MAKIRITA AMANI:
Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo ambapo tunapata nafasi nzuri ya kwenda kuweka ubora kwenye kile ambacho tunafanya.

NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ndiyo msingi mkuu wa mafanikio yetu ya leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu COMFORT ZONE…
Kila mmoja wetu ana eneo lake la faraja, eneo ambalo amezoea kufanya na kupata matokeo fulani.
Kwa kuwa mtu ana uhakika na eneo hilo, basi anaendelea kubaki pale.
Anafanya kile ambacho amezoea kufanya, kwa sababu ana uhakika wa matokeo fulani na pia changamoto ameshazijua.
Lakini eneo hili siyo eneo zuri kwa mafanikio, kwa sababu hakuna kitu kikubwa na cha kipekee kinachofanyika kwenye COMFORT ZONE.
Kinachofanyika ni mwendelezo wa kilichofanyika jana, hivyo matokeo ya leo yanakuwa kama ya jana.
Kama unafanya kile ambacho umekuwa unafanya kila siku,
Kwa mtindo ambao umekuwa unafanya,
Ukiwa na fikra na mategemeo ambayo umekuwa nayo siku zote,
Huhitaji sayansi ya roketi kujua kwamba utapata matokeo ambayo umekuwa unapata kila siku.
Kama unafanya kile ambacho unajisikia amani kufanya, hakikutishi, hakikupi hofu ya kushindwa na kupingwa au kukatishwa tamaa na wengine, upo kwenye COMFORT ZONE yako.
COMFORT ZONE imekuwa kifo na kaburi la ndoto kubwa sana za watu wengi.
Lazima uweze kutoka kwenye eneo hilo kama unataka kufanya makubwa zaidi na kupata matokeo bora zaidi.
Na siku ya kuondoka kwenye eneo hilo siyo nyingine bali leo.
Leo hii, kipi unakwenda kufanya ambacho kitakusukuma kuondoka kwenye wigo wako wa mazoea? Kipi hatari unachokwenda kujaribu leo, ambacho kitakuweka kwenye hatari ya kushindwa na kupingwa na wengine?
Kama hakuna kitu cha aina hiyo unachoweza kufanya leo, kuna uwezekano mkubwa kwamba unakwenda kupoteza siku ya leo kama ilivyo.
Fanya kitu leo na kila siku ambacho kitakuondoa kwenye COMFORT ZONE yako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.