Nimekua nakuambia hili mara kwa mara, na leo nakukumbusha tena kwamba siyo lazima kila mtu ajiajiri na kuwa na biashara. Lakini kila mtu anapaswa kuwa na mifereji mingi ya kipato, hasa kwa walioajiriwa. Kutegemea mshahara pekee kama njia kuu ya kipato, ni hatari mno, kama ambavyo kila mtu amekuwa anaona kwake mwenyewe na kwa wengine pia.
Lakini pia, kuna kuishi maisha na kuna kusukuma maisha. Naamini kabisa ya kwamba, mtu ambaye anaishi maisha ya kufanya kazi, apate fedha, atumie, ziishe, akope, atumie, apate mshahara, alipe mkopo, akope tena, anafanya hivyo mwaka nenda mwaka rudi, haishi. Badala yake anasukuma maisha.

Sasa hayo hapo juu ndiyo maisha ya waajiriwa walio wengi, haijalishi mshahara ni laki au mamilioni. Mishahara imekuwa haikutani na mara zote haitoshi. Hata ikiongezwa na gharama za maisha nazo zinaongezeka.
Hivyo basi rafiki, ili kuishi, lazima uweze kuwa na uhuru wa kifedha. Lazima uweze kukidhi mahitaji yako na kuwa na uhuru wa kuchagua kipi unataka kwenye maisha yako.
SOMA; BIASHARA LEO; Tengeneza Utegemezi Wa Mteja Kwenye Biashara Yako….
Usisahau pia kwamba madeni ni utumwa, hivyo unahitaji uhuru wa kutokuwa na madeni ya aina yoyote ile.
Sasa zipo njia mbalimbali za kutengeneza mifereji mingi ya kipato, lakini njia nyingine zinahitaji uwe na kiasi kikubwa cha fedha kuanza, ambacho huenda huna kwa sasa.
Lakini njia moja, unaweza kuanza nayo popote pale ulipo, na kwa chochote ulichonacho. Njia hiyo ni kuanzisha biashara, kuanzia chini kabisa na kuitengeneza ikue kwa mafanikio.
Kwa njia hii unatengeneza uhuru wa kifedha na pia kuweza kufanya kile ambacho unakidhibiti kwa asilimia 100.
Uhuru wa kifedha na uwezo wa kuanzia popote ulipo ni sababu muhimu sana kwa kila mtu kuingia kwenye biashara, iwe ni ya bidhaa au huduma. Kuwa na kitu ambacho unakitoa kwa wengine, na wao waone thamani kupitia kitu hicho, waweze kukulipa pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog