Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kupata matokeo mazuri leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KILA MTU ANGEFANYA…
Kwa kawaida watu wanapenda kufanya vitu rahisi, vitu ambavyo havina changamoto.
Lakini ukweli ni kwamba, kitu kikiwa rahisi, kila mtu anafanya na thamani yake inakuwa ndogo.
Biashara zenye mafanikio zingekuwa rahisi na zisizo na changamoto, KILA MTU ANGEFANYA na zisingekuwa zenye mafanikio tena.
Kazi nzuri na zinazolipa zingekuwa rahisi na zisizo na changamoto, KILA MTU ANGEFANYA na zingeishia kuwa za kawaida sana.
Chochote unachoangalia kwa wengine na kuona ni chema na ungependa na wewe kufanya, jua kabisa siyo rahisi kufanya na kina changamoto nyingi.
Hivyo unapokuwa njia panda, kati ya rahisi na yenye changamoto, kama unataka kupiga hatua, pita yenye changamoto.
Changamoto zinawapunguza wale ambao siyo makini, hivyo ushindani unakuwa mdogo.
Changamoto zinakufanya ukue zaidi katika kuzitatua na hivyo kuweza kupiga hatua.
Changamoto zinaongeza thamani, kwa sababu watu wanakimbia chenye changamoto, lakini pia wanaotatuliwa changamoto wanakuwa tayari kulipa vizuri.
Ingekuwa rahisi na isiyo na changamoto, kila mtu angefanya na thamani yake ingeshuka. Usikimbilie urahisi, kimbilia kitu chenye thamani.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.