Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya vitu vinavyowazuia watu wengi kupata mafanikio makubwa, ni kukosa falsafa wanazoziishi kwenye maisha yao. Watu wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kama bendera inayofuata upepo. Wanafanya kile ambacho wengine wanafanya, hata kama hakina maana kwao.

Jim Rohn alikuwa mwandishi na mhamasishaji ambaye kwa zaidi ya miaka 40 alikuwa akifundisha watu jinsi ya kujenga falsafa za maisha yao. Jim alianza maisha kama kijana wa kijijini, ambaye kazi pekee aliyokuwa anajua ni kukamua ng’ombe, baadaye alipata kazi ya kuajiriwa, lakini alikuja kugundua falsafa ambayo ilimfanya asikae kwenye kazi ile kwa muda mrefu.

Kwenye makala hii ya leo nakwenda kukushirikisha falsafa 10 za Jim Rhon ambazo kama utazielewa na kuanza kuziishi leo, utaweza kupata mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako. karibu tujifunze na uchukue hatua ili kufanikiwa.

  1. Faida ni bora kuliko mshahara.

Jim Rhon anasema; “profits are better than wages, wages make you are life, profit make you a fortune.”

Akimaanisha faida ni bora kuliko mshahara, mshahara utakupa fedha ya kuendesha maisha pekee, lakini faida inakupa mafanikio makubwa.

Jim anatuambia kwamba hii ndiyo falsafa iliyobadili kabisa maisha yake, akaweza kuondoka kwenye ajira na kuingia kwenye biashara.

Ukiangalia huu ni ukweli usiopingika, hata mshahara uwe mkubwa kiasi gani, huwa unaishia tu kuendesha maisha. Ndiyo maana mwisho wa mwezi ila mfanyakazi anayetegemea mshahara huwa umeshaisha, hata kama analipwa mshahara mkubwa kiasi gani.

Rhon anatuambia, kama umeajiriwa, basi unahitaji kuwa na kitu cha pembeni ambacho kinakuzalishia faida. Na faida ya kitu cha pembeni ikishazidi na kuwa mara mbili ya mshahara wako, unaweza kuachana kabisa na ajira yako.

Na hapa ndipo nimekuwa nakusisitiza sana kuhusu BIASHARA NDANI YA AJIRA, kwamba kama umeajiriwa na huna biashara yoyote, yaani kipato chako pekee ni mshahara, basi umejiweka kwenye hatari kubwa sana. Soma kitabu nilichoandika cha BIASHARA NDANI YA AJIRA na kitakusaidia sana.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

  1. Usitake urahisi, kuwa mgumu.

Jim anatuambia; “Don’t wish it was easier, wish you were better. Don’t wish for less problems, wish for more skills. Don’t wish for less challenge, wish for more wisdom.”

Akimaanisha usitamani ingekuwa rahisi, tamani kuwa bora, usitake matatizo kidogo, taka ujuzi zaidi, usitake changamoto chache, taka kuwa na hekima zaidi.

Kitu pekee kitakachokuwezesha kufanikiwa kwenye haya maisha siyo kupata urahisi, maana maisha hayatakuwa rahisi, bali wewe kuwa mgumu, maana kila wakati utakutana na ugumu. Usije ukajidanganya kwamba ukiondoka pale ulipo sasa, ambapo unaona ni pagumu, utaweza kwenda pengine ambapo ni rahisi. Kila sehemu itakuwa ngumu kama wewe mwenyewe hutakuwa mgumu.

Mafanikio kwenye maisha ni uwezo wako wa kupambana na changamoto, kuvuka magumu na kutokukata tamaa, maana utakutana na ugumu wa kila aina, ila kama utakuwa mgumu, basi utadumu.

SOMA; Wewe Siyo Wa Kwanza Kupitia Magumu Unayopitia, Haupo Mwenyewe, Amka Na Endelea Na Mapambano.

  1. Usipoteze hata siku moja, ni ghali mno kwako.

Jim anatuambia; “Days are expensive. When you spend a day you have one less day to spend. So make sure you spend each one wisely.”

Akimaanisha siku ni ghali sana, unapotumia siku yako moja, maana yake umepunguza siku moja kwenye maisha yako. Hivyo tumia siku zako kwa umakini mkubwa.

Kuna watu muda kwao ni kitu kisicho na thamani yoyote. Yaani mtu anaweza kupoteza muda wake kwa kufanya vitu ambavyo havina umuhimu kabisa, havihusiani kabisa na maisha yake kuwa bora.

Huwa tunajisahau na kufikiri tutaishi hapa duniani milele, lakini siku zetu zinahesabika. Hivyo chukulia kila siku inayopita kama siku unayokaribia kifo chako, na usikubali kabisa kupoteza hata siku moja, usikubali kupoteza saa nzima hufanyi kitu cha maana, na hata kila dakika yako, hesabu yapi muhimu unayofanya yanayokupeleka kwenye mafanikio yako makubwa.

Muda ni ghali sana, usiuchezee na kuupoteza hovyo.

  1. Uongozi ni mgumu na una changamoto.

Jim anasema; “The challenge of leadership is to be strong, but not rude; be kind, but not weak; be bold, but not a bully; be thoughtful, but not lazy; be humble, but not timid; be proud, but not arrogant; have humor, but without folly.”

Akimaanisha, changamoto ya uongozi ni kuwa imara lakini siyo katili, kuwa mwema lakini siyo dhaifu, kuwa na jasiri lakini siyo mnyanyasaji, kuwa mtu wa kufikiri lakini siyo mvivu, kuwa mnyenyekevu lakini siyo mwoga, kuwa na fahari lakini siyo kiburi, kuwa mcheshi lakini siyo mpumbavu.

Kwa kifupi, uongozi ni mgumu, kwa sababu unahitaji kuwa mahali fulani ambapo ni katikati, usiwe juu sana na wala usiwe chini sana. Kwa sababu hakuna kazi ngumu kama kuwaongoza watu, na ni ngumu kwa sababu watu wanaendeshwa na hisia na siyo fikra. Kama watu wangekuwa wanaendeshwa na fikra, ingekuwa rahisi sana kuwaongoza.

Angalia viongozi wote wanaoshindwa, utaona kabisa kwamba wanaenda kinyume na falsafa hii ya Jim Rhon. Rudia tena kusoma sifa hizo za uongozi na ziishi kwenye maisha yako, maana hutafanikiwa kama hutakuwa kiongozi bora.

  1. Maisha ni maumivu, huwezi kukwepa.

Jim anatuambia; “We must all suffer one of two things: the pain of discipline or the pain of regret.”

Akimaanisha kila mmoja wetu lazima ataumia na kimoja kati ya hivi viwili; maumivu ya nidhamu au maumivu ya majuto.

Iko hivi, ili kupata chochote kwenye maisha yako, unahitaji nidhamu ya hali ya juu sana. Na nidhamu, kwa maneno ya kawaida tu tuseme ni kujitesa, maana itabidi uikatalie vitu vizuri ulivyozoea ili kupata kile unachotaka. Sasa wengi hawapendi maumivu ya nidhamu, wanajiambia kabisa hawawezi kujitesa.

Ambacho wanakuwa hawajajua ni kwamba, kwa kukataa maumivu ya nidhamu, wanajipeleka wenyewe kwenye maumivu ya majuto. Kwamba maisha yao yote wataumia kwa majuto kwa nini hawakuchukua hatua fulani na maisha yao yangekuwa bora zaidi. Ubaya wa maumivu ya majuto ni kwamba utaenda nayo maisha yako yote.

Amua leo ni maumivu gani unayataka, ya nidhamu au ya majuto, na usijidanganye kwamba unaweza kukwepa maumivu kwenye haya maisha, hicho kitu hakipo.

  1. Hamasa pekee haitoshi, tabia ni muhimu.

Jim anatuambia; “Motivation is what gets you started. Habit is what keeps you going.”

Akimaanisha, hamasa ndiyo inayokusukuma kuanza, tabia ndiyo itakayokuwezesha kuendelea.

Hakuna ukweli kama huu, hasa kwangu ambaye nimepata bahati ya kuwakochi watu wengi, nimekuwa naona hili kila siku. Mtu anapata mafunzo ninayotoa, anahamasika sana na kusema maisha yangu lazima yabadilike, lakini baada ya siku chache unakuta ile hamasa imeshapoa na wamerudi kwenye mazoea.

Unapochunguza unagundua hamasa ilikuwepo, tena kubwa, lakini tabia zilibaki zile za awali. Ili ufanikiwe, lazima uzijue na kuziishi tabia za mafanikio, kama ambavyo waliofanikiwa wanaishi. Wengi hukimbilia kupata hamasa, lakini hawapo tayari kubadili tabia, kwa sababu hawataki maumivu ya nidhamu, mwishowe wanabaki na maumivu ya majuto.

Jijengee tabia za mafanikio na ishi hizo wakati wote, hilo litakuwezesha kufanikiwa zaidi kuliko kuwa na hamasa pekee.

  1. Mwili wako ni hekalu takatifu.

Jim anasema; “Take care of your body. It’s the only place you have to live.”

Akimaanisha utunze sana mwili wako, ndiyo sehemu pekee unayoishi.

Watu wengi wamekuwa wanachukulia miili yao kama majalala, ambapo kila uchafu unaingia, hakuna kuchagua. Hili ndiyo linapelekea wengi kuwa na maisha ya hovyo, kusumbuka na maradhi na hata kufa wakiwa na umri mdogo.

Rafiki yangu, ili ufanikiwe, uchukulie mwili wako kama hekalu takatifu ambalo hakuna uchafu wa ana yoyote unaoweza kuingia. Kwa kufanya hivi utautunza mwili wako na wenyewe utakuwezesha kufanikiwa sana. Huwezi kufanikiwa kama huna afya imara.

Uchafu unaoweka kwenye mwili wako ni vyakula vya hovyo, vilevi vya aina yoyote ile, habari na taarifa hasi. Vyote hivi vinavyoofisha mwili na kukuzuia wewe kufanikiwa. Weka mwili wako safi, afya yako itakuwa imara na mafanikio yatakuwa yako.

SOMA; Fanya Vitu Hivi Vitatu (03) Na Utaendelea Kuwa Na Ujana Ndani Yako Licha Ya Umri Kwenda.

  1. Elimu ya darasani haitakupa mafanikio makubwa.

Jim anasema; “Formal education will make you a living; self-education will make you a fortune.”

Akimaanisha; elimu ya darasani itakupa maisha, elimu binafsi itakupa mafanikio makubwa. Watu wengi huwa wanaacha kujifunza pale wanapohitimu masomo, na hili ndiyo kosa linalowapoteza kabia kwenye maisha yao. Elimu ya darasani inakuwezesha kupata kazi ya kawaida, ambayo itakupa maisha ya kawaida.

Ili kufanikiwa zaidi, unahitaji kujifunza wewe mwenyewe zaidi kwenye yale maeneo muhimu kwako. Lazima kila siku ujifunze na kuwa bora zaidi ndiyo utaweza kufanikiwa. Kama umeacha kujifunza kwa sababu umemaliza shule, unajiweka mbali na mafanikio makubwa.

  1. Usipopanga maisha yako, watu watakupanga.

Jim anatuambia; “If you don’t design your own life plan, chances are you’ll fall into someone else’s plan. And guess what they have planned for you? Not much.”

Akimaanisha, kama hutatengeneza mpango wa maisha yako, utaishia kwenye mipango ya maisha ya wengine. Na unafikiri watu watakuwa wamekupangia nini? Siyo makubwa.

Kama unataka kufanikiwa, lazima uwe na mpango wa maisha yako, lazima uwe na mpango wa mafanikio unaoufanyia kazi kila siku. Kama huna mpango wa aina hiyo, utaishia kuwa ndani ya mipango ya wengine, na hakuna anayeweza kukupangia wewe mafanikio makubwa.

Kwa maneno mengine, kama hujui jinsi ya kutumia vizuri muda wako, watu watauchukua ha kuutumia, kama hujui utumieje nguvu zako, wengine watazitumia. Maisha ni kujipanga au utapangwa. Na huwezi kufanikiwa kama unapangwa na wengine.

  1. Kama kuna kitu hukipendi kibadili, wewe siyo mti.

Jim anatuambia; “If you don’t like how things are, change it! You’re not a tree.”

Akimaanisha kama hupendi jinsi vitu vilivyo, vibadili, wewe siyo mti.

Unaweza ukashangaa jinsi watu wanavyolalamikia vitu ambavyo hawavipendi. Labda ni aina ya maisha wanayoishi, labda ni mazingira waliyopo, labda ni kazi walizonazo au hata biashara wanazofanya. Watu wanajidanganya kabisa isingekuwa vitu fulani basi wangefanikiwa.

Huo ni uongo, kama ambavyo Jim Rhon anatuambia kama kuna kitu hukipendi kibadili, usiiishie tu kukilalamikia na kuendelea nacho, wewe siyo mti kwamba inabidi ukae hapo ulipo. Chukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi, kwa kwenda kule ambapo ni muhimu zaidi, kwa kufanya yale ambayo yana maana kwako zaidi. Usiwe mtu wa kulalamika, kulalaika hakutakusaidia lolote.

Rafiki, hizi ndiyo falsafa kumi za Jim Rhon ambazo kama utaanza kuzifanyia kazi leo, na kuziishi maisha yako yote, basi utapiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Kumbuka hakuna chochote au yeyote anayekuzuia wewe kufanikiwa ila wewe mwenyewe. Chagua na tengeneza falsafa ya maisha yako ya nafanikio utakayoiishi kila siku na hutabaki pale ulipo sasa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji