Rafiki yangu mpendwa,

Inapokuja kwenye biashara, vikwazo vikubwa huwa ni viwili, muda na fedha. Kama kila mtu angeweza kuwa na muda wowote anaotaka na akawa na fedha zozote anazotaka kuwa nazo, basi angeweza kuendesha biashara yake kwa jinsi anavyotaka yeye.

Lakini vitu hivyo viwili vina ukomo, muda wetu ni masaa 24 tu kwa siku, hakuna anayeweza kuongeza zaidi ya hapo. Na pia kiasi cha fedha tunachokuwa nacho, hasa mwanzoni mwa biashara huwa kina ukomo.

Ili kuvuka vikwazo hivyo viwili, watu wamekuwa wanatumia nyenzo au kama wanavyoita kwa kiingereza leverage, yaani unatumia kitu ambacho huna ila unanufaika. Kwenye fedha, nyenzo ni kutumia fedha za wengine, na hapa ndipo mikopo na hata ushirika unapohusika. Kwenye muda nyenzo inayotumika ni kutumia muda wa wengine, ambapo unawaajiri watu wafanye kile unachotaka kufanya ila huna muda wa kufanya.

Nyenzo hizi, pamoja na kuwa na manufaa kwa anayezitumia, huwa zinakuja na gharama zake na changamoto pia. Kwa upande wa fedha, unapotumia fedha za wengine utalipa gharama ya riba ambayo inaweza kuwa kubwa na pia wakati mwingine utapoteza nguvu ya kufanya maamuzi kwenye biashara yako. Kwenye muda wa wengine, unapoajiri unajiingiza kwenye jukumu la kuanza kuwasimamia watu, ambao wanaweza kuwa na changamoto nyingi.

Ili kuepuka changamoto za fedha, watu wamekuwa wanadunduliza akiba na kupata mitaji ya kuanzisha biashara, kisha kuiacha biashara ijikuze yenyewe kwa kurudisha faida yote kwenye biashara.

Ili kuepuka changamoto za kuajiri, watu wengi wamekuwa wanaendesha biashara zao wenyewe, wakisimamia kila kilicho muhimu. Na hapa ndipo wengi wanapokwama kwenye ukuaji wa biashara zao, maana ni vigumu kufanya kila kitu mwenyewe.

Mwandishi Elaine Pofeldt kupitia utafiti aliofanya kwa wafanyabiashara wanaoendesha biashara zao wenyewe na wenye mafanikio makubwa, ametuandalia kitabu ambacho ni mwongozo mzuri kwa wale wanaoanza biashara zao wenyewe.

Kupitia kitabu hichi, Elaine anatuonesha kwamba unaweza kabisa kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa, zaidi ya dola milioni moja za kimarekani (shilingi bilioni mbili za kitanzania) na pia ametuonesha ni kwa jinsi gani tunaweza kufanya hivyo.

million dollar one person bussiness

Karibu sana kwenye uchambuzi wa kitabu cha THE MILLION-DOLLAR, ONE-PERSON BUSINESS tujifunze jinsi ya kuja na wazo bora la biashara unayoweza kuendesha mwenyewe, jinsi ya kutengeneza mikakati ya kuigeuza ndoto yako kuwa uhalisia na jinsi ya kukuza biashara yako baada ya kuanza.

BISHARA YA MTU MMOJA SIYO HITAJI LA KILA MTU.

Ukweli ni kwamba, kukuza biashara ukiwa kama mtu mmoja na ikafikia ngazi kubwa kabisa siyo rahisi. Lakini siyo watu wote wanaopenda kufanya vitu na watu wengine. Wapo wengi ambao wanapenda kuwa na uhuru wao, kufanya kile wanachotaka kwa namna wanavyotaka wao, na hao ndiyo wanaopenda kuendesha biashara zao wao wenyewe, kwa jinsi wanavyotaka wao.

MAZINGIRA YAMEKUWA RAHISI KUANZISHA BIASHARA.

Kwenye zama tunazoishi sasa, mazingira yamerahisisha sana kuanzisha biashara. Popote ulipo, ukiwa na uwezo wa kuingia kwenye mtandao wa intaneti, unaweza kuandikisha na kuanzisha biashara yako ndani ya muda mfupi. Hata hapa nchini kwetu Tanzania, sasa hivi unaweza kusajili biashara au kampuni yako kupitia mtandao wa intaneti.

HUHITAJI KUFANYA KILA KITU MWENYEWE.

Licha ya kwamba utaendesha biashara yako mwenyewe, huhitaji kufanya kila kitu mwenyewe. Unaweza kuwatumia watu wengine kukuzalishia chochote unachotaka, wewe ukakipa jina lako na kuuza. Kupitia mtandao wa intaneti unaweza kuuza chochote unachotaka kuuza kama unaweza kutafuta soko. Maana wazalishaji ni wengi, ila wenye uwezo mkubwa wa kuuza ni wachache.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Umuhimu Na Upekee Wako Kwenye Biashara Unayofanya.

MAHITAJI MATATU YANAYOWAFANYA WATU KUENDESHA BIASHARA ZAO WENYEWE.

Hitaji la kwanza; udhibiti wa muda. Wengi wa wanaoingia kwenye biashara zao wenyewe, wanataka kudhibiti muda wao wenyewe. Hawataki kuwa waajiriwa, ambapo watawajibika kwa watu wengine. Na pia hawataki kuajiri ambapo watahitaji kuwasimamia wengine. Wanataka kutumia muda wao kwa namna wanavyotaka wao.

Hitaji la pili; kuwa na fedha za kutosha kufanya wanachotaka kufanya. Hapa watu wanasukumwa kutengeneza kiasi cha fedha kitakachowawezesha kuishi kama wanavyotaka wao.

Hitaji la tatu; kuishi maisha wanayotaka wao wenyewe. Unapoajiriwa, mtu mwingine anakupangia uendesheje maisha yako. Unapoajiri watu wengine, inabidi uwepo karibu nao kuhakikisha wanafanya kama unavyotaka wafanye, yote hayo yanakuzuia wakati fulani usifanye baadhi ya vitu unavyotaka.

AINA SITA ZA BIASHARA AMBAZO UNAWEZA KUENDESHA WEWE MWENYEWE.

MOJA; Bishara ya kuuza vitu kupitia mtandao wa intaneti, hapa ni sawa na kufungua soko kwenye mtandao wa intaneti na kuuza chochote unachoweza kuuza. Hata kama hujakitengeneza wewe mwenyewe.

MBILI; Uzalishaji. Wengi wakisikia uzalishaji wanaweza kukataa kwamba ni biashara inayoweza kufanywa na mtu mmoja. Lakini kwa zama hizi, unaweza kuzalisha na kuuza chochote. Unachohitaji ni kuwa na wazo na kuwa na soko, kisha kuwatumia watu wengine kuzalisha unachotaka na wewe ukauza. Tena kama utajumuisha na namba moja hapo juu, unaweza hata usiguse kinachozalishwa. Unachofanya ni unakuwa na mtandao unaotumia kuuza kile unachozalisha, na unakuwa na wazalishaji, halafu wewe unakuwa kama mtu wa kati, mteja anakulipa wewe, wewe unamlipa anayezalisha na anatuma bidhaa kwa mteja. Yaani unaingiza fedha bila hata ya kugusa chochote, ni kuwa na wazo bora lenye kutatua changamoto za watu na kujua jinsi ya kuwafikia.

TATU; Uandaaji wa maarifa na taarifa. Kupitia mtandao wa intaneti, na hata njia za kawaida kama vitabu, video na sauti, unaweza kuandaa na kuuza maarifa na taarifa mbalimbali ambazo wengine wanazihitaji ili kufanya maamuzi fulani. Kupitia uandishi unaweza kujenga biashara kubwa unayoweza kuiendesha wewe mwenyewe.

NNE; huduma za kitaalamu na biashara ya ubunifu kama huduma za masoko, huduma za ushauri mbalimbali na hata huduma ya uongeaji. Hapa mtu anaweza kutumia taaluma au uzoefu wake kuanzisha biashara ambapo anawasaidia wengine kwenye yale maeneo yenye uhitaji. Anafanya hivi kwa ushauri au usaidizi kwa kadiri wateja wake wanavyohitaji.

TANO; Huduma binafsi kama ya ukocha au ushauri. Hapa mtu anaweza kuanzisha biashara yake kama kocha kwenye maeneo mbalimbali ambayo yeye ana ujuzi au zoefu ambao wengine wanauhitaji.

SITA; Mali na majengo. Hii ni aina ya biashara ambapo mtu mmoja anaweza kumiliki mali na majengo ambayo anauza au anapangisha kwa watu wengine.

NJIA TATU UNAZOHITAJI KUTUMIA KUENDESHA BIASHARA YA MTU MMOJA.

Kwa kuwa huwezi kuwa na muda wa kufanya kila kitu, kuna njia tatu za kurahisisha ufanyaji wa mambo kwenye biashara inayoendeshwa na mtu mmoja.

Moja; kutoa kazi kwa wengine (outsourcing), hapa unatoa kazi kwa watu wengine ambao wanakufanyia kwa mkataba maalumu. Huhitaji kuwaajiri watu hao, hivyo wanakupa unachotaka kwa makubaliano mliyowekeana. Hii inakupunguzia mzigo wa kuwa na watu unaowasimamia kufanya unachitaka wafanye.

Mbili; kutengeneza mifumo inayojiendesha yenyewe. Hapa mtu huhitaji kufanya kila kitu wewe mwenyewe, badala yake unatengeneza mifumo inayokusaidia kwa yale ambayo siyo lazima ufanye mwenyewe. Mfano kutuma na kujibu jumbe mbalimbali kwa njia ya simu au barua pepe. Kukusanya mawasiliano ya wateja wako. Kuwasiliana na wateja wako na kadhalika.

Tatu; teknolojia ya simu. Simu zimerahisisha sana ufanyaji wa biashara, kitu ambacho kingetumia muda mrefu kuafikiwa, sasa unaweza kufanya kwa muda mfupi sana.

KITU PEKEE KINACHOFANYA BIASHARA YA MTU MMOJA KUFANIKIWA.

Haijalishi ni biashara ya aina gani mtu anakuwa amechagua kufanya, ili biashara ambayo mtu mmoja anaendesha ifanikiwe, lazima iwe ni kitu ambacho yeye mwenyewe anakipenda na yupo tayari kukifanya hata kama halipwi. Kama unataka kuingia kwenye biashara ya mtu mmoja kwa sababu unaona utafanikiwa haraka, unajidanganya. Mafanikio yako, lakini siyo ya haraka.

Wengi wanaoingia kwenye biashara wenyewe, wanakuwa hata hawakupanga wataingia kwenye biashara, ila wanajikuta na uhitaji fulani ambao hawawezi kupata suluhisho lake, wanatengeneza suluhisho kwao na kuwashirikisha wengine pia.

USIDANGANYIKE, WATU NI MUHIMU SANA.

Kwa kuwa unafanya biashara mwenyewe, usijidanganye kwamba huhitaji watu wengine, kwamba unafanya kila kitu mwenyewe. Unachokuwa umekwepa ni kubeba mzigo wa kuajiri watu, lakini bado utahitaji kuwatumia wengine kukamilisha yale unayotaka na kuhitaji. Hivyo utahitaji kufanya kazi na watu kwa mikataba maalumu. Utahitaji kuwatumia watu wengine kusambaza kile unachouza. Hivyo unahitaji kuweza kushirikiana na wengine ili biashara yako iweze kukua.

Na muhimu zaidi, wateja wako ni muhimu sana, unahitaji kutengeneza nao uhusiano mzuri ili waweze kuwa wateja waaminifu kwenye biashara yako.

SOMA; Huo mnyororo shingoni kazi yake nini? (gharama ya uhuru unayopaswa kulipa ili kufanikiwa).

JE BIASHARA GANI UNAWEZA KUFANYA WEWE MWENYEWE?

Kama tulivyoona hapo juu, kuna ina sita za biashara unazoweza kuendesha wewe mwenyewe. Lakini huo siyo ukomo, hayo ni majibu ya utafiti wa mwandishi wa kitabu. Hivyo unaweza kufanya biashara yoyote ambayo wewe unataka, wewe mwenyewe, kama utaweza kutimiza yafuatayo;

Moja; lazima upende sana kile utakachokuwa unafanya, iwe ni kitu kinachokunyima usingizi, kitu ambacho huwezi kukivumilia kwa namna kilivyo.

Mbili; lazima uwe na soko unaloweza kulifikia, ujue kabisa wapo watu wenye uhitaji wa kile unachopanga kuuza na ambao wanamudu kulipa ili kukipata.

Tatu; lazima uchague njia ambayo rahisi kwako kutumia kuwafikia wateja wako na isiyokuhitaji uwe na watu uliowaajiri. Mtandao wa intaneti ni njia nzuri ya kuwafikia wateja wako. Angalia jinsi gani biashara yako inaweza kutumia intaneti, simu na hata njia nyingine kuwafikia wateja wako.

Nne; unahitaji kuwajua watu utakaopaswa kushirikiana nao ili biashara yako iweze kwenda vizuri. Kuna vitu vingi huhitaji kufanya wewe mwenyewe, jua watu gani wanaweza kukufanyia kwa gharama ambayo wewe utaweza kutengeneza faida kwa mauzo utakayofanya.

Tano; jipe muda na kuwa tayari kuweka kazi, utahitaji kujituma zaidi na itakuchukua muda kufikia mafanikio makubwa. Japo muda unatofautiana kulingana na biashara, lakini kadiri unavyokuwa umehamasika kwenye biashara yako, na kadiri unavyojituma, itakuchukua muda mfupi zaidi.

NGUVU YA JINA KWENYE BIASHARA YA MTU MMOJA.

Pamoja na kwamba utaendesha biashara yako mwenyewe, unahitaji kujenga jina lako kibiashara au jina la biashara yako. Unahitaji kujijengea sifa fulani ambapo mtu akisikia jina lako au jina la biashara yako, anajua kabisa nini anakwenda kupata. Unahitaji kuweka nguvu kubwa kwenye kujenga na kulinda jina lako kibiashara, hii ni silaha muhimu kwenye mafanikio yako. Inafika wakati watu wanafanya biashara na wewe kwa sababu ya jina lako, na siyo kwa sababu ya kile unachouza, kwa sababu huenda wanaweza kukipaka kwa wengine, lakini jina lako linawapa uhakika na imani zaidi.

KITU KIMOJA UNACHOHITAJI ILI KUENDESHA BIASHARA YAKO BILA YA MSONGO WA MAWAZO.

Kinachoua biashara nyingi zinazoendeshwa na mtu mmoja, ni msongo wa mawazo unaotokana na nitakula nini kesho. Wafanyabiashara wengi wadogo huwa hawana uhakika wa maisha, hivyo wanatoa fedha kwenye biashara zao changa kwa ajili ya kuendesha maisha, kama kupata chakula, kulipa kodi na gharama nyingine muhimu.

Ili uweze kuendesha na kukuza biashara yako vizuri, lazima akili yako iwe imetulia kwenye biashara hiyo. Na ili akili yako itulie kwenye biashara yako, unahitaji kuwa na uhakika wa kuendesha maisha yako bila ya kuondoa fedha kwenye biashara yako. Bila ya kuwa na kiasi cha fedha cha kuwezesha maisha yako kwenda bila ya kugusa fedha ya biashara, biashara itakufa.

NJIA NNE ZA KUPATA FEDHA ZA KUENDESHA MAISHA BILA YA KUGUSA BIASHARA YAKO.

Najua uliposoma hapo juu kwamba lazima uwe na fedha za kutosha kuendesha maisha yako bila kugusa biashara yako unaweza kuwa umeanza kuona labda wewe siyo wa kupita njia hii, kwa sababu huna fedha nyingi za kukuwezesha kuendesha maisha yako bila ya kugusa biashara yako.

Zipo njia nne unazoweza kutumia kupata fedha ya kuendesha maisha bila ya kugusa biashara yako.

Moja; kuanza biashara kama kitu cha pembeni. Hapa unakuwa na ajira ambayo inakuingizia kipato na biashara yako inakuwa kitu cha pembeni. Kwa njia hii unaweza kuendesha maisha yako kwa mshahara huku ukiendelea kukuza biashara yako.

Mbili; punguza sana gharama zako za maisha, hapa unachagua kuishi maisha magumu kwa kipindi ambacho unaanzisha na kukuza biashara yako. Matumizi yoyote ambayo siyo muhimu kabisa unaachana nayo. Kwa njia hii unaweka akiba itakayokuwezesha kuendesha maisha yako kwa miezi sita mpaka mwaka mmoja bila ya kugusa biashara yako.

Tatu; kupata watu wengine watakaowekeza kwenye biashara yako. Kama biashara unayotaka kuanzisha ni kubwa kuliko unavyoweza kuanza mwenyewe, unaweza kuwakaribisha watu wengine wakawekeza fedha zao na ukawapa sehemu ya umiliki wa biashara, lakini wewe ndiye unayeendesha biashara. Ukiwa na biashara unayoweza kuiendesha vizuri na ukawa na wawekezaji, itakuwa rahisi kwako kuweka juhudi kwenye kukuza biashara bila ya kujali kuhusu fedha.

Nne; tumia njia nyingine za kupata fedha kama kushiriki mashindano mbalimbali ya mawazo bora ya kibiashara. Kuna taasisi nyingi huwa zinaendesha mashindano ya watu kutoa mawazo bora ya kibiashara na wazo linaloshinda linafadhiliwa. Kama unaweza kulieleza wazo lako vizuri, kuchambua jinsi gani unawafikia wateja na jinsi gani unatengeneza faida, unaweza kushinda ufadhili na ukaweza kuendesha biashara yako vizuri.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA WAKATI UNAENDESHA BIASHARA YAKO MWENYEWE ILI IWEZE KUKUA ZAIDI.

Moja; endelea kujifunza na kuwa bora zaidi kila siku. Hutaweza kudumu kwenye biashara unayoendesha mwenyewe kama utafanya vitu kwa mazoea. Teknolojia inakua kila siku, kuna njia mpya za kurahisisha kazi zako zinagunduliwa kila siku. Unahitaji kuwa unajifunza ili uweze kupiga hatua.

Mbili; linda sana muda wako, usitumie muda wako hovyo, unahitaji kuweka vipaumbele vyako vizuri kwa kuhakikisha unafanya yale tu ambayo hayawezi kufanywa na watu wengine. Kuwa na makundi manne ya vitu, vitu unavyohitaji kufanya sasa, vitu unavyoweza kufanya baadaye, vitu ambavyo unaweza kuwapa wengine wakafanya na vitu ambavyo unapaswa kuacha kufanya kabisa. Kabla hujafanya kitu, angalia kwanza kinaenda kwenye kundi lipi ndipo ukiweke kwenye kundi husika.

Tatu; usisahau maono yako makubwa. Unapoanza biashara na ukawa na majukumu mengi, ni rahisi sahau maono yako makubwa na kumezwa na shughuli za biashara. Unahitaji kuendelea kujikumbusha ndoto yako kubwa. Hivyo kila siku asubuhi na kabla hujalala, jiumbushe ndoto yako kwa kuandika kila unachotaka kwenye maisha yako. Hii itakusaidia uendelee kuwa kwenye mstari sahihi wa kufika unakotaka kufika.

Nne; jifunze kusema hapana. Utakapoanza biashara yako, zitajitokeza fursa mbalimbali ambazo zitaonekana ni nzuri kuliko biashara unayokuwa umeanza. Wakati mwingine watu watakuja kwako na mawazo mengi yanayoonekana ni mazuri. Wapo watakaokuambia unapaswa kufanya hivi au kufanya vile. Mara zote jikumbushe ndoto yako kubwa na kama kitu hakichangii kufikia ndoto yako sema HAPANA, na usitake kumbembeleza yeyote.

Tano; weka mkazo kwenye biashara yako. Ili biashara yako ikue, unahitaji kuweka mkazo wa hali ya juu. Biashara yako inahitaji muda wako, itahitaji fedha na itahitaji nguvu. Lazima upunguze mambo yote yasiyo muhimu yanayotumia rasilimali hizo tatu ili uweze kuelekeza kwenye biashara yako. Ondokana na usumbufu na kelele zinazokutoa kwenye biashara yako.

Rafiki, hayo ndiyo muhimu sana unayopaswa kuyazingatia ili uweze kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa wewe mwenyewe. Mambo haya yanaweza kukusaidia hata kama una biashara iliyoajiri. Na pia baada ya kukuza biashara yako kwa kuanza mwenyewe, unaweza kuchagua mwenyewe kama unafurahia kuiendesha mwenyewe au unataka kuajiri wengine wakusaidie.

Kumbuka lengo lako kuu la kuingia kwenye biashara ni kupata uhuru kamili, hivyo fanya kile kinachokuweka wewe kwenye uhuru kamili unaotaka kwenye maisha yako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji