Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NANI ANAYEJALI?

Hii ni kauli ambayo huwa inatumiwa na watu waliokata tamaa, watu ambao wapo tayari kuacha chochote ambacho wamekuwa wanakazana kufanya.

Kauli hii pia hutumiwa na wale wasiokuwa waadilifu, wale ambao wapo tayari kufanya chochote bila ya kujali madhara yake kwa wengine.

Wengi wanapofika hatua fulani, huona hakuna anayejali, na hivyo kuchukua hatua ambazo siyo nzuri kwao, labda kuacha wanachofanya au kufanya kitu ambacho siyo sahihi kufanya.

Asubuhi hii napenda kukuambia ya kwamba yupo anayejali, ambaye huwezi kumdanganya au kumficha chochote unachotaka kufanya.

Mtu huyo ni wewe mwenyewe.

Hata ujifiche kiasi gani, chochote utakachofanya kitabaki na wewe, utajua kabisa uliacha au ulifanya kitu ambacho siyo sahihi. Na hali hiyo itakutesa wakati wote wa maisha yako.

Hivyo basi, wakati wowote unapofika hatua ya kukata tamaa au kuwa tayari kufanya lolote ukiamini hakuna anayejali, upo wewe na unajali sana.

Muhimu zaidi, wakati wowote unapokuwa njia panda, unapokuwa huna uhakika ufanye nini, basi fanya lililo sahihi, ambalo upo tayari kuonekana kwa wengine ukiwa unafanya hilo.

Yupo anayejali kwa kila jambo unalofanya, kubaliana naye kwanza kabla ya kufanya jambo lolote.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz