua kwa ufupi sana jinsi uhuru ulivyo na gharama, nikupe mfano unaoendana na kisa hichi.
Kuna marafiki wawili ambao walisoma pamoja, lakini baada ya kuhitimu hawakuwahi kuonana, wanakuja kuonana miaka kumi baadaye. Mmoja anaonekana kuwa na mafanikio makubwa, maisha mazuri, afya nzuri. Mwingine anaonekana kuchoka na maisha kama hayaendi vizuri kwake.
Rafiki wa kwanza anaanza kumwambia mwenzake, mimi nimeajiriwa na kampuni fulani, kila mwezi wananipa mshahara kiasi fulani, wananipa nyumba ya kukaa, wananipa gari ya kusafiri na afya yangu wanailinda na kuigharamia wao wenyewe.
Rafiki wa pili ambaye ni mjasiriamali, ambaye ameanzisha kampuni tatu na zote hazijafanya vizuri, hana uhakika wa mwezi ujao fedha ya kuendesha maisha anaipata wapi, anamwangalia mwenzake kwa wivu, akitamani yale ndiyo yawe maisha yake. Akimwangalia na kuona anaweza kunufaika na fursa fulani ambayo ni nzuri kwake, akamwambia kesho twende nikakuoneshe fursa nzuri itakayokufaa, muda wa mchana utakuwa mzuri.
Rafiki wa kwanza akamjibu muda wa mchana haitawezekana, nitakuwa kazini, siwezi kutoka muda wa kazi. Rafiki wa pili akamwambia, basi kama hutaweza kutoka, niambie kama utakuwa na kiasi fulani cha fedha, ili nisitoe fursa hiyo kwa wengine mpaka utakapopata muda. Rafiki wa kwanza akamwambia kwa sasa fedha sina, ni mpaka mwisho wa mwezi, na hapo nina madeni ya kulipa.
Rafiki wa pili akamwangalia mwenzake kwa butwaa, akasema, unaniambia kwamba kazi inakupa kila kitu, lakini huna muda wa kufanya chochote unachotaka wewe, na wala huna fedha za kufanya yale muhimu, na kama haitoshi una madeni ya kulipa? Ni bora niendelee kupambana kwenye ujasiriamali, nikipanga kutumia muda wangu nitakavyo na kipato ninachopata niweze kukisimamia mwenyewe.
Rafiki yangu, naamini umepata kile ambacho nilitaka upate hapo, na sihitaji kuongeza maelezo mengi zaidi.
Kikubwa unapaswa kujua ni kwamba, kila kitu kwenye maisha kina gharama, na uhuru una gharama tena kubwa. Ni labda uwe tayari kuteseka, uwe tayari kupitia magumu lakini ujijengee msingi imara wa baadaye. Au umkabidhi mwingine mateso yako na yeye akuhakikishie kupata yale ya msingi, lakini ahakikishe hutapata mafanikio makubwa, maana ukiwa huru sana hatanufaika na wewe.
Maisha ni kuchagua rafiki, na unaweza kuteseka mwanzoni na baadaye mambo yakaenda vizuri, au usiteseke sana mwanzoni ila maisha yako yakaenda na kiasi fulani cha mateso mara zote.
Uhuru una gharama kubwa, na mafanikio ni zao la uhuru. Wengi hawapo tayari kulipa gharama hiyo kubwa, ndiyo maana hawafanikiwi.
Chagua leo, unataka kuwa mbwa au unataka kuwa mbwa mwitu, halafu ishi maisha yako kwa kile ulichochagua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.
Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa; www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha
Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha
Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog