Mara nyingi watu wanapoweka mipango yao ya kibiashara, hujiangalia wao zaidi.
Hili huanzia kwenye kufikiria biashara ya kufanya, wengi hufikiria kile ambacho wanapenda wao, na kwenda nacho kwa njia ambayo wanaitaka wao.
Pia katika mabadiliko ya kibiashara, wengi hujiangalia wao. Kwa mfano katika maamuzi ya kubadili bei au kubadili huduma mtu anazotoa, wengi huangalia upande wao zaidi.
Lakini tukirudi kwenye msingi mkuu wa biashara, biashara ni njia ya kutoa thamani kwa wengine. Unaona hapo kuna thamani na wengine, lazima thamani iwepo na lazima wengine, wale wanaoihitaji thamani hiyo pia wawepo.

Hii ina maana kwamba, unaweza kuwa na thamani, lakini wengine wasione thamani hiyo. Na ndiyo maana hata kama unafanya biashara unayoipenda, angalia kwanza kipi ambacho unaongeza thamani kwa wengine. Watu gani ambao unawasaidia kupiga hatua, ambao watakuwa tayari kutoa fedha zao ambazo huenda wamezipata kwa shida sana na kukupa wewe.
SOMA; BIASHARA LEO; Mwisho Wa Ufalme Wa Mteja.
Mipango yako yote unayoweka kwenye biashara, anza kwanza kumfikiria mteja. Kwa kumwangalia mteja, yule ambaye unamhudumia na kumsaidia kutatua changamoto au kumpa mahitaji yake. Lolote unalotaka kubadili, angalia je litaongeza thamani zaidi kwa mteja? Litarahisisha mteja kupata ile thamani ambayo unaitoa?
Usijiangalie wewe pekee, angalia na wale ambao wanafanya wewe uwepo. Hii itakufanya uendeshe biashara yako kwa mafanikio makubwa, kwa kuwa na wateja ambao wananufaika sana na biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog