Habari za leo rafiki?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa tunayotaka kwenye maisha yetu. Hakuna jambo lolote lenye thamani ambalo ni rahisi kufanya. Kila kitu kina changamoto, hivyo kutatua changamoto hizi ndiyo njia pekee ya kufanikiwa.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kushindwa kwenye biashara. Kila mfanyabiashara mwenye mafanikio leo, ana hadithi ya kushindwa alipokuwa anaanza biashara. Wapo ambao wameshindwa kwenye biashara nyingi lakini leo wamefanikiwa.

Pia wapo wale ambao kila biashara wanayoanzisha inashindwa, kitu ambacho kinawafanya wakate tamaa na kuona hakuna namna tena kwa wao kufanikiwa kwenye biashara. Hawa ndiyo tunakwenda kuzungumza pamoja hapa, tuone ni hatua zipi wanaweza kuchukua.

Kabla hatujaangalia ni njia zipi za kuchukua pale mtu anaposhindwa kwenye kila biashara anayoanzisha, tupate maoni ya msomaji mwenzetu anayepitia kwenye hali hii;

Changamoto kubwa kila ninapojaribu biashara napata hasara, najitahidi sana kusoma vitabu kujifunza na ni mvumilivu sana navumilia mpaka najikuta hata mtaji unakufa nakopa, na biashara hizo ninazofanya wengine wanafanikiwa… Mpaka sasa sijajua ni wapi nakosea hivyo changamoto kubwa kwangu kwa sasa ni mtaji na kutopata faida niliyokusudia. – Salma R. L.

Kama ambavyo ametushirikisha msomaji mwenzetu Salma, wapo wengi ambao wanapitia hali kama anayopitia yeye. Wanaanzisha biashara inakufa, wanaanza nyingine nayo inakufa. Wanajaribu kuwa wavumilivu lakini uvumilivu wao ndiyo unawapoteza zaidi kuliko kuwasaidia.

Hapa nakwenda kuwashirikisha hatua za kuchukua pale unaposhindwa kwenye kila biashara unayoanzisha. Na hili nitalifanya kwa njia ya maswali, ili mtu ujihoji na kuona wapi unapokosea mpaka biashara unazoanzisha zinashindwa.

Swali la kwanza; je unaijua biashara yako vizuri?

Sehemu muhimu kabisa ya mafanikio ya biashara, ni kuijua biashara yenyewe. Bila ya kuijua biashara kiundani, utakuwa unajidanganya kama unafikiria unaweza kufanikiwa.

Je unaijua biashara nje ndani? Unajua kila kitu ambacho kinahusu biashara hiyo? Kuanzia upatikanaji na uandaaji wa bidhaa au huduma, upangaji wa bei, washindani kwenye biashara na hata kitu cha tofauti unachokwenda kufanya wewe?

Hili ni muhimu sana kwa sababu watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara ambazo hawazijui kwa undani. Wanasukumwa kuingia kwa sababu wanaona wengine wanafanya, na ukiwaangalia kwa nje unaona wana mafanikio makubwa kwenye biashara hiyo.

Kama kinachokusukuma kuingia kwenye biashara ni kwa sababu wengine wanafanya na unaona wamefanikiwa, jiandae kushindwa. Hii ni kwa sababu hata uone watu wana mafanikio kiasi gani kwa nje, ndani ya kila biashara kuna changamoto.

Kama unaingia kwenye biashara ambayo huna cha kukutofautisha na wengine, unafanya kile ambacho kila mfanyabiashara anafanya, jiandae kushindwa. Kwa sababu kama watu wanaweza kupata unachotoa kwa wengine, nini kiwasukume kuja kwako?

Ijue biashara vizuri kabla hujaingia, na hata unapoingia endelea kujifunza. Pia hakikisha kipo kitu cha tofauti ambacho unakifanya kwenye biashara. Tofauti na hapo utashindwa, hata kama wengi kiasi gani wanaonekana kufanikiwa kwenye biashara hiyo.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Pale Unapoelekea Kukata Tamaa.

Swali la pili; je unawajua wateja wako, mahitaji yao na unawafikiaje?

Tatizo kubwa sana kwa wanaoanza biashara, wengi huingia kwa mazoea. Kwa sababu wengine wanafanya, basi na wao wanafanya. Mbaya zaidi wanaingia na mtazamo kwamba ukishakuwa na biashara wateja wanakuja tu. Hivyo wanakuwa na biashara ambazo mteja ni mtu yeyote.

Hapo wanashangaa kwa nini biashara zao zinakosa wateja, lakini hawashangai wanaanzaje biashara huku wakiwa hawana mteja wanayemlenga.

Unapoingia kwenye biashara, chagua aina ya wateja ambao unakwenda kuwahudumia, wateja hawa ni watu ambao wana shida, changamoto au uhitaji wa kile ambacho unakitoa. Jua wateja hao wanapatikana wapi na unawafikiaje. Pia jua kwa wale wenye uhitaji ila hawajaijua biashara yako wanajuaje upo na kuja kununua kwako.

Hivyo usifanye biashara kwa mazoea, kufikiri kila mtu ni mteja wako, chagua wateja wa kuwahudumia vizuri. Pia usijidanganye wateja watakuja, zama zimebadilika, wafuate wateja kule walipo. Jua wateja wako wanapatikana wapi na unawezaje kuwafikishia bidhaa na huduma zako, au kuwafikishia matangazo yatakayowafanya wajue na wewe upo.

Swali la tatu; je unaisimamia biashara yako kwa karibu?

Utawasikia watu wengi wanalalamika biashara ni ngumu na zinawashinda, lakini angalia namna wanasimamia biashara zao, utaona ni maajabu kwa wao kuweza kuwa kwenye biashara kwa muda wote huo. Unakuta mtu ni mfanyabiashara, lakini hajui mzunguko halisi wa fedha kwenye biashara yake. Hajui kwa hakika mwezi mzima mauzo, matumizi na faida ni kiasi  gani. Yeye vitu vikipungua ananunua, akiwa na shida anachukua fedha na kutumia.

Kwa mwenendo huo biashara ikipona ni kwa bahati mno. Unapaswa kuwa na usimamizi mzuri sana kwenye biashara yako. Na hatua ya kwanza kabisa ni kuitenganisha biashara na wewe binafsi, wewe ni wewe na biashara yako ni biashara yako, usichanganye vitu hivi viwili.

Unapaswa kuwa na kumbukumbu sahihi za biashara yako. Jua kila fedha kwenye biashara iko wapi, kama imeingia ni kutoka wapi na kama ni kuondoka imeenda wapi. kwa njia hii itakuwa rahisi kwako kujua kama biashara inajiendesha kwa faida au hasara, kabla haijafa.

Biashara huwa hazifi ghafla kama ajali, huwa zinaanza kidogo kidogo, kwa hasara ndogo ndogo. Kwa kuwa wafanyabiashara hawana usimamizi wa karibu, huwa hawalioni hilo haraka na kupelekea biashara kufa kabisa. isimamie biashara yako kwa karibu mno, na utaweza kuiokoa isife.

SOMA; USHAURI; Hatua Muhimu Za Kuchukua Ili Kuondoka Kwenye Madeni Na Kuongeza Kipato Chako.

Swali la nne; je upo tayari kubadilika kwa haraka kiasi gani?

Mabadiliko yalikuwepo, yapo na yataendelea kuwepo. Hiyo ni sheria ya asili na ni vyema ukaifanya kuwa kanuni ya maisha yako. Biashara zinabadilika, hali zinabadilika, mahitaji ya watu yanabadilika. Lakini cha kushangaza, watu wengi wanang’ang’ana kufanya biashara zao kama ambavyo wamezoea kufanya. Na hapo ndipo changamoto kubwa inapoanzia.

Jambo muhimu sana kwenye biashara ni kuyaona mabadiliko kabla hata hayajafika, na kuchukua hatua kabla hayajaleta madhara kwenye biashara yako. Iwapo utakuwa na usimamizi mzuri wa biashara, utaona mabadiliko.

Pia fuatilia tabia za wateja wako, kama unaona vitu fulani havihitajiki kama ulivyodhani, usikazane kuweka vitu hivyo, bali badilika na fuata yale ambayo watu wanahitaji.

Biashara haipaswi kukufurahisha wewe, bali inapaswa kumfurahisha mteja. Hivyo lolote unalofanya, angalia sana wateja wako wanalipokeaje kisha badilika kadiri wateja wanavyoenda.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Swali la tano; je una njia mbadala pale mambo yanapokwenda tofauti na mipango?

Waswahili wanasema mipango siyo matumizi, na hilo lipo wazi kabisa. utajipanga utakavyo kabla hujaingia kwenye biashara, lakini unapoingia, unakutana na mambo mengine mengi ambayo hukuyategemea. Hapo lazima uwe na njia mbadala ya kuhakikisha unaendelea vizuri na biashara yako.

Jambo muhimu sana ni muda wa biashara kuzalisha faida. Watu wengi hutegemea biashara ianze kuzalisha faida haraka baada ya kuianza. Lakini uhalisia haupo hivyo. Biashara huwa zinachelewa kuzalisha faida, kipindi cha mwanzo biashara itakuwa inakutegemea wewe ili kujiendesha. Sasa kama wewe binafsi unategemea kupata fedha a kuishi kutoka kwenye biashara hiyo, haiwezi kupona. Kwa sababu utakachokuwa unafanya ni kutumia mtaji wa biashara, sasa ukishaanza kutumia mtaji, huna tofauti na mkulima anayekula mbegu.

Maswali hayo matano yanatuwezesha kuzitafakari biashara zetu vizuri kabla ya kuzianza na hata baada ya kuzianza, yanatuwezesha kuweka mipango sahihi ya kibiashara na kuchukua hatua haraka pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo yetu. Fanyia kazi maswali haya ili uweze kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog