Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo 

letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza watu wenye imani kubwa hapa duniani. Je unawajua watu hao? Karibu tujifunze

Imani ndiyo nguvu kubwa ya binadamu hapa duniani, hata wale wanaoenda kwa waganga kinachowafanya waende na kuamini kwa mganga basi siyo kitu kingine zaidi ya imani. 

Imani ndiyo mahali ambapo watu wanaoamini wanaweza kufanikiwa katika yale wanayofanya kila siku.

Lakini pia, adui mkubwa wa imani ni mashaka, watu wengi kwa sasa wanateseka kwa kutokuwa na imani hata na maisha yao binafsi. Mtu hana imani na kazi anayofanya, hana imani ndoto aliyokuwa nayo yaani wengine wakifikiria ndoto zao na jinsi imani ilivyo mwisho wa siku wanaishia kukata tamaa tu hapa duniani.

Rafiki, imani ndiyo inayotuamsha asubuhi na mapema na kwenda kufanya kile kitu unachopenda na imani ya mtu juu ya kitu anachoamini ndiyo inampa mtu hamasa kubwa ya kuendelea kufanya mambo makumbwa hata kama wengine wanaona haiwezekani. Bila kuwa na imani ni sawa na bure katika haya tunayofanya. Kitu unachofanya una imani nacho ndiyo maana unaendelea kukifanya kwa sababu unaamini kitakupa matokeo au mafanikio unayoyataka.

Ndugu msomaji, shabaha yangu leo ni kutaka kukushirikisha mfano wa watu wenye imani kubwa hapa duniani. Watu wenye imani kubwa hapa duniani si watu wengine bali tunaishi nao majumbani mwetu kama siyo kuwaona kwa wengine ambao ni watoto wadogo. 

Watoto wadogo wana imani kubwa ambayo haijawahi kutokea katika maisha ya watu wazima.

Watoto wadogo wana uhakika wa kula kila siku bila kujua chakula kinatoka wapi. Watoto wadogo wana imani kubwa kutoka kwa wazazi wao kuwa wanaweza kuomba chochote kutoka kwa wazazi wao na wakafanikiwa bila shida yoyote. Watoto wadogo huwa wanadai tu mahitaji yao kutoka kwa wazazi wao na huku wakiamini kuwa wazazi wao wanaweza kuwapatia kile wanachoomba.

Tukiwa na imani kama watoto wadogo basi tunaweza kutenda makubwa katika maisha yetu na wala hatutoweza kudanganywa. Wewe ambaye imani yako ni haba utaendelea kuwa jalala la matatizo mengi yasiyoisha. Kama unafanya chochote na huna imani nacho kiache mara moja kwani kufanya bila imani ni kupoteza muda tu rafiki yangu.

Hatua ya kuchukua leo, kuwa na imani kama ya watoto wadogo na imani yako itaponya yale unayotaka. Pasipo kuwa na imani kama watoto wadogo tutakuwa na maisha yasiyokuwa na maana hata kidogo. Imani ndiyo chemchem ya matunda tunayotaka kuyaona kupitia ndoto zetu.

Kwa kuhitimisha rafiki, akili na imani ni vitu viwili vinavyokwenda sambamba kwa wakati mmoja yaani concurrent. Akili yako ukiimanisha basi itakupa kile unachokiamini, chunga sana kile unachokiamini kwa sababu akili inatenda kulingana na imani yako na tukikosa imani chanya katika maisha tunapoteza maisha.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.