Ni siku mpya ambayo napaswa kuitumia vizuri katika kutimiza malengo makuu niliyoyaweka mwaka huu. Nidhamu, juhudi na maarifa ni dira na nguzo yetu katika kuyafikia malengo katika kila hatua ambayo tunapaswa kuifanyia kazi. Pamoja na hayo pia ni muhimu sana kuweka juhudi katika mafanikio ya mwili na roho ili maisha yetu yawe na thamani zaidi. Afya njema na imani thabiti ni msingi bora wa mafanikio katika hatua zote za kimaisha katika kuyafikia malengo yetu.

Maendeleo yanayojitokeza katika sekta ya ujenzi yamechangia kwa kasi mabadiliko ya sera na uchumi kwenye maendeleo ya makazi, biashara na uwekezaji wa ardhi na majengo. Katika sekta ya ujenzi zipo taasisi na kampuni binafsi na za serikali ambazo zimeanza kufanya biashara ya uuzaji wa nyumba kwa namna tofauti. Hata watu binafsi nao hujikuta wakifanya biashara ya ununuzi na uuzaji wa nyumba kwa sababu mbalimbali ambazo zimewasukuma kufanya biashara hii. Changamoto kubwa ya biashara hii ni rasilimali fedha kwa walio wengi na kutotambua hatari zinazoikabili aina hii ya uwekezaji. Lengo la Makala hii ni kukukumbusha umuhimu wa kuwa na maarifa kwenye biashara ili kupunguza changamoto ambazo zinaendelea kuwatesa baadhi ya marafiki. Leo nitazungumzia hatua tano muhimu zitakazokuongoza kutafakari na kujipima kabla hujanunua nyumba ili kuepuka baadhi ya changamoto ambazo leo zinawatesa baadhi ya marafiki.

nyumba28

FANYA UTAFITI KUTAMBUA HATARI

Ni muhimu sana ukafanya utafiti kwenye nyumba kabla hujaamua kufanya malipo ya aina yoyote, hii itakusaidia kutambua fursa zilizopo na mambo hatarishi ambayo yatakufanya ujutie baada ya kununua nyumba hiyo. Si kila anayefanya biashara ni muaminifu kwa kiwango unachofikiria wewe, umakini wako katika kufanya maamuzi ndio kutakufanya ushindwe au ufanikiwe kupata kile ulichokusudia. Jiridhishe kuhusu uhalali wa umiliki wa anayekuuzia, uliza kama inadaiwa kodi au deni la mkopo, fahamu matumizi halisi ya nyumba hiyo kama inaendana na malengo yako, watazame majirani na watembelee kwa nyakati tofauti, dadisi ubora wa nyumba hiyo, fikiria kuhusu uhalali wa kimazingira kuepuka majanga ya bomoabomoa, moto, mafuriko na vimbunga. Nunua nyumba sehemu salama kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza ambazo zingeweza kuzuilika endapo ungekuwa makini kabla hujafanya malipo ya aina yoyote. Utashi wako katika kufanya maamuzi ndio utakao amua kuhusu furaha na usalama wa nyumba utakayoinunua.

SOMA; Hizi Ndizo Mbinu Bora Za Kuepuka Majanga Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

PATA USHAURI WA WATAALAMU

Wakati tulionao ni wakati sahihi wa kufanya mambo kwa ufanisi na ubora unaokidhi viwango vyote vya kitaalamu katika kufanikisha biashara na uwekezaji wa majengo. Ni vizuri ukapata ushauri binafsi kutoka kwa wataalamu kabla hujafanya maamuzi ya aina yoyote, ni vema ukawatembelea wanasheria wabobezi wa majengo, washauri wa ujenzi, wakala wa bima na rasilimali nyumba. Wataalamu wana maarifa na ujuzi wa ziada kuhusu biashara unayokwenda kuifanya, watakushauri kwa namna tofauti kwenye kila hatua kuhakikisha unakuwa salama hata baada ya biashara kufanyika. Hivi sasa wamejitokeza wakala wengi sana wanaojihusisha na rasilimali nyumba na wapo vizuri sana kwenye uthamini na utafiti wa masoko ya nyumba, usiogope kuwatembelea wataalamu hawa, wapo kwa lengo la kukuhudumia wewe. Hili ni eneo muhimu sana ambalo unapaswa kulizingatia ili kulinda usalama na ubora kwenye nyumba unayokwenda kuinunua. Mikataba na maamuzi yote mtakayokubaliana unapaswa kutafakari zaidi ili isiwe tatizo kwa upande wako.

ZINGATIA LENGO KUU LA UNUNUZI WA NYUMBA

Malengo ni dira kuu katika maamuzi yetu kwenye kila hatua ya maisha, ni muhimu sana kujiuliza kama nyumba unayokwenda kuinunua ni sehemu ya malengo yako au ni fursa imejitokeza mbele ya akili yako, hata kama ni fursa nzuri na una uwezo nayo ni vema ukatafakari upya kama imekidhi vigezo au uwezekano wa kuitumia kwa matumizi uliyo yapanga kuyafanya. Kama matumizi ya eneo ni makazi na wewe lengo lako ni kuifanya kuwa hoteli au zahanati ni vizuri ukapata muongozo kabla hujafanya malipo ya aina yoyote, tafakari mazingira yaliyokuzunguka kama ni rafiki na matumizi ya nyumba unayokwenda kuinunua, fikiria kuhusu muundo na muonekano wa nyumba hiyo kama itakufanya uwe mwenye furaha katika kutimiza malengo yako. Wengi wamejikuta kwenye majuto baada ya kuona mapungufu mengi tofauti na walivyotarajia baada ya hatua zote za  ununuzi wa nyumba kukamilika. Usirubuniwe na umaridadi wa maneno ya kibiashara yakutoe nje ya uwezo wako wa kufikiri na kutafakari mambo kwenye kila hatua. Hatua hii itakusaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi ambayo yatakufanya ufurahie maisha yako wakati wote.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Pale Unapohitaji Mkopo Kwa Ajili Ya Ujenzi Wa Nyumba Ya Ndoto Yako.

TAFAKARI UWEZO WAKO KIFEDHA

Biashara ya ununuaji na uuzaji wa nyumba hufanyika kwa namna tofauti kutegemea na lengo kuu la muuzaji. Njia ya nipe nikulipe, mnada na njia ya mkopo ndizo hutumika na wafanyabiashara wengi katika kufikia lengo la kibiashara. Tafakari sana kuhusu hali ya uchumi na uwezo wako kifedha kama utamudu vizuri katika kukamilisha malipo ya ununuzi wa nyumba hiyo bila tatizo. Kama umenunua kwa njia ya mkopo tafakari sana kuhusu chanzo chako cha fedha kama kitashindwa kuzalisha fedha au kufa kabla hujakamilisha malipo, utafanya nini endapo hali ya uchumi itakuwa mbaya kwenye chanzo chako cha fedha, fikiria kuhusu kupanda kwa gharama za maisha kama hazitakuathiri kumudu marejesho ndani ya muda wa malipo ya ununuzi wa nyumba hiyo. Hii ni hatua muhimu sana itakayokufanya uepukane na msongo wa mawazo na fikra za kusadikika endapo utakuwa umesimamia msingi imara wa vyanzo vyako vya fedha kumudu vema mabadiliko yoyote ya kiuchumi.

TAFAKARI GHARAMA ZA ZIADA

Ni muhimu sana kufikiria gharama za ziada ambazo mara nyingi huwa hazionekani wakati wa mauziano ya nyumba. Gharama za kuwalipa wataalamu na gharama za marekebisho au umaliziaji wa nyumba zinapaswa kuainishwa mapema kabla ya utekelezaji wa maamuzi ya aina yoyote. Tafakari kuhusu gharama za huduma za kijamii kama vile mifumo ya taka ngumu, umeme, maji safi na maji taka, usafiri na mawasiliano kama utaweza kuzimudu bila matatizo ya aina yoyote. Hizi ni baadhi ya gharama ambazo zinatosha kuwatesa baadhi ya marafiki na kuwafanya wajutie kuchagua mazingira yaliyo nje ya uwezo wao. Usisite kudadisi kuhusu ubora na uchakavu wa miundombinu na gharama za huduma hizi ili kutathmini uwezo wako wa kifedha na ikiwezekana kuanzisha wigo wa kupunguziwa gharama za ununuaji wa nyumba hiyo. Hatua hii ni muhimu kuwa na mtaalamu ambaye atakuwezesha kukupa makadirio ya gharama za manunuzi ya nyumba na marekebisho ya aina yoyote mtakayokubaliana.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com