Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanajua aina moja ya akaunti ya kifedha, ambao ni akaunti ya benki, au akiba na uwekezaji ambao wamekuwa wamefanya. Hivyo ukitaka kuangalia utajiri wa mtu, unaangalia ni kiasi gani cha fedha anacho kwenye akaunti zake za benki na uwekezaji kiasi gani amefanya.

Lakini ipo aina nyingine ya akaunti ya kifedha, ambayo wengi hawaijui na imekuwa kikwazo kwa wengi kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha aina hii ya akaunti na jinsi inavyokuzuia kufikia utajiri. Pia nitakushirikisha njia za kukuza aina hiyo ya akaunti ili uweze kufikia utajiri.

Kabla sijaendelea, huwa wapo watu wanaopenda kujidanganya na kujiwekea unafiki. Hawa ni watu ambao wakisikia neno utajiri basi wanaona ni kitu kibaya. Kama wewe ni mmoja wa watu hao, unaweza tu ukaishia hapa, na ukaendelea na mambo mengine. Kwa sababu kama ukisikia utajiri unajisikia vibaya, basi jua hutaufikia utajiri. Na japo unaweza kuwahadaa watu kwa nje kwamba ukisikia utajiri unajisikia vibaya, ndani yako unajua kabisa ni kwa jinsi unatumia muda mwingi wa maisha yako kufikiria fedha. Moja ya hatua za kupata fedha na kufikia utajiri, ni kuwapenda matajiri, lakini hii ni makala ya siku nyingine.

Aina ya pili ya akaunti ya kifedha, ukiacha akaunti ya benki, ni akaunti ya fedha ya kisaikolojia. Kila mmoja wetu, ana kiwango chake cha kifedha kwenye fikra zake, ambacho ndiyo ameshajiambia anapaswa kupata kiwango hicho. Yaani kila mmoja wetu, kuna kiwango chake cha fedha, ambacho ameshakiweka kwenye fikra na mawazo yake, na akishapata kiwango hicho basi akili yake inatulia na hakazani tena kupata fedha zaidi.

652d5-tangazo2bmasikini

Inapotokea mtu kiwango cha fedha alichonacho kipo chini ya kile anachohitaji kisaikolojia, ataweka juhudi zaidi, atajisukuma zaidi ili kupata kiwango cha fedha anachohitaji. Atafanya kazi hata usiku na mchana, ili kufikia kiwango kile kinachompa kuridhika.

Sasa hatari na shida kubwa ipo pale kiwango cha fedha cha mtu kinapokuwa kikubwa kuliko kiwango alichojiwekea kisaikolojia. Hapa ndipo utashangaa vituko ambavyo wengi wanafanya na fedha, wanakazana kupoteza fedha ili warudi kwenye kile kiwango ambacho wamekubaliana nacho kisaikolojia.

Pale mtu anapopata fedha nyingi kuliko alivyozoea, na inayozidi kile kiwango chake cha kifikra cha fedha, atatafuta kila njia ya kupunguza na kupoteza fedha hizo mpaka arudi kwenye kiwango sahihi kwake. Atanunua vitu ambavyo hata hahitaji, atagawa fedha kwa watu wasio hata na uhitaji, atafanya maamuzi mabovu kibiashara na kiuwekezaji. Yeye mwenyewe anaweza asielewe kwa nini anafanya hivyo, lakini akili yake inapambana arudi kwenye kiwango chake cha fedha alichozoea.

SOMA; Huo mnyororo shingoni kazi yake nini? (gharama ya uhuru unayopaswa kulipa ili kufanikiwa).

Kama umewahi kumsikia mtu anasema akiwa na fedha basi akili yake inapotea kabisa, ni mpaka fedha hizo ziishe ndiyo anaweza kukaa chini na kufikiri. Na wengi wanapokuwa hawana fedha wanakuwa na mawazo mazuri sana ya utekelezaji. Tena wakiwaona watu wanatumia fedha vibaya, wanasema kabisa wangepata fedha hizo wangefanya mambo mazuri sana. Ni mpaka pale wanapopata fedha hizo ndiyo wanapoteza kabisa mawazo mazuri waliyokuwa nayo, wanapoteza fedha hizo, na zikishaisha ndiyo wanaanza kujutia kwamba wamefanya nini.

Waangalie watu wote ambao wamepata fedha nyingi kwa mkupuo, kiasi kikubwa cha fedha ambacho hawajawahi kukishika kwenye maisha yao. Waangalie watu ambao wameshinda bahati nasibu, waangalie watu ambao wamerithi mali, waangalie watu ambao wamepokea mafao. Wengi haiwachukui muda wanakuwa wameshapoteza fedha nyingi walizopata na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida.

Wanakuwa wamepata fedha nyingi kwenye akaunti ya benki, lakini akaunti yao ya kisaikolojia inasoma kiwango cha chini. Hivyo wanaacha kufikiria kabisa kuhusu fedha, wanaanza kupoteza fedha, mpaka zinapofika kwenye kile kiwango chao cha kisaikolojia ndiyo wanastuka na kuanza kufikiria kuhusu fedha.

Njia pekee ya kuepuka kurudishwa nyuma na akaunti hii ya fedha ya kisaikolojia ni kukuza zaidi akaunti hii. Unahitaji kujizoesha kifikra na kisaikolojia kuwa na fedha nyingi, hata kama bado hujazishika kwenye mikono yako au kuwa nazo kwenye akaunti yako ya benki. Na unaweza kuanza kwa kufikiria mara kumi ya kipato unachopata sasa, kisha kufikiria kipato hicho mara kwa mara, kukiwekea mipango na kuweka lengo lako la kipato liwe ni kukua kufikia mara kumi ya kipato chako cha sasa. Kwa njia hii utaongeza kiwango chako cha fedha kisaikolojia.

Pia unaweza kufikiria mara 100, mara 1000 na hata zaidi ya kipato unachopata sasa. Fikra zote hizo zitaiandaa akili yako kupokea fedha zaidi na kuweza kutulia na fedha zaidi unazopata. Unapofikiria mara elfu moja ya kipato unachopata sasa, ongezeko kidogo halitakusumbua kama linavyokusumbua sasa.

Unahitaji pia kujifunza kutobadilishwa na fedha. Kwa sababu watu wengi huwa ni rahisi sana kuwasoma kiwango cha fedha walichonacho kwa kuwaangalia kwa nje. Watu wengi wakiwa hawana fedha utawajua hata wasipokuambia. Pia wakiwa na fedha utajua tu, hata kama hakuna anayekuambia. Tabia zao kwa upande wa fedha zinafanya kila mtu ajue kama wana fedha au la. Hii inawafanya watu hao kuwa wateja wa watu wengine, kwa sababu watu wakishajua una fedha, watahakikisha wanazipata fedha hizo, iwe ni kwa kuomba, kwa kuiba au kwa kukuuzia kitu. Jifunze kutokusomeka kirahisi kwa nje kama una fedha au la.

Rafiki, ninayo mafunzo mengi na mazuri kuhusu ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, mafunzo haya yameingia kwa ndani sana kuhusu fedha, kuanzia kuongeza kipato, kudhibiti matumizi, kuwekeza na kufikia uhuru wa kifedha. Kama hujayapata mafunzo haya, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, nitakupatia mafunzo haya ili uweke sawa upande wako wa kifedha.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji