Habari za leo rafiki yangu,

Karibu kwenye kipengele chetu cha makala za nyeusi na nyeupe ambapo tumekuwa tunauangalia ukweli jinsi ulivyo, bila ya kupindisha maneno wala kutaka kubembelezana. Kwa kuwa ukweli huwa unaumiza, wengi hupenda kuukwepa au kuuficha. Lakini hayo yote hayaubadili ukweli.

Leo kwenye nyeusi na nyeupe nakwenda kukupa mbinu za kupata gari aina ya Noah ya rangi nyeusi au rangi yoyote ambayo unaipenda wewe.

Kabla hatujaangalia unawezaje kupata Noah yako, kwanza nijibu swali kwa nini Noah?

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2017, kumekuwa na juhudi za serikali za kuhakikisha ya kwamba wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi. Juhudi hizi zilipelekea baadhi ya makampuni kuzuiwa kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi pamoja na kuundwa kwa kamati kuchunguza mikataba ya uchimbaji wa madini.

Baada ya kamati zilizoundwa kutoa majibu ya uchunguzi waliofanya, iligundulika kwamba makampuni ya madini yamekwepa kodi na malipo mengi, kiasi kwamba iwapo watalipa fedha hizo zot, kila mwananchi anaweza kupatiwa gari aina ya Noah.

Hapo ndipo ulipoanza utani kwenye mitandao ya kijamii, watu wakisema kwamba wanasubiri Noah zao, na wengine wakawa wanachagua rangi kabisa. kitu ambacho kilianza kama utani, kuna watu wakawa wanaanza kuamini kabisa kwamba Noah zinakuja na wanaendelea kusubiri.

Hapa ndipo tunapohitaji kuuangalia ukweli kama ulivyo, bila ya kujifurahisha na lolote. Iwapo fedha zote zinazodaiwa kwenye makampuni hayo ya madini zitalipwa kwa serikali, hakuna mwananchi hata mmoja ambaye atapewa Noah, achilia mbali kugaiwa fedha hizo moja kwa moja. Ni kitu ambacho hakijawahi kutokea popote duniani na hakuna msingi wowote wa kitu kama hicho kutokea. Naomba ieleweke wazi hii siyo siasa wala propaganda, bali ni ukweli kama ulivyo.
 
 
Sasa basi nirudi kwa wale marafiki zangu ambao wanasubiri Noah zao nyeusi au rangi nyingine. Hapa nataka nikupe mbinu ya kuweza kupata Noah yako, hutakuwa na haja ya kuendelea kusubiri Noah ambazo huna uhakika kama zinakuja.

Hizi hapa ni hatua kumi muhimu za kuhakikisha unapata gari yako aina ya noah, au hata gari ya aina nyingine.

1. Jua kwa nini unahitaji gari hiyo.

Je unahitaji tu kwa sababu kila mtu anayekuzunguka naye ana gari? Ni maamuzi ya hovyo, achana na mpango huo.

Je unaitaka kwa sababu unaweza kufanyia biashara? Maamuzi mazuri endelea.

Je unaitaka kwa sababu itakurahisishia kwenye shughuli zako? Maamuzi mazuri, endelea.

2. Jua gharama ya ile gari unayohitaji.

Baada ya kujua sababu halisi ya wewe kutaka gari, jua gharama yake. Hapa sasa utajiuliza iwapo unaweza kununua gari mpya kabisa, ambayo ni gharama kubwa, au kununua gari ambayo imeshatumika, ambapo gharama inakuwa chini kidogo.

Ukichagua kununua gari ambayo imeshatumika, kuna mawili hapo, labda uagize moja kwa moja kutoka nje, au kununua iliyoagizwa yaani imetumika nje. Au kununua ambayo imetumika hapa hapa nchini. Hapo pia kuna tofauti ya bei na ubora pia.

3. Jua fedha unatoa wapi.

Unataka kukopa ili ununue gari? Maamuzi mabovu, achana nayo.

Je katika kipato chako unachoingiza, unahitaji kutenga kiasi gani ili ndani ya mwaka mmoja au miwili uwe umefikisha kiasi cha kununua ile gari ambayo unaitaka?

Njia bora ya kununua gari yako ni kupitia akiba zako, na siyo kukopa. Hata kama ni gari ya biashara, kama ni ya kwanza, utakuwa salama iwapo utanunua kwa fedha zako na siyo kukopa.

Usiwe na haraka ya kuipata hiyo gari, umeishi miaka mingi bila gari na maisha yako yalikuwa yanaenda, jipe subira ya mwaka mmoja au miwili ya kujichanga ili uweze kununua Noah yako.

4. Kama huna udhibiti wa fedha, weka kwenye akaunti maalumu.

Kwa kuwa umechagua kujichanga ili kufikisha fedha ya kuweza kununua gari yako, unaweza kukutana na changamoto ambazo zinaweza kupelekea wewe kutumia fedha ulizoweka akiba. Hivyo unahitaji kuwa na njia ya kuzuia wewe usitumie fedha hizo.

Hivyo unaweza kufungua akaunti maalumu, ambayo unaweka tu na hutoi, ndani ya kile kipindi ambacho umepanga kufikisha kiasi kile cha fedha.

5. Anza kutafuta taarifa na maarifa zaidi kuhusu magari.

Wakati unaendelea kujichanga ili kufikia kile kiasi cha kupata gari yako, endelea kujielimisha kuhusu magari. Pata maarifa sahihi kuhusu magari, jua changamoto mbalimbali na jinsi ya kuzitatua.

Kama bado hujajifunza kuendesha gari fanya hivyo na hakikisha unafuatilia na kupata leseni ya udereva. Ili unaponunua gari yako, uwe tayari na uzoefu kiasi wa kuendesha.

6. Tafuta fundi unayemwamini, ambaye atakuwa msaada kwako kuhusu magari.

Unahitaji kuwa na fundi wa magari ambaye unamwamini sana, huyu atakuwa msaada kwako kuhusu magari.

Kwanza atakusaidia iwapo umechagua kununua gari kwa mtu moja kwa moja, utaenda naye akusaidie kukagua gari kabla hujainunua. Ni muhimu awe fundi mwaminifu kwako, ili akuambie ukweli. Ukiwasikiliza madalali utauzia gari mbovu kabisa.

Pili huyu atakuwa fundi wa gari lako wakati wote. Ukishakuwa na gari, unahitaji kuwa na fundi mmoja ambaye ndiye analifanyia kazi kila wakati, hii inakusaidia sana. Ikiwa unatengeneza gari yako kwa mafundi mbalimbali, likitokea tatizo hutajua fundi yupi kasababisha.
 

7. Wakati wa kununua gari.

Kile kiasi ulichokuwa unachanga kinapotimia na sasa unahitaji kununua gari, inategemea unanunua kwa nani.

Kama unanunua kwa mtu, hakikisha anayekuuzia ni mmiliki wa gari, akupe kadi ya gari iliyoandikwa majina yake, ambapo utahitaji pia akupe kitambulisho chake ili uwe na uhakika yeye ndiye mmiliki hasa wa gari. Hii itakusaidia kuepukana na changamoto mbalimbali, ambazo huwa zinajitokeza pale unapouziwa gari na mtu wa tatu.

Kama gari unaagiza, unaweza kuagiza mwenyewe au kununua kwa waagizaji, jua kodi unayopaswa kulipa kwa kuingia kwenye tovuti ya TRA kukokotoa kiasi cha kodi unayopaswa kulipa kwa gari unayoagiza (unaweza kufungua hapa; http://gateway.tra.go.tz/umvvs/ )

8. Baada ya kununua gari.

Kama umenunua kwa mtu, hakikisha unabadili kadi ya gari ili kumiliki gari hiyo moja kwa moja. Hili linafanyika kupitia TRA na gharama za kufanya hivyo zipo hapa; https://www.tra.go.tz/index.php/2012-11-20-06-36-17

Kama umeagiza kutoka nje, jiandae kutoa gari yako mapema inapofika kwa kulipa kodi zote husika. Kuchelewa kufanya hivyo kutapelekea wewe kutozwa faidia ambazo ni kubwa mno.

Ikatie gari yako BIMA KUBWA, ili ikusaidie kwa changamoto unazoweka kukutana nazo. Achana na bima ndogo, kama umeweza kutenga fedha kununua gari, basi hakikisha kila mwaka unatenga fedha ya kulipia bima kubwa.

9. Sasa una gari, itumie kwa matumizi uliyokusudia.

Baada ya kuwa na gari yako, itumie kwa matumizi uliyokusudia. Kila wakati angalia namna bora ya kunufaika na gari hiyo.

Kama ni gari ya matumizi binafsi, igeuze kuwa darasa au chuo, kwa kusikiliza vitabu vilivyosomwa (AUDIO BOOK) kila unapokuwa unaendesha. Hili litakuwezesha wewe kujifunza mambo mengi ukiwa ndani ya gari lako. Kama unahitaji AUDIO BOOKS unaweza kuzipata hapa; http://www.amkamtanzania.com/p/blog-page.html

10. Itunze gari yako.

Ukishanunua gari siyo kwamba umemaliza kila kitu, gari inahitaji huduma kama mwili wa binadamu unavyohitaji huduma.

Mara kwa mara kuna service za kufanya kwenye gari, jua wakati wa kufanya hivyo na zingatia.

Pale unaposikia sauti au hali usiyoielewa kwenye gari yako, wasiliana na fundi wako uliyemchagua kuhudumia gari yako.

Pia iendeshe gari yako kwa uangalifu na kuzingatia sheria ili kuepuka ajali.

Gari ni matunzo, kadiri utakavyoitunza vizuri, ndivyo unavyoifaidi na kuifurahia.
 

Hizi ndiyo hatua kumi za kupata gari kwa juhudi zako mwenyewe, bila ya kutegemea mtu yeyote anayekuahidi ambaye huna uhakika wa kuipata. Fanyia kazi haya uliyojifunza siyo tu kwenye kununua gari, bali kwenye mambo mengine yote muhimu kwa maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,


Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.