Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu TATIZO SIYO KUJUA NINI CHA KUFANYA…

Kila mtu anajua nini anapaswa kufanya, angalau kwa kiasi fulani,

Mfanyakazi ambaye yupo kazini lakini hajitumi kwenye majukumu yake,

Mfanyabiashara ambaye biashara yake haikui,

Mtu ambaye anahitaji kufanya mazoezi,

Mtu ambaye anahitaji kujiweka vizuri kifedha,

Wote hao wanajua nini wanapaswa kufanya ili kupata kila wanachotaka,

Lakini wengi hawafanyi, na hata wanaoanza kufanya, wanaishia njiani.

Hivyo tatizo kubwa siyo kutokujua nini cha kufanya, tatizo kubwa ni kuwa na nidhamu ya kuweza kufanya kile mtu anachotaka kufanya, bila ya kuishia njiani haya kama changamoto ni kubwa.

Nidhamu ndiyo inayowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoishia kuwa kawaida.

Vipo vishawishi vingi vya kuacha kufanya kile unachopaswa kufanya, kwa sababu mara nyingi huwa ni kigumu.

Na zipo changamoto nyingi zinazoingilia kile ambacho mtu amechagua kufanya.

Wasio na nidhamu binafsi hawawezi kuvuka mambo hayo mawili, hivyo licha ya kujua wanachopaswa kufanya, wanaendelea na maisha yao bila ya kufanya.

Usiwe wewe rafiki yangu, ukishajua unachopaswa kufanya, FANYA, ije mvua, lije jua, FANYA.

Fanya kwa sababu huna namna nyingine, kwa sababu ndiyo njia pekee uliyonayo, kwa sababu ndiyo maisha umechagua.

Unakwenda kufanya nini leo ambacho umekuwa unaweka pembeni kila siku?

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz