Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu WATU WABAYA KATIKATI YA WATU WABAYA…
Wakigombana watu wawili, halafu ukachukua nafasi ya kumsikiliza kila mmoja kwa wakati wake nini kimesababisha wagombane, kila mmoja atakuwa na lawama kwa mwenzake.
Kila mmoja atakuambia mwenzake ndiye mbaya, ndiye aliyefanya jambo ambalo lilipelekea ugomvi utokee. Labda mmoja alisema neno ambalo lilimuudhi mwenzake, mwenzake akamjibu kwa neno kali zaidi halafu ugomvi ukaibuka.
Je hapo nani mbaya kwa mwenzake?
Ukiangalia kwa kina, utaona wote ni wabaya, kila mtu ana ubaya wake ndiyo maana ugomvi umeibuka. Kama mmoja angekuwa mwema, wala ugomvi usingetokea.
Kwa mfano wapo watu wawili wameshindwa kuelewana, maongezi yameanza kwenda kwenye maneno makali, mmoja akaamua kunyamaza na kuondoka, unafikiri utatokea ugomvi? Jibu ni hapana, labda awepo kichaa ambaye anachotaka yeye ni ugomvi tu.
Ninachotaka tutafakari hapa rafiki ni kwamba, sisi ni watu wabaya ambao tunaishi katikati ya watu wabaya.
Na hatujiambii hivi kujidharau au kujikatisha tamaa, bali kutumia fursa hiyo kuepuka kuingia kwenye ugomvi na wengine.
Pale ambapo unajikuta kwenye hali ya kutoelewana na wengine, unachohitaji kufanya ni kukumbuka kwamba ubaya wako ndiyo utapelekea hali kuwa mbaya au ngumu zaidi. Hivyo unahitaji hatua za makusudi kuhakikisha hali inakuwa nzuri.
Unapokubali kwamba wewe ni mtu mbaya unayeishi katikati ya watu wabaya, unalazimika kuwa mwema ili kuondokana na changamoto zisizo za lazima.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.