Rafiki yangu mpendwa,

Hivi unaona jinsi ambavyo haya majuma ya mwaka 2018 yanavyokwenda kasi? Kama huoni yakienda kasi, basi huenda kuna shida kubwa upande wako. Inawezekana hakuna makubwa unayofanya na hivyo unaona kama siku haziendi kabisa.

Lakini pale unapokuwa na makubwa unayofanyia kazi, pale unapokuwa na kila saa na dakika ya siku yako umeipangia kazi, pale unapofanya kazi masaa 14, 16 na hata 18 kwa siku, muda siyo tu unakimbia, bali unapaa.

Lakini kama una muda wa kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, kama una muda wa kusoma, kusikiliza na kuangalia habari, kama una muda wa kubishana timu ipi ni bora, msanii yupi ni bora au chama kipi cha siasa ni kizuri, lazima utaona muda wako ni mwingi sana, na ndiyo maana unaupoteza.

Karibu tena kwenye TANO ZA JUMA, mkusanyiko wa mambo makubwa matano niliyojifunza juma hili na ambayo wewe pia rafiki yangu unaweza kujifunza na kama utachukua hatua basi maisha yako yatakuwa bora sana.

Rafiki, nikukumbushe zaidi kwamba mipango mizuri ya kufanyia kazi, na kipindi kizuri cha kujifanyia tathmini ni juma moja. Unaweza kuzipangilia vizuri siku zako saba za wiki, masaa yako 168 na mwisho wa juma ukapata muda wa kutafakari kila siku iliendaje na kila saa iliendaje.

Hivyo leo hii, kama siku haijaisha, pata muda wa kujitafakari kwa juma unalomaliza, na pia panga mambo unayokwenda kufanyia kazi juma namba 30 tunalokwenda kuanza. Usikubali kupoteza juma lako kwa kuanza juma  bila ya mipangilio, na usikubali kupoteza siku yako kwa kuanza siku bila ya kuipangilia vizuri. Na inapokuja kwenye masaa ya siku, hakikisha unatumia kila saa kufanya yale yaliyo muhimu kwako kufikia ndoto kubwa za maisha yako.

Rafiki, karibu kwenye tano za juma hili namba 29, juma lililokuwa bora sana, jifunze na panga kuchukua hatua ili maisha yako yawe bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; NGUVU YA UBISHI KWENYE MAFANIKIO MAKUBWA.

Juma hili nimefanikiwa kusoma vitabu vinne, lakini kitabu kimoja kimenisukuma sana. Kabla sijakuambia kuhusu kitabu hichi, nikupe siri moja ambayo huwa naitumia kuchagua kitabu gani nisome. Kwanza huwa nasoma sifa za kitabu kwa wale ambao wanakuwa wameandika sifa kwenye kitabu hicho, kisha huwa nasoma dibaji na shukrani, kisha nasoma sura zilizopo kwenye kitabu hicho, halafu nachagua kufungua ukurasa wowote wa kitabu na kusoma aya yoyote na kujiuliza kama kuna kitu cha kufanyia kazi nimeondoka nacho.

Sasa juma hili, kwenye moja ya vitabu tulivyokuwa tunasoma kwenye kundi letu la usomaji wa vitabu ni kitabu THE POWER OF RELENTLESS; 7 SECRETS TO ACHIEVING MEGA-SUCCESS, FINANCIAL FREEDOM AND LIFE OF YOUR DREAMS kilichoandikwa na Wayne Root. Nianze kwa kusema, baada ya kuwa nimesoma vitabu vingi kuhusu mafanikio, nimekuwa naona ujumbe ni ule ule lakini unasemwa kwa lugha tofauti. Na nimekuwa nasema kwamba, kitabu cha msingi kabisa kwenye mafanikio ni THINK AND GROW RICH, na kitabu muhimu kabisa kwenye fedha ni THE RICHEST MAN IN BABYLON na kitabu bora kabisa kwenye ujasiriamali ni RICH DAD POOR DAD. Niliwahi kusema siku za nyuma, kama utasoma vitabu hivyo vitatu tu, na kufanyia kazi kila unachojifunza kwenye vitabu hivyo, utapata mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.

power of relentless

Sasa nilipoanza kukikaga kitabu THE POWER OF RELETNLESS, au kama tunavyoweza kusema kwa kiswahili NGUVU YA UBISHI, niliona ni kitabu cha tofauti kabisa kuhusu mafanikio. Kwa sababu kimekuwa siyo kitabu kuhusu mafanikio, bali hadithi ya mtu mbishi kuliko mtu yeyote ambaye nimewahi kumsikia. Mtu mbishi na msumbufu, ambaye akisikia neno HAPANA ndiyo kama linamhamasisha. Mtu akimwambia hapana ni sawa na amemwambia rudia tena, na atarudia mpaka apate anachotaka. Na kwa mifano, ameonesha jinsi gani ameweza kupata kila alichowahi kutaka kwenye maisha yake, licha ya kuambiwa haiwezekani.

Mtu huyu ni Wyne Root, ambaye huwezi kumwelezea kwa neno moja, kwa sababu ni mtangazaji wa tv, mbashiri wa michezo, mwanasiasa aliyegombea uraisi, mjasiriamali, mwandishi na mhamasishaji. Kwenye uandishi pekee ameandika vitabu kumi, ambavyo vyote vimeuza sana.

Kwenye kitabu hichi cha NGUVU YA UBISHI, Wayne anatushirikisha jinsi nguvu ya ubishi ilivyoweza kuyabadili maisha yake na jinsi inavyoweza kuyabadili maisha yako pia.

Wayne ametushirikisha MISINGI SABA ya kutuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana licha ya kila mtu kusema haiwezekani. Na katika kila msingi, Wayne anatushirikisha mfano wake binafsi wa jinsi alivyoweza kutumia msingi huo kupata mafanikio makubwa.

Kabla sijakushirikisha misingi hii saba, niseme kitabu hichi ni moja ya vitabu vilivyonisukuma sana, na kunifanya nione pamoja na kuwa na ndoto kubwa sana, lakini hatua ninazochukua bado sana. Nimekuwa nafikiri nachukua hatua kubwa, nimekuwa nafikiri muda wangu umebana sana, lakini baada ya kusoma mifano ya jinsi Wayne anavyojisukuma, nimejifunza naweza kufanya zaidi ya ninavyofanya sasa, yaani zaidi mno.

Karibu kwenye misingi saba ya ubishi ya kukuwezesha kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Msingi wa kwanza; ubishi wa moyo.

Wayne anatuambia msingi wa kwanza kabisa wa mafanikio makubwa ni kuwa na ubishi wa moyo. Wayne anasema hata kama uwe na akili kiasi gani, kama huna moyo mgumu, kama huna moyo ambao haukati tamaa, hutaweza kufanikiwa. Wayne anasema mioyo yetu ina uwezo mkubwa kuliko hata akili zetu. Kama mioyo yetu itakubali kitu, hakuna kinachoweza kutuzuia.

Msingi wa pili;ubishi wa ung’ang’anizi.

Hapa Wayne anatuambia kama hutakuwa king’ang’anizi, hutaweza kupata chochote kikubwa kwenye maisha yako. Kwa sababu pale tu utakapotamka kwamba unataka makubwa kwenye maisha yako, kila kitu kitaibuka kukupinga, kukuzia usipate unachotaka.

Wayne anasema utashindwa na kuanguka, wazoefu na wataalamu watakuambia unachotaka hakiwezekani, na hapo ndiyo unahitaji kuwa na hasira zaidi, kuwaonesha kwamba siyo tu inawezekana, bali inawezekana kwa mafanikio makubwa.

Wayne anasema inabidi uwe mbishi kiasi kwamba watu inabidi wakukubalie ili uache kuwasumbua. Yaani uwe king’ang’anizi mpaka mtu aone njia pekee ya wewe kuacha kuwasumbua ni wakubaliane na wewe. Na wakishakubaliana na wewe, usifanye makosa, wafanye wajione walichelewa kukubaliana na ulichokuwa unataka kwao.

Msingi wa tatu; ubishi kwenye kuweka malengo.

Wayne anasema kama hutaweka malengo makubwa, malengo ambayo kila anayeyasikia anashtuka na kukuambia hapana, usiweke malengo makubwa hivyo, utashindwa na itakuumiza, basi jua hutaweza kufikia mafanikio makubwa.

Wayne anasema, lenga kwenye kufikia nyota za juu kabisa, na hata kama hutafikia, basi utaishia kwenye mwezi. Lakini kama utalenga kwenye mwezi, unafikiri utaishia wapi?

Wayne anatuambia tunapaswa kuweka malengo makubwa sana, kisha kuweka muda wetu na nguvu zetu zote kuyafikia. Kwa mfano anasema chochote unachochagua kufanya, basi kazana kukifanya kwa ubora sana, kufika ngazi ya juu kabisa, kuwa namba moja, kutawala. Usitake kuwa kawaida, maana utapotea kabisa.

Msingi wa nne; ubishi kwenye maandalizi.

Wayne anasema watu wengi wanapata shida ya kufikia malengo yao makubwa, kwa sababu hawana maandalizi kabisa. Yaani kile ambacho watu wanasema wanafanya maandalizi, hakuna wanachofanya, wanajiliwaza tu.

Kwa mfano Wayne ana dhana anaiita KUJAZA BOMBA lako la fursa. Hapa Wayne anasema kwamba watu wengi hawana fedha kwa sababu bomba la fursa walilonalo halijajaa vya kutosha, yaani lipo tupu. Anasema kila mtu anapaswa kuwa anajaza bomba lake la fursa kila siku.

Kwa mfano unakuta mtu ana biashara, na wateja wake ni wale wale. Mteja mmoja akiacha kununua basi kipato chao kishashuka. Wayne anasema biashara kama hiyo ni bomba la fursa, na kazi yako kama mfanyabiashara ni kila siku kuwa unawafikia wateja wapya. Kiasi kwamba mteja mmoja akicha kununua leo, kuna watatu wapya wanaonunua.

Wayne pia anasema usijaribu kuendesha maisha ukiwa na chanzo kimoja cha kipato pekee, ni hatari kubwa mno kwenye maisha ya sasa. Jaza bomba lako la fursa, na mara zote kuwa na njia mbadala za kuingiza kipato, na zifanyie kazi kila siku.

Msingi wa tano; ubishi kwenye kujijengea jina.

Wayne anatuambia inachowazuia watu wengi kufanikiwa ni kutokujulikana. Kama watu hawakujui, hawawezi kununua kile ambacho unauza, kama watu hawakujui, ni sawa na haupo kabisa hapa duniani.

Hivyo ili ufanikiwe sana, unahitaji kujenga jina lako, na jina la biashara au huduma unazotoa. Kiasi kwamba mtu akisikia jina lako au biashara yako hajiulizi hivi huyu anajihusisha na nini. Bali anajua kwa hakika unajihusisha na nini na anajua kwako anapata nini.

Kwa kujijengea jina, unaweza kuwafikia wengi na pia unajenga uaminifu wako kwa wengine. Hata watu ambao hawajawahi kukutana na wewe, wanakuamini kupitia jina lako.

Msingi wa sita; ubishi kwenye kusimulia hadithi.

Wayne hapa amenifundisha kitu kimoja muhimu sana, ambacho sitakisahau maisha yangu yote. Wayne anasema ukweli unaeleza, hadithi zinauza (FACTS TELL, STORIES SELL). Huu ni ukweli ambao mtu yeyote aliye hai, na mwenye malengo makubwa kwenye maisha yake, anapasa kuuelewa.

Watu hawanunui kwa sababu umewaeleza ukweli wa unachouza, watu wananunua kwa sababu ya hadithi unayowaeleza, ya jinsi unachowauzia kitakavyofanya maisha yao kuwa bora, kwa kutumia mifano hai. Wayne anasema tunahitaji kueleza hadithi kama tunataka kuwashawishi watu kununua chochote.

Na kwa uhalisia, sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, ambao tangu enzi na enzi, hadithi imekuwa sehemu kubwa ya kufundisha, kuonya na hata kurithishana maarifa na maadili muhimu. Wayne anatoa mfano wa Biblia, kitabu ambacho kimesomwa na watu wengi zaidi duniani, ukiangalia Biblia ni mkusanyiko wa hadithi.

Watu wanakumbuka hadithi zaidi, wanajihusisha na hadithi zaidi kuliko ukweli au taarifa zinazoelezea kitu.

Hivyo nikukumbushe tena, kama unataka kuuza, simulia hadithi.

Wayne hapa amenifundisha kitu kingine muhimu sana, ameeleza nguvu ya video katika kusambaza hadithi na kuwashawishi watu kuchukua hatua. Wayne anasema kwenye kila kitu ambacho watu walimkatalia, alirekodi video yenye ushawishi kwa nini watu wanapaswa kumkubalia na baada ya watu kuangalia video hizi, basi walikubali mara moja. Kila unapoweza, tengeneza video za ewe kueleza hadithi na ushawishi kwa chochote unachouza, itakuwa rahisi kwako kuwauzia wengi zaidi.

Msingi wa saba; ubishi wa kuchukua hatua kubwa sana.

Wayne anatuambia, fursa haitakufuata ulipo, fursa haitaonekana kwa urahisi, fursa inapaswa kusakanywa, inapaswa kuwinda, inapaswa kuangushwa na kisha kupelekwa nyumbani, kama ambavyo mtu anakwenda kuwinda mnyama porini, siyo kazi rahisi.

Yaani kama kwa namna yoyote ile unafikiri utakaa tu na vitu vitaenda sawa, unajidanganya sana, labda kama unachotaka ni kusukuma maisha tu, hapo huhitaji kupambana. Lakini kama unataka makubwa, kama unataka kutoka ulipo sasa na kufika mbali zaidi, lazima upambane sana.

Lazima uweke sababu pembeni, lazima uache kuhesabu muda, na kujiambia kama ni muda wa kazi au muda wa kupumzika. Lazima ujitoe sana, na lazima unachofanya kiwe muhimu na kiwe na maana kwako, maana la sivyo utajiona kama huna maisha.

Maisha yako ni ile alama unayoicha baada ya kuwa umejitoa sana. Angalia ni watu gani ambao tunawakumbuka leo, je wale ambao waliishi maisha ya kawaida au maisha yasiyo ya kawaida? Wewe jitajie tu jina la kila unayemjua leo na unajifunza kwake, kuanzia wanafalsafa, viongozi wa kidini na hata viongozi wa kiserikali, matajiri na wagunduzi wakubwa. Wote waliyatoa maisha yao kwa ajili ya kile ambacho waliamini ni sahihi na waliweza kuwasaidia wengi. Kama wewe ni mkristo, unajua Yesu aliweza kuwaokoa wengi, lakini iligharimu maisha yake. Hivyo usijidanganye kwamba ni rahisi, ni ngumu na unahitaji kujitoa sana.

Kama nilivyokuambia rafiki yangu, hichi ni kitabu ambacho kimenifanya nifikiri mara mbili juu ya hatua ninazochukua, kwa sababu kwa niliyoona Wayne anafanya, nahitaji kupiga hatua zaidi na zaidi. Siyo kwa sababu nataka kushindana naye, siyo kwa sababu namwonea wivu ila kwa sababu amenionesha inawezekana, na mimi sina sababu kwa nini isiwezekane.

Rafiki, jifunze misingi hii saba, angalia unaitumiaje kwenye kila unachofanya na anza kufanyia kazi sasa. Na eneo ambalo kila mmoja wetu anapaswa kufanyia kazi ni kwenye mauzo. Kila mtu anapaswa kuuza na kila siku unapaswa kuongeza mteja mpya kwenye mauzo yako.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

#2 MAKALA YA WIKI; FAIDA NI BORA KULIKO MSHAHARA.

kwenye makala ya wiki hii, nimekushirikisha falsafa kumi za aliyekuwa mwandishi na mhamasishaji wa mafanikio Jim Rhon, falsafa ambazo yeye mwenyewe anasema zilibadili maisha yake, na falsafa ambazo kama utazifanyia kazi pia zitabadili maisha yako sana.

Moja ya falsafa zake, ambayo anasema ilimnufaisha sana ni pale alipojua kwamba faida ni bora kuliko mshahara, na hivyo kuanza biashara ya pembeni licha ya kuwa alikuwa kwenye ajira.

Soma falsafa hizi kumi na zifanyie kazi ili maisha yako yawe bora zaidi. Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Faida Ni Bora Kuliko Mshahara; Falsafa Kumi (10) Za Jim Rhon Zitakazokuwezesha Kupata Mafanikio Makubwa Sana. (https://amkamtanzania.com/2018/07/19/faida-ni-bora-kuliko-mshahara-falsafa-kumi-10-za-jim-rhon-zitakazokuwezesha-kupata-mafanikio-makubwa-sana/)

#3 TUONGEE PESA; PESA INA WIVU.

Rafiki, pesa ni sawa na mpenzi mwenye wivu sana, mpenzi ambaye anataka muda wote uwe naye, muda wote ufikirie kuhusu yeye. Na inapotokea unatoa muda wako kwa vitu vingine, mpenzi huyo wala hafikirii mara mbili, anakuacha na kwenda kwa wale wanaompa muda wake.

Hivi ndivyo pesa ilivyo, pesa inaenda kwa wale ambao wanaijali, wale ambao wanajua jinsi ya kuitumia, wale ambao wanailinda muda wote na kwao inajisikia kuwa salama.

Mtu mmoja aliwahi kusema, ukichukua fedha zote duniani, ukazigawa sawa sawa kwa kila mtu duniani, baada ya muda mfupi fedha zote zitakuwa zimerudi kwa wale matajiri wakubwa. Kwa sababu matajiri hao wanaujua mchezo wa fedha, wanajua jinsi ya kuzivutia fedha na kuzifanya zisiondoke.

Rafiki, usikazane sana na fedha, bali kazana na ile saikolojia ya fedha. Mtu mmoja aliwahi kusema watu hawana shida ya fedha, ila watu wana shida ya mawazo yanayoweza kuwapatia fedha na kuzikusanya kwao zaidi. Anasema kama fedha ingekuwa shida, basi wezi wasingekuwa wanahitaji kuiba tena na tena.

Rafiki, ninachotaka kukukumbusha ni kimoja, tengeneza mfumo ambao utaifanya fedha iwe rafiki kwako, fedha ikujali kwa sababu unaijali. Na ni rahisi kufanya hivyo iwapo kila fedha unayopokea, cha kwanza unachofanya ni kuweka pembeni fedha ambayo utaizalisha zaidi kabla hata hujatumia. Lakini kama wewe utapata fedha na kinachoanza ni matumizi, fedha zitaendelea kutengana na wewe, maana huzijali.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KAMA UNATAKA ZAIDI, NJOO KWENYE KISIMA CHA MAARIFA.

Rafiki, pamoja na mafunzo ambayo nimekuwa natoa bure kupitia mtandao wa AMKA MTANZANIA, wapo watu wengi ambao wamekuwa wananiandikia ujumbe au barua pepe wakihitaji ushauri wangu kwenye mambo mbalimbali ambayo wamekwama. Na mara zote ninapoangalia yale waliyokwama ni mambo ambayo kama wangekuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA yangekuwa rahisi sana kwao. Lakini wanateseka kwa sababu hawapo kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Hivyo rafiki yangu, kama umekuwa unasoma kazi zangu, lakini bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, nakuambia kwamba hujitendei haki. Kwa sababu kuna maarifa mengi zaidi ambayo unayakosa, ambayo kwa kuyafanyia kazi utapiga hatua kubwa zaidi na utaondokana na changamoto nyingi zinazokuzuia kufanikiwa sasa.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, nitumie ujumbe kwenye wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na nitakupa maelekezo ya kujiunga.

#5; TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KITU KIBAYA KULIKO KUSHINDWA.

“It is hard to fail, but it is worse never to have tried to succeed.” – Theodore Roosevelt

Watu wengi hufikiri kitu kibaya kabisa kwenye maisha ni kushindwa, lakini hicho siyo kitu kibaya. Kwanza kabisa kushindwa ni kitu kizuri, maana unaposhindwa maana yake unakuwa umejifunza njia isiyo sahihi, na hivyo unaweza kujaribu tena kwa njia ambayo ni sahihi zaidi.

Kitu kibaya kuliko kushindwa ni kutokujaribu kabisa. Kwa sababu unakuwa hata hujajifunza, yaani unakuwa umeshinda, na hujui hata kwa ni nini umeshindwa, hivyo hakuna msaada wowote unaoweza kukusaidia kwenye hali kama hiyo.

Chochote unachotaka rafiki, jaribu, jaribu na kuwa tayari kushindwa. Maana kupitia kushindwa utajifunza zaidi kuliko usipojaribu kabisa. Furahia pale unaposhindwa, kwa sababu kwa uhalisia hujashindwa, ila umejifunza njia isiyo sahihi ya kufanya. Kwa lugha nyingine, una nafasi ya kufanya kilicho sahihi na ukafanikiwa zaidi.

Rafiki, hizo ndiyo tano za juma namba 29, juma ambalo lilikuwa bora sana kwetu, juma ambalo linatuacha, linatukabidhi kwa juma namba 30 ambalo juhudi zetu ndiyo zitakazoleta matokeo tofauti kabisa.

Naamini unakwenda kuanza juma namba 30 ukiwa na nguvu ya UBISHI na UNG’ANG’ANIZI ambao hakuna yeyote anayeweza kukuzuia. Maana kama kuna anayeweza kukuzuia, itakuwa vigumu kwako kufanikiwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji