Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DUNIA ISIYO NA SUBIRA…
Tunaishi kwenye dunia ambayo kila kitu ni SASA na HAPA.
Watu tunategemea kila kitu kitokee haraka kama tunavyotaka sisi wenyewe.
Hatuna subira ya kutoa muda kwa kitu ambacho kinachelewa.
Fikiria mtandao ambao unakusumbua na huwezi kupakua picha unayotaka kupakua, unaachana nayo mara moja na kwenda kwenye jambo jingine.
Ni ulimwengu wa kipekee sana ambapo tunataka kasi kwenye kila kitu.
Kitu ambacho tumekijua leo, tunakitaka jana. Yaani unakitaka mno kitu ambacho ulikuwa hata hukijui.
Maendeleo ya teknolojia yamefanya kasi hii ya dunia iwezekane, kuanzia mitandao yenye kazi kubwa, usafiri wenye kazi kubwa na hata vitu vya matumizi ambavyo vina kasi kubwa kwenye shughuli ndogo ndogo kama kupika, kufanya usafi n.k.
Wakati tunaweza kufurahia hali hii kwenye maeneo mengi ya maisha yetu na hata kuwabeza wale ambao hawawezi kwenda kasi kama sisi, kuna maeneo ya maisha yetu ambayo tukiweka kasi, tunapoteza zaidi ya kupata.
Kwenye fedha, kadiri unavyozitaka kwa kasi, ndivyo unayopoteza nyingi zaidi.
Kwenye mafanikio, kadiri unavyoyataka yaje kwako kwa kasi, ndivyo yatakavyokukimbia zaidi.
Katika maisha ya kawaida, vitu vyenye thamani kubwa kwetu kama mafanikio, fedha, mahusiano afya na hata kazi au biashara, vinahitaji subira ya hali ya juu. Ukikosa subira, utakimbizana na kila kitu na kuishia kupata matokeo ambayo ni mabaya zaidi.
Kukosekana kwa subira kwenye maeneo mengi ya maisha yetu, kusitudanganye tuone kwamba kila eneo la maisha yetu linahitaji kasi, yapo mengi mno yanayohitaji subira ya hali ya juu.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.