MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Hii ni nafasi nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUJIKUBALI SISI WENYEWE KWANZA….
Kila mtu anapenda kukubalika na wengine, lakini je unajikubali wewe mwenyewe kwanza?
Kila mtu anapenda kuheshimiwa na wengine, lakini je unajiheshimu wewe mwenyewe kwanza?
Kila mtu anataka kupendwa na wengine, lakini je unajipenda wewe mwenyewe kwanza?
Sheria ni kwamba, watu wanakupa wewe kile ambacho unajipa wewe mwenyewe.
Kama hujiheshimu hakuna atakayeweza kukuheshimu, kama hujikubali kila mtu pia hatokukubali.
Hivyo kabla hujaendelea kujiuliza na kulalamika kwa nini watu wanakuchukulia kwa namna fulani, hebu kwanza jiulize wewe mwenyewe unajichukulia kwa namna gani?
Kila kitu kinaanza na wewe, na watu wanajifunza kwako jinsi ya kukuchukulia na jinsi ya kwenda na wewe.
Hata kama unalipwa kiasi kidogo, ni wewe mwenyewe umewaruhusu watu wakulipe kiasi kidogo, watu wasingeweza kujua kama unafaa kulipa kiasi kidogo kama usingewakubalia.
Kwa maana hii basi, ni muhimu sana kuwa na misingi ya maisha ambayo inaendana na yale maisha ambayo unayataka. Kuwe na mambo ambayo lazima uyafanye, hata iweje. Yale ambayo yatawafundisha wengine namna gani wakuchukulie wewe.
Wewe pekee ndiye unawafundisha watu wakuchukulieje, hivyo wafundishe vizuri, kwa namna unavyotaka wewe. Chochote unachotaka watu waoneshe kwako, anza kukionesha kwako wewe mwenyewe, wengine nao watalazimika kufanya hivyo.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.