Zipo biashara ambazo huwa zinaanza kwa hamasa na nguvu kubwa. Biashara hizo zinakua kwa kasi sana, watu wanapata mahitaji yao na wanaridhishwa sana. Lakini baada ya muda, biashara hizi zinaacha kuwapendeza watu, zinatoa huduma mbovu na watu kuzikimbia.
Yapo mengi yanayoweza kusababisha hali ya aina hii kwenye biashara, lakini kubwa kabisa ni mahitaji binafsi na mahitaji ya wengine kwenye biashara.

Ninachomaanisha hapa ni hichi;
Watu wengi huanza biashara kwa mahitaji yao binafsi, labda ni changamoto za kifedha, au kutaka kufanya kitu cha ziada. Lakini msukumo mkuu unabaki kuwa kwao binafsi na siyo watu wengine.
Hivyo mwanzo huwa na hamasa kubwa ya kuweka juhudi kwenye biashara hizo, ili kupata kile wanachotaka ndani yao. Kadiri muda unavyokwenda, mambo mawili huweza kutokea;
Moja; watu hao wanapata kile walichokuwa wanataka, sasa binadamu akishapata anachotaka huwa ana tabia ya kujisahau. Na hapa ndipo hamasa inashuka na kuanza kufanya kwa mazoea.
Mbili; watu hao wanakosa kile walichokuwa wanajua watakipata kwa haraka sana, na hivyo wanakata tamaa na kuacha.
Hili ndiyo hupelekea huduma kuwa mbovu mara baada ya biashara kuanza kwa kasi kubwa.
SOMA; BIASHARA LEO; Nenda Zaidi Ya Matatizo Na Mahitaji.
Kuepusha hili, unapaswa kuanza biashara kwa kuangalia mahitaji ya wengine, badala ya kujiangalia wewe mwenyewe pekee, angalia na wale ambao unawapatia kile ambacho unakiuza au kutoa. Hapo unapata hamasa ya kuendelea kutoa kile unachotoa, hata kama umepata au kukosa kile unachotaka.
Hakuna ubaya wowote kuwa na mahitaji binafsi pale unapoanza biashara, kila mtu ana mahitaji binafsi kwenye chochote anachofanya. Shida ni pale mahitaji binafsi yanapokuwa sababu pekee ya wewe kuwa kwenye biashara. Unahitaji kuona kile unachotoa namna kinavyochangia kwenye maisha ya wengine, kuona namna wanavyonufaika na kutatua changamoto zao.
Ukichanganya mahitaji binafsi na mahitaji ya wengine, utaweza kufanya biashara yenye mafanikio makubwa sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog