Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanatumia sababu za ajabu sana kuendesha biashara zao kwa uzembe. Moja ya sababu hizo ni kuogopa kuwasumbua wateja.

Wapo wafanyabiashara ambao wamekuwa wanapoteza wateja kwenye biashara zao, kwa sababu wanaogopa kuwasumbua.

Labda ni kumkumbusha mteja kuja tena kwenye biashara, wengi huona wakifanya hivyo mteja ataona ni kama anasumbuliwa. Hivyo wanamwacha tu, mteja akikaribishwa pengine anaenda na hutamwona tena.

Biashara

Wakati mwingine ni kuhusu malipo, labda mteja amenunua kitu ila hakulipa, sasa wafanyabiashara wengi husubiri wakiamini kwamba mteja atakumbuka na kulipa mwenyewe. Hapa husubiri mteja alipe na asipofanya hivyo, wao hukwama. Hawapendi kuwasisitizia wateja hao kulipa kwa kuwakumbusha mara kwa mara, kwa kuona itakuwa ni usumbufu kwa wateja wao.

Eneo jingine ni kwa wateja walioahidi kununua. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanawaachia tu, wakiamini wateja watakumbuka na kununua kama walivyoahidi. Wanaona kuendelea kuwakumbusha itakuwa ni kuwasumbua, na hapo wanawapoteza kabisa.

Ukweli ni kwamba, iwapo biashara yako ina thamani kwa wateja wako, chochote unachofanya hakitakuwa usumbufu kwao, badala yake kinakuwa ni bahati nzuri kwao.

Kama wateja wanathamini kweli kile unachofanya, unapowakumbusha kukaribia tena, wanaona ni nafasi nzuri ya kupata huduma kwako na watakuja. Unapowakumbusha kulipa wanaona ni wajibu wao kwa sababu wanapata huduma kutoka kwako. Na unapowakumbusha ahadi yao ya kununua au kulipia, wanafurahi kwa sababu maisha yanaweza kuwa yamewafanya wasahau ahadi waliyoweka.

SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Yako Inavyozidi Kukua, Unahitaji Kubadili Mikakati…

Swali linakuwa utajuaje kama wateja wanathamini biashara yako kweli?

Na jibu ni rahisi, kwa kufanya kile ambacho unaona ni usumbufu. Wale wanaojali hawataona ni usumbufu, na kwa hakika watafurahia kile unafanya kwa sababu wataendelea kutegemea kupata huduma zaidi kutoka kwako.

Lakini wale wasiojali, wataona ni usumbufu na wataachana na wewe, hutawaona tena. Na hapo unakuwa umefanya jambo jema la kuwasafisha wateja wako, kubaki na wale muhimu ambao unaweza kuwahudumia vizuri.

Usiogope kufanya jambo jema la biashara yako kwa kuona unawasumbua wateja. Kama ni kuitangaza biashara yako, iutangaze sana. Watu wanakutana na jumbe nyingi kila siku, ni rahisi kusahau kuhusu wewe. kama unawakumbusha wateja kuhusu kulipa au kununua, fanya hivyo mara nyingi uwezavyo, kwa sababu watu wana mambo mengi na wanasahau.

Kadiri unavyoonesha umakini na biashara yako, ndivyo pia wateja wanavyokukubali na kupenda kuendelea kuwa na wewe. Ila kama utaendesha biashara yako kwa aibu, wateja nao watakuonea aibu na wataachana na wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog