Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tutakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu TABIA…

Sisi binadamu ni viumbe wa tabia,

Tabia ni kitu chenye nguvu sana kwenye maisha yetu.

Tupo tulipo sasa, kutokana na tabia ambazo tumeshajitengenezea.

Kwanza tunazijenga tabia, halafu tabia zinatujenga.

Unaanza kujifunza tabia, unaifanyia kazi, halafu baada ya muda tabia inatawala maisha yako, hata kama huitaki, inaendesha maisha yako.

Tabia ambazo ni mbaya huwa ni rahisi mno kuzijenga, lakini ni ngumu sana kuzivunja. Tabia kama uvivu, uzembe, ulevi n.k zinajengeka kirahisi.

Tabia ambazo ni nzuri huwa ni ngumu mno kuzijenga, lakini rahisi sana kuzivunja. Tabia kama uchapa kazi, nidhamu, kuweka akiba n.k unahitaji kuweka nguvu kubwa, lakini ni rahisi kuachana nazo.

Unapohitaji kuondokana na tabia fulani uliyonayo, lazima uibadili na tabia nyingine, ambayo itachukua nafasi ya tabia unayoiacha.

Na lazima uweke muda wa kujenga tabia hiyo, kufanya hata kama hujisikii kufanya.

Hivyo rafiki, tabia yoyote uliyonayo sasa, unaweza kuibadili na kujenga tabia nyingine nzuri. Inahitaji muda na juhudi kuweza kujenga tabia nzuri. Na pia inahitaji nidhamu kuweza kuendelea na tabia yoyote nzuri.

Ni tabia ipi mbaya unataka kuondokana nayo, na ipi nzuri unataka kujijengea?

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz