Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUWA TAYARI…

Kama ipo sababu moja inayoua na kukwamisha ndoto za wengi basi ni KUWA TAYARI…

Wengi wamekuwa na mipango na ndoto kubwa, ila hawaanzi kwa sababu wanaona bado hawajawa tayari.

Kuna vitu ambavyo wanataka kuwa navyo kabla ya kuanza, hivyo kabla hawajavipata wanaona hawapo tayari.

Ukweli ni kwamba, dunia haitajipanga kama unavyotaka wewe ndiyo uweze kuanza.

Dunia haitakupa kila kitu unachokitaka kwa wakati unaotaka na kwa mpangilio ambao umepanga wewe.

Hivyo unapopanga kufanya kitu chochote, unahitaji kuanzia pale ulipo, ukianza na kile ambacho unacho.

Ukishaanza, hata kama huna kila kitu unachotaka, dunia itaanza kukupa kila unachotaka. Utaanza kuona njia mbadala za kupata ulichotaka hata kama siyo kama ulivyotaka.

Wakati mwingine unahitaji kuanza ukiwa na imani kwamba mambo yatakwenda vizuri, na mara zote huenda vizuri hata kama unakutana na changamoto mbalimbali.

Usisubiri mpaka dunia ijipange kama unavyotaka wewe, anza na dunia itakuwa inakupa kile unachotaka kwa wakati ambao unakihitaji, au ukapata mbadala wake.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz