Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Ni siku nyingine mpya na nzuri ambapo tumepata nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NZURI NA BORA…
Kufanya kitu kwa uzuri pekee hakutoshi, bali tunapaswa kufanya kwa ubora wa hali ya juu.
Hii ni kwa sababu ubora pekee ndiyo utakaokutofautisha na wengi ambao wanafanya vizuri.
Ubora pekee ndiyo utawafanya watu waweke thamani kubwa kwenye chochote unachofanya.
Na ni ubora pekee ambao unamsukuma mtu kwenda hatua ya ziada, kwenda zaidi ya anavyokwenda kwa wakati husika.
Lakini pia, nzuri ni adui wa bora,
Watu wengi wakishafanya vizuri wanaona wamefanya sana, wanaridhika na kujisahau, na hilo linawazuia kuwa bora zaidi.
Hivyo unapozoea kufanya kwa uzuri na kuridhika kwa kufanya vizuri, unasahau kuna ubora zaidi na kushindwa kufikia ubora huo.
Ubora hauna kikomo, kila unachofanya, hata kama upo juu kiasi gani, bado ipo nafasi ya kukifanya kuwa bora zaidi.
Hivyo, mara zote usikazane tu kuwa mzuri au kufanya vizuri, badala yake kazana kuwa bora zaidi. Kila siku kwa kila unachofanya, jiulize unawezaje kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa jana? Kwa njia hii utafanya makubwa na kufanikiwa zaidi.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.