Rafiki yangu mpendwa,

Kwa kipindi ambacho nimepata nafasi ya kufanya kazi na watu kwa karibu kwa kuwashauri na kuwakochi ili kuwa bora zaidi na kufanikiwa zaidi, nimejifunza kitu kimoja kutoka kwa wengi.

Watu wengi wanaposhawishika kuchukua hatua ya kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi, huwa wanajisahaulisha uhalisia wa maisha na sheria za asili. Huwa wanaingia kwenye kitu kipya wanachofanya wakiamini ni rahisi na ndiyo kitawapatia kila wanachotaka.

Nadhani imewahi kutoka kwako au kwa mtu unayemjua, ambaye alitoka kazi moja akilalamikia ni mbaya na kwenda kwenye kazi nyingine akiwa na matumaini makubwa. Au kutoka kwenye biashara moja ambayo mtu anailalamikia na kwenda kwenye biashara nyingine. Inawezekana pia ni mtu kutoka kwenye aina moja ya mahusiano na kwenda kwenye aina nyingine.

Maisha Hayajawahi

Watu wanapokuwa wanatoka kwenye kile walichozoea, na kwenda kwenye kitu kipya, huwa wanaweka matumaini makubwa sana kwenye kitu hicho kipya. Ni mpaka wanapoanza kufanya ndipo wanakutana na ukweli kwamba hakuna tofauti kubwa kati ya walichoacha kufanya na walichoanza kufanya.

Na muhimu zaidi, urahisi waliouona mwanzo wakati wanaingia, hawauoni tena wakishaingia. Wakishaingia ndiyo wanaona vitu ambavyo awali havikuwa vinaonekana.

Kitu kimoja muhimu sana ambacho wewe rafiki yangu nataka ukumbuke pale unaposhawishika kuchukua hatua muhimu kwenye maisha yako ni hichi; chochote unachokwenda kufanya, utakutana na ugumu na hata changamoto. Hata ushawishike kiasi gani kwamba kitakuwa rahisi, usijidanganye kwamba hakutakuwa na changamoto.

Ni sheria ya asili kwamba vitu huwa vinakuwa na ugumu na changamoto zake. Na kama kitu hakina ugumu wala changamoto, thamani yake pia inakuwa siyo kubwa.

SOMA; Huo mnyororo shingoni kazi yake nini? (gharama ya uhuru unayopaswa kulipa ili kufanikiwa).

Na kingine muhimu ambacho nataka uondoke nacho rafiki yangu ni hichi, kama kuna kitu unakimbia kule unakotoka, basi jua utaenda kukutana nacho kule unakokwenda. Kama unaondoka kwenye kazi moja au biashara moja kwa sababu ya kitu fulani unakikwepa, utashangaa sana pale utakapoingia kwenye kazi au biashara mpya na kugundua ulichokuwa unakikwepa umekutana nacho tena, labda kwa sura tofauti.

Hii ni kwa sababu, chochote unachojaribu kukikimbia kwenye maisha yako, kinaanzia ndani yako. Hivyo kukikimbia ni kujidanganya mwenyewe, utakutana nacho kwa namna ambayo hukutegemea.

Fanya chochote unachotaka kufanya kwa sababu ndiyo kitu sahihi na muhimu kwako kufanya. Na siyo kwa sababu unajiambia ndiyo kitu rahisi ambacho hakitakuwa na changamoto yoyote.

Pia kuwa makini sana na wale wanaokuletea fursa na kukushawishi kwamba ukichagua kufanya kile wanakuambia ufanye basi mafanikio ni uhakika na hakuna changamoto.

Popote panapohusisha fedha na mafanikio, ndugu wa karibu changamoto na matatizo hawakosekani. Yeyote anayekuambia hakutakuwa na changamoto wala matatizo, stuka haraka, kuna kitu anataka kukuibia.

Kabla hujakimbia chochote hakikisha kwanza umetatua tatizo ni nini. Kwa sababu usipotatua tatizo linaloanzia ndani yako, utakimbia utakavyo, lakini litaendelea kukufuata. Itakuwa ni sawa na mbwa ambaye anaangalia mkia wake halafu haupendi, hivyo anaamua kukimbia ili awe nao mbali. Kadiri anavyokazana kukimbia ndivyo mkia wake unavyozidi kumfuata.

Unapofanya chochote, jiandae kwa changamoto na magumu utakayokutana nayo kwenye safari yako ya mafanikio. Ondokana na dhana kwamba unachokwenda kufanya kitakuwa rahisi kuliko ulichokuwa unafanya awali. Vitu vizuri kwenye maisha siyo rahisi, na vitu rahisi kufanya huwa havina thamani kubwa.

Chagua kufanya kwa sababu ni muhimu na kwa sababu upo tayari kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora, pamoja na kukabili ugumu na changamoto utakazokutana nazo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha