MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tutaweza kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUENDELEA KUCHOCHEA MOTO…
Hakuna moto wowote ambao unaweza kuwaka milele iwapo hautaendelea kuchochewa. Kama ni moto wa kuni basi lazima uendelee kuweka kuni, kama ni wa mkaa lazima uendelee kuongeza mkaa. Na hata kama ni moto wa gesi, kadiri unavyoendelea kuwaka gesi inaendelea kupungua, hivyo baada ya muda lazima uongeze gesi ili kuchochea moto.
Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye kufanyia kazi malengo na mipango yetu.
Mwanzoni tunakuwa na moto mkubwa wa kufanya, hamasa inakuwa juu na tunafanya makubwa. Lakini kadiri tunavyokwenda, hamasa hii inapungua. Tunapokutana na changamoto, ndiyo kabisa moto huo unakuwa umekutana na maji, unazima haraka mno.
Dawa ya hilo ni kuendelea kuchochea moto huo kila siku, endelea kuchochea hamasa yako ya kufanya kile unachofanya kila siku.
Hamasa nzuri ya kutumia ni ile inayotoka ndani yako, ule msukumo wa kwa nini unafanya. Siyo hamasa ya nje ya nini unapata.
Hivyo ni muhimu sana kujua KWA NINI unafanya kile ambacho unafanya. Ni msukumo upi ambao unatoka ndani yako, ambao unakufanya uache mengine yote na kufanya hicho unachofanya.
Jikumbushe hili kila unapoianza siku yako na kila unapoanza kufanya kile unachofanya. Unapokutana na changamoto na mambo kuonekana ni magumu, usiangalie tu changamoto na ugumu, badala yake angalia KWA NINI ulichagua kufanya hicho unachofanya.
Kama KWA NINI yako ni kubwa na inatoka ndani yako, utapata msukumo mkubwa wa kuendelea, hata kama mambo ni magumu kiasi gani. Lakini kama KWA NINI yako ni ndogo na inatoka nje, hutafika mbali, itakuwa ni sawa na moto wa mabua, ambao unawaka haraka na kuisha haraka.
KWA NINI unafanya kile unachofanya?
KWA NINI upo hapa duniani?
KWA NINI asubuhi na mapema ukiache kitanda na kwenda kwenye shughuli zako?
Lazima kuwe na sababu kubwa, na siyo fedha au kuonekana na wengine pekee. Lazima kuwe na muunganiko mkubwa kutoka ndani yako na kile unachofanya.
Huu ni moto ambao unapaswa kuuchochea kila siku ya maisha yako ili usizime.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.