Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya ukomo ambao sisi binadamu tunao ni wa muda, kwamba muda wetu una ukomo na ndiyo maana hatuwezi kufanya kila tunachotaka kufanya. Ukomo mwingine ni nguvu, ambapo kadiri tunavyokwenda, nguvu zetu zinapungua na kushindwa kufanya yale tunayotaka kufanya.

Kuna ujumbe huwa watu wanapenda kuutumia sana kuhusu muda na nguvu.

Kwamba ukiwa kijana unakuwa na muda na nguvu, lakini unakuwa huna fedha na uzoefu. Ukiwa mtu mzima unakuwa na nguvu na fedha, lakini unakuwa huna muda. Na ukiwa mzee unakuwa na muda na uzoefu, lakini unakuwa huna nguvu.

Sasa ipo njia ya kukuwezesha wewe kuwa na muda na nguvu kipindi chote cha maisha yako, hata kama umri unakwenda, bado unaendelea kuwa na nguvu zako kama vile bado ni kijana. Unakuwa na muda wa kufanya yale muhimu, na pia nguvu za kufanya yale ambayo unayotaka kufanya kwenye maisha yako.

MIMI NI MSHINDI

Kuna vitu vitatu muhimu ambavyo ukivifanya utaweza kuwa na muda na nguvu kipindi chote cha maisha yako. Jifunze vitu hivi na chukua hatua ili maisha yako yawe bora.

Moja; kula nusu ya ulichozoea kula.

Watu wengi wanakula chakula mara mbili ya wanachopaswa kula, kwa kifupi watu wanakula chakula kingi mno, na hili linakuwa mzigo kwao.

Ukiwa mtu mzima, chakula kina kazi mbili kwenye mwili wako, kazi ya kwanza ni kuupa mwili nguvu, na kazi ya pili ni kusaidia mwili kujitengeneza kama una majeraha.

Unapokula chakula kingi kuliko uhitaji wa mwili, chakula hicho kinageuzwa na kuhifadhiwa kama mafuta, na hapa ndipo watu wanakuwa na uzito uliopitiliza. Uzito ukishakuwa mkubwa mwili unakosa nguvu ya kufanya shughuli zake vizuri. Pia uzito huo unakaribisha magonjwa kama ya shinikizo la damu, kisukari na saratani ambayo yanafanya mwili kuwa dhaifu na kushindwa kuchukua hatua.

Kula nusu ya chakula ambacho umezoa kula sasa. Hakuna kanuni yoyote kwamba kwa nini ule mara tatu kwa siku, tena chakula kingi na kizito. Kula pale unaposikia njaa na kula kiasi kidogo cha chakula. Kuliko ule mara tatu kwa siku, chakula kingi, chagua kula mara tano, vitu vidogo vidogo au kula mara mbili, mlo mmoja chakula kizito na mlo mwingine chakula kidogo.

Kwa vyovyote vile, punguza sana kiasi cha chakula unachokula, na sukari na wanga ndiyo sumu kubwa kwenye mwili wako, maana hivi ndivyo wengi huwa wanakula na vinakwenda kugeuzwa kuwa mafuta.

Kadiri umri unavyokwenda ndivyo mwili unahitaji chakula kidogo zaidi. Lakini wengi wamekuwa wanaendelea kula kama walivyokuwa wanakula wakiwa vijana wanaokua, wakati wameshafika umri wa utu uzima.

SOMA; Huo mnyororo shingoni kazi yake nini? (gharama ya uhuru unayopaswa kulipa ili kufanikiwa).

Mbili; pumua mara mbili ya unavyopumua sasa.

Watu wengi hawapumui kwa namna wanavyopaswa kupumua, labda ni kuulize lini ulikaa chini na kusema sasa wacha nipumue? Mara chache sana, muda mwingi umekuwa unapumua kwa mazoea, kwa sababu hewa inaingia na kutoka bila hata ya wewe kujua.

Kupumua ndiyo njia kuu ya mwili kupata hewa ya oksijeni ambayo inaenda kuunguza chakula kwenye seli na mwili unapata nguvu. Pia ndiyo njia ya kuondoa hewa ukaa ambayo unazalishwa wakati mwili unatengeneza nguvu kutoka kwenye chakula.

Usipopumua vizuri, mwili unashindwa kuunguza chakula na kupata nguvu, na pia hewa ya ukaa inajikusanya mwilini na inasababisha mwili kuchoka. Kama umewahi kufanya mazoezi makali, au hata kutembea sana kisha ukasikia misuli inakaza sana, ni kwa sababu misuli hiyo inakuwa imekosa hewa ya oksijeni na hivyo inatengeneza nguvu bila oksijeni na kinachozalishwa ni tindikali inayoleta maumivu.

Usipopumua vizuri, maana yake unaunyima mwili nguvu, na kibaya zaidi unauumiza mwili kwa kutokuondoa hewa isiyohitajika mwilini.

Kwa maisha yetu ya haraka, ambapo hatuna muda, kupumua ni kitu cha mwisho mtu yeyote kufikiria. Hivyo tumekuwa tunafanya kwa mazoea.

Unahitaji kupumua mara mbili ya unavyopumua sasa, unahitaji kuvuta hewa kwa kina na kwa muda mrefu, kisha kutoa hewa hiyo nje kwa kina na kwa muda pia. Unahitaji kuhesabu muda unaofanya hivyo, kuhakikisha mwili unapata pumzi za kutosha.

Na unapojikuta kwenye wakati mgumu, kabla hujafanya chochote, jipe dakika chache za kupumua kwa kina, kabla hujamaliza utakuwa umeshaanza kuona hatua za kuchukua.

Pumua kwa kina na mwili wako utakuwa na nguvu, akili yako itaweza kufikiri kwa usahihi na chakula ulichokula kitatumika vizuri.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE HEALING POWER OF MIND (Nguvu Ya Tahajudi Kwenye Afya, Uzima Na Uamsho)

Tatu; tumia uwezo mkubwa uliopo ndani yao.

Watu wengi wamekuwa wanakufa na uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yao. Walipokuwa watoto walikuwa wakiulizwa wanataka kuwa nani wanasema bila ya shaka, nataka kuwa msanii, nataka kuwa daktari, nataka kuwa mwandishi, nataka kuwa mfanyabiashara na kadhalika. Katikati hapo, wanakutana na mfumo wa elimu, ambao unawaambia yale walikuwa wanafikiria yalikuwa ni utoto. Uhalisia ni kusoma vizuri, kufaulu na kupata kazi ya kuajiriwa. Wanafuata hilo kwa adabu, wanamaliza masomo, wanafanya kazi na wanastaafu, kazi haikuwa inawafurahisha na ule uwezo mkubwa bado upo ndani yao. Wanakuja kustuka muda umekwenda, na wanaona hawawezi tena kuanza.

Rafiki yangu, leo hii jikumbushe kile ulichokuwa unataka kufanya na maisha yako ulipokuwa mtoto. Na kama huko ni mbali, kuwa mkweli na nafsi yako na jiambie sasa ni kitu gani unapenda sana kukifanya, hata kama hakuna mtu anayekulipa kwa kufanya.

Ukishajua kitu hicho, anza kukifanya sasa. Tafiti zinaonesha watu wanaofanya kile wanachopenda, wanaishi muda mrefu, na wanaugua mara chache ukilinganisha na wasiofanya wanachopenda.

Anza kutumia uwezo mkubwa ulipo ndani yako, fanya kile ambacho unakipenda hasa na kifanye kila siku, na kwa hakika utaishi muda mrefu, ukiwa na nguvu na hamasa ya kufanya zaidi.

Rafiki yangu, hayo ndiyo matatu muhimu ya kuzingatia sana ili uweze kuwa na muda na nguvu za ujana hata kama umri wako umekwenda. Kula nusu ya unachokula sasa, pumua mara mbili ya unavyopumua sasa na fanya kile unachopenda kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji