Nimepewa siku nyingine tena ambayo napaswa niitumie vizuri kwa kadri nitakavyoweza ili iweze kuleta tija kwa maisha yangu binafsi pamoja na maisha ya kizazi hiki ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Hii ni zawadi ya pekee ambayo thamani yake hakuna mwanadamu anaweza kuielezea pasipo na shaka ya aina yoyote. Zawadi iliyo kuu kwangu ni uzima na afya njema ambayo Mungu ameendelea kunitunuku hata muda huu ambao umenilazimu niwaambie jambo marafiki na jamaa zangu wa Tanzania.Leo napenda niwakumbushe marafiki ambao wapo kwenye hatua mbalimbali za uwekezaji wa ardhi na majengo ambao wamedhamiria kweli kufikia malengo makuu waliyojiwekea na wana mpango wa kuomba mkopo kupitia taasisi za fedha, Ni jambo jema sana kuzitumia taasisi hizi za fedha kufikia ndoto zetu kwa namna zozote vile itakavyowezekana, hii ni mbinu mojawapo ambayo baadhi ya marafiki zetu hutumia taasisi za fedha kama chanzo saidizi kwenye uwekezaji huu. Changamoto ni kwamba wengi wa marafiki wameshindwa na marafiki wachache ndio wamefanikiwa zaidi katika kuzifikia na kuzitumia vizuri taasisi hizi za fedha ambazo zinaendelea kuanzishwa na kukua kwa wingi ndani ya Tanzania. Kwanini wachache wafanikiwe na wengi washindwe kufanikiwa, tatizo ni nini. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia pale unapohitaji mkopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako ya kibiashara.

FAHAMU DHUMUNI KUU LA MKOPO

Kwa nini unafikiri kwamba ni lazima upate mkopo katika kufikia malengo yako, je endapo hautapata mkopo unaohitaji kuna mbinu yoyote mbadala itakayo kuwezesha kutimiza malengo yako? Hayo ndiyo baadhi ya maswali yangu ambayo mara zote ninapokutana na marafiki ambao wanahitaji kubwa la kuwezeshwa na taasisi za fedha kwa ajili ya ununuzi wa viwanja au ujenzi wa nyumba. Ni muhimu sana kuwa na dira ya jambo lolote unalokwenda kulifanya kabla hujaomba mkopo, kufanya hivyo kutakuwezesha kutembea kwa uhakika katika kutimiza malengo yako. Soma mfano ufuatao:

“Bwana Stephano Magulilwa wa uyole Mbeya aliomba mkopo wa kiasi cha Tsh. 20,0000,000 kwenye moja ya taasisi ya fedha ili kumalizia nyumba yake kwa ajili ya kulala wageni. Baada ya kupata mkopo huo alianza ujenzi haraka iwezekanavyo, mkopo huo alipaswa arudishe ndani ya muda wa miaka miwili(2) pamoja na riba. Lakini fedha hiyo haikufikia hata nusu ya umaliziaji wa jengo hilo, na mbaya zaidi ameandikiwa faini mbalimbali kutoka mamlaka za usimamizi wa mazingira na ujenzi kwa kutofuata taratibu rasmi za ujenzi. Kwa sasa yupo njia panda, pesa yote ipo kwenye jengo ambalo halizalishi na linaendelea kuchakaa, anadaiwa fedha za adhabu na mamlaka mbalimbali zaidi ya kiasi cha Tsh. 7,000,000 na muda wa kuanza kufanya marejesho kwenye taasisi ya fedha umeshafika. Kinachomuumiza akili zaidi ni biashara zake ambazo anazifanyia bidii sana kuzikuza lakini hali ya uchumi inazidi kumuangamiza, biashara inazidi kuwa mbaya pamoja na juhudi zote anazozifanya”.

Amekuja kwa marafiki kuomba ushauri wenu kuhusu nini cha kufanya ili ajinasue hapo alipofikia…..!!!!!!!!!!

Mara zote tumekuwa tunasisitiza sana umakini katika kuweka malengo na hatua mbalimbali za kimkakati ambazo zitakuwezesha kufikia malengo yako kwa uhakika huku ukiwa na furaha na amani ya moyo wako. Hakikisha unajipanga vizuri kwa kile unachokwenda kukifanyia kazi ili kuepuka mikwamo ambayo imetokana na kukosa ufahamu kwa kile anachokwenda kukifanya.

JIPE MUDA WA KUFANYA UTAFITI

Zipo sheria na taratibu mbalimbali zinazozisimamia taasisi za fedha katika kutoa huduma kwa wananchi, lakini kila taasisi ya fedha imeweka vigezo mbalimbali na tofauti kwa wateja wao ili kuwawezesha kupata huduma mbalimbali ikiwemo ya mkopo. Unapaswa ujipe muda mwingi wa kufanya tafiti ili kupata taarifa sahihi zinazohusiana na aina ya mkopo unao uhitaji, watembelee mameneja wa taasisi za fedha, watembelee mawakala wanao husika na mikopo ya mali, bima, wanasheria na washauri wa ujenzi. Ni muhimu sana kufanya utafiti ili kupata wigo mpana wa uchaguzi wa taasisi ambayo kwako itakupa unafuu zaidi katika kufikia malengo yako. Utafiti utakufanya ujitathmini upya kwa kile unachokwenda kukifanya, kutofanya utafiti utajiweka kwenye hatari kubwa usiyoijua. 

Tafakari sana kabla hujafanya maamuzi kwa vitendo. Usirubuniwe kwa ukarimu na hamasa ya kuwa una sifa zote za kukopesheka na kwamba usiwe na shaka yoyote. Ni lazima utambue kuwa hiyo ni biashara na wewe ni mteja, lengo lao ni kupata faida kupitia wewe, hivyo akili yako inapaswa itangulie mbele tamaa ibaki nyuma, Huwezi kupewa mkopo endapo hakuna kitu ambacho kitarudisha fedha zao endapo utakutwa na mkwamo wa kiuchumi.

MAANDALIZI NA UHAKIKI WA NYARAKA MUHIMU

Kwenye jambo lolote linalohusiana na fedha usipende kukurupuka, utulivu na ushirikiano wa mwili na akili yako ni muhimu sana. Nyaraka zina nguvu sana katika kukufanikisha kufikia malengo yako, pia nyaraka hizo zinaweza kuwa ni silaha kali zitakazo tumika kukuangamiza wakati usio utarajia, hivyo ni muhimu sana ukapata muda wa kutosha wa kuhakikisha unatimiza vigezo vyote vinavyotakiwa katika hali ya kuaminika huku na wewe ukiwa makini katika kujitathmini kwa chochote utakachopewa au kuamriwa kukifanya. Utashi wa akili yako ndiyo utakao amua hatma ya nini cha kufanya, kama hujiamini ni vema ukaambatana na mtaalamu au wakala wako atakayekusimamia vizuri katika makubaliano yoyote yatakayofanyika. Usiingie makubaliano ya aina yoyote ikiwa kwa upande wako yatakuwa siyo rafiki na itakuwia vigumu sana kwenye utekelezaji wa mipango yako. Wengi wameumia kupitia nyaraka zao wenyewe kwa sababu hawakuwa makini wakati wa makubaliano, maana wao muhimu ilikuwa ni kupata fedha tu. Pia baadhi ya nyaraka huchukua muda mwingi na hugharimu fedha katika maandalizi yake, hivyo ni muhimu sana ukajiandaa mapema katika kutimiza majukumu yako.

Ushauri wangu kwako rafiki, ni muhimu sana kuchukua tahadhari kwa kila hatua unayokwenda kuifanya. Hii dunia si nyepesi kama tunavyoitazama kwa macho yetu ya nyama na damu, baadhi ya wafanyakazi wa taasisi za fedha si waaminifu kabisa, matatizo mengine huwa ni ya kutengenezwa ili kukutia kwenye mkwamo wa aina yoyote kwa manufaa fulani watakayo yaona kwako. Huwa sishauri nyumba yako ya kwanza ya kuishi ujenge kwa mkopo, usitegemee mkopo kwa kuweka dhamana nyumba yako ya kuishi kwa ajili ya kampuni yenu, hakikisha nyumba yako inayoiombea mkopo ni nyumba ya kibiashara na itajilipa yenyewe pasipo kuathiri mambo yako mengine ya kiuchumi. Epuka tabia ya kupenda kukopa pasipo na ulazima wowote, hii itakufanya uwe na amani wakati wote wa uhai wako, maana hali ya uchumi wa sasa unaendeshwa kisiasa zaidi kupitia sera na taratibu mbalimbali za kiutawala, mabadiliko ya aina yoyote yanaweza kuathiri shughuli za kibiashara na uwekezaji tunaoufanya.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com